TAMKO
LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR KULAANI MASHAMBULIZI NA MAUAJI YA
VIONGOZI WA DINI PAMOJA NA KUPINGA KAULI ZA UCHOCHEZI DHIDI YA ZANZIBAR
Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu Mlezi wa Viumbe. Sala na
salamu zimfikie Mtume wetu Mtukufu Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake
waongofu na wote wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya Malipo.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar lililokaa Jumapili tarehe
23/2/2013 katika kikao cha kutathmini matukio ya kushambuliwa na kuuliwa
viongozi wa Dini yakiwemo ya karibuni ya kupigwa risasi na kuuliwa Padri Mushi
pamoja na kupigwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa
Mwakaje na kuendelea kutolewa kwa kauli za uchochezi dhidi ya Zanzibar
linatamka ifuatavyo:
1. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani vikali na kwa
nguvu zote matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini likiwemo tukio
la karibuni la kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi kulikofanywa na wahalifu
wasioitakia mema Zanzibar.
2. Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linapenda kuweka wazi kuwa uhai ni tunu kubwa kutoka kwa
Mwenyezi Mungu aliyotunukiwa binaadamu hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiondoa
haki hiyo isipokuwa yeye mweyewe Mwenyezi Mungu. Kutokana na ukweli huu ndio
maana Sheria za Kiislamu zimeweka wazi mtu mwenye kumuuwa mwenziwe naye auliwe
kama inavyoelezwa katika Kitabu kitufu cha Quran kama ifuatavyo:
“Na humo (katika Taurati) tuliwaandikia ya kwamba mtu (huuwawa kwa sababu ya
kuuwa mtu) kwa mtu, ……….” (5:44)
Hivyo, vitendo vya kiharamia vya
kushambuliwa viongozi wa Dini kulikoanzia kwa kumwagiwa tindi kali Sheikh
Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa
risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali
Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje kwa dhulma kulikofanywa na wahalifu ni jambo
lisilokubalika na Uislamu na Waislamu wenyewe. Aidha wahusika wa matendo haya
wawe wafuasi wa Dini yoyote ile bado watahesabika ni wahalifu kwani vitendo vya
kihalifu na kiharamia kamwe haviwezi kunasibishwa na Dini fulani.
3. Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo husika kufanya upelelezi wa kina kuhusu
matukio haya kwa kuzingatia uadilifu na misingi ya kazi zao ili kuwabaini wahalifu
na kufikishwa katika vyombo vya kisheria. Aidha Baraza linavitahadharisha
vyombo hivyo kuepuka kufanya kazi yao kwa kusukumwa na matashi binafsi, jazba,
chuki, matashi ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Dini pamoja na shindikizo
la baadhi ya vyombo vya habari.
4. Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linalaani na kupinga kwa nguvu zake zote kauli aliyoitoa
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania na baadhi ya vyombo vya habari kuihusisha
Zanzibar na ugaidi kutokana na tukio la kuuliwa Padri Mushi. Kauli hii
inaonesha kuwa Mheshimiwa Waziri anaibagua Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwasababu tunavyoelewa sisi suala la usalama wa nchi ni suala la
Muungano hivyo huwezi kuihusisha Zanzibar pekee na suala la ugaidi. Hivyo,
Baraza linaona kuwa kauli hizi zinazotolewa ni mbinu za makusudi za kuichafua
Zanzibar katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na chuki binafsi dhidi ya
Zanzibar na watu wake.
5. Aidha Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linamtaka Mheshimiwa Waziri kwa kulinda heshima yake
kuwajibika kwa Watanzania kwa kujiuzulu kutokana na kushindwa kulinda usalama
wa wananchi wakiwemo viongozi wa Dini ambao ndio walezi wa jamii.
6. Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linalaani kauli za uchochezi zinazoendelea kutolewa na baadhi
ya vyombo vya habari zinazochochea chuki, uadui, hasama na mtafaruku kati ya
Waislamu na Wakristo na kusahau kuwa Waislamu wameishi na Wakristo kwa amani,
mapenzi na mashirikiano hapa Zanzibar karne na karne. Baraza linaona kuwa vyombo
hivyo vya habari vinatekeleza ajenda ya kuivuruga Zanzibar kwa kuchochea vita
vya kidini ili kufikia malengo yao wanayoyajua wenyewe. Hivyo, Baraza linaiomba
Serikali kuvidhibiti kwa kuvichukulia hatua vyombo vyote vinavyotumia matukio
haya kuchochea uadui na chuki kati ya Waislamu na Wakristo.
7. Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo vya habari vya Zanzibar kuwajibika kwa
Wazanzibari wanaolipa kodi kwa kuwapasha taarifa sahihi juu ya matukio muhimu
yanayotokea katika jamii yao badala ya wananchi kutegemea kupokea taarifa za
upotoshaji na uchochezi kutoka katika vyombo vya habari visivyotutakia mema.
8. Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linaziomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kuwasilisha kwa Watanzania taarifa ya
wazi ya matokeo ya uchunguzi wa matukio haya kwa kuanzia na lile la kumwagiwa
tindi kali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri
huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga
na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje.
9. Baraza la Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Zanzibar linawaomba Wazanzibari wote kuwa watulivu katika kipindi
hichi ambapo upelelezi wa matukio haya ukiendelea. Aidha Baraza linawasihi
Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti zao za kidini kulinda umoja wao na
kudumisha amani pamoja na kukataa kugawanywa ili kuwatoa katika ajenda yao ya
msingi ya kudai Mamlaka Kamili ya Zanzibar katika Muungano.
MOLA WETU MTUKUFU TUNAKUOMBA UINUSURU ZANZIBAR NA WATU WAKE DHIDI YA MAADUI WA
NDANI NA NJE WASIOITAKIA MEMA NCHI YETU
Imesainiwa na:
Sheikh Ali Abdalla Shamte
Amir wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar