Zakaatul-Fitwr, 'Iydul-Fitwr Na Swawm Ya Sittatush
Shawwaal
Tunakaribia kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhaan na mambo matatu
yafuatayo ya muhimu yanayotukabili yanapasa kuzingatiwa ili tukamilishe Swawm
zetu ipasavyo na tupate fadhila zake.
1- ZAKAATUL-FITWR
Inaitwa Zakaatul-Fitwr (Zakaah ya Kufuturu au Kufutari) kutokana
na kumalizika Swawm ya Ramadhaan. Imefaridhiwa mwaka wa pili wa Hijrah katika
mwezi wa Ramadhaan.
Hikmah Yake
Ni kutwaharisha Swawm ya Muislamu kutokana na maneno machafu, ya
upuuzi wakati alipokuwa amefunga kwa kulisha maskini chakula ili nao wapate
chakula kizuri siku ya ‘Iyd.
Ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kuswali Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr. Dalili ifuatayo inathibitisha:
Ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kuswali Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr. Dalili ifuatayo inathibitisha:
عَنْ ابْنِ عَبَّاس ٍقَالَ فَرَضَ رَسُولُ
اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ طُهْرَةً
لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا
قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ
فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ . " رواه أبو داود بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ .
Kutoka Ibn ‘Abbaas
(Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Mtume amefaridhisha Zakaatul-Fitwr
kuwa ni twahaara ya mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, na
kulisha masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalah basi hiyo ni Zakaah
iliyotakabaliwa, na atakayeitoa baada ya Swalah basi hiyo ni miongoni mwa
sadaka” [Abu Daawuud kwa isnaad iliyo nzuri].
Na ndio kusudio ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((قَدْ
أَفْلَحَ مَن تَزَكَّى))
((وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّى))
((Hakika amekwishafanikiwa
aliyejitakasa)) ((Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akaswali)) [Al-A’laa: 14-15]
‘Umar bin ‘Abdul-Aziyz alikuwa akiamrisha watu kutoa Zakatul-Fitwr
na huku akisoma Aayah hizo tukufu.
Wakati Unaowajibika Kutoa
Kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhaan hadi asubuhi
kabla ya Swalah ya ‘Iydul-Fitwr. Inaweza pia kutolewa siku mbili tatu kabla.
Mtoto atakayezaliwa siku hiyo kabla ya kuzama jua imewajibika kutolewa
Zakaatul-Fitwr.
Anayewajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr Na Kitu Gani Cha Kutoa
عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَال فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ
الْفِطْرِ صَاعًا مِنْ تَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ
وَالْحُرِّ وَالذَّكَرِ وَالأُنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ
الْمُسْلِمِينَ وَأَمَرَ بِهَا أَنْ تُؤَدَّى قَبْلَ خُرُوجِ النَّاسِ إِلَى
الصَّلاةِ . صحيح البخاري
Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma): "Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa
mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa
Waislamu kwa kutoa swaa'* moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri, na
akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-'Iyd)" [Al-Bukhaariy]
- swaa’ moja = kilo mbili na nusu hadi tatu au (mteko) viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne.
Kinachotolewa Ni Chakula Kinachotumika Na Watu Katika Nchi:
عن أبي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ رَضِيَ اللَّهُ
عَنْهُ قَالَ "ُكُنَّا نُعْطِيهَا فِي زَمَانِ
النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَاعًا مِنْ طَعَامٍ أو صَاعاً من
الشعير, أو صاعاً من تَمر, أو صاعاً من زَبيب، أو صاعاً من أقِط البخاري
Abu Sa'iydil-Khudriyy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema:
"Tulikuwa tukitoa zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) swaa’
moja ya chakula, au swaa’ ya shayiri au swaa’ ya tende au swaa’ ya zabibu au
swaa’ ya aqit" (mtindi mkavu) (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao
zama za hizo) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho kuhusu mas-alah
mbali mbali ya Zakaatul-Fitwr:
2- ‘IYDUL-FITWR
Inaitwa ‘Iydul-Fitwr (‘Iyd ya kufuturu au kufutari) kutokana na
Waislamu kumaliza funga ya Ramadhaan. Hivyo haifai kufunga Swawm siku ya ‘Iyd,
bali ni sikukuu ya Waislamu ya kusherehekea, kufurahi kwa kila njia zilizomo
katika mipaka ya Dini.
a) Apasayo Kufanya Muislamu Yaliyo Sunnah
Kuoga Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali
فقد صح في الموطأ وغيره أَنَّ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ
عُمَرَ كَانَ يَغْتَسِلُ يَوْمَ الْفِطْرِ قَبْلَ أَنْ يَغْدُوَ
إِلَى الْمُصَلَّى
Imethibitika katika Muwattwaa na vitabu vinginevyo kwamba
‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akioga siku ya
‘Iydul-Fitwr kabla ya kwenda Muswallaa.
Kujipamba Na Kuvaa Nguo Nzuri
وعن جابر رضي الله عنه قال : كان للنبي صلى الله
عليه وسلم جبة يلبسها للعيدين ويوم الجمعة . صحيح ابن خزيمة
Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Mtume
alikuwa ana jubbah akilivaa siku za ‘Iyd mbili na siku ya Ijumaa” [Swahiyh Ibn
Khuzaymah]
Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akivaa nguo zake
nzuri kabisa siku ya ‘Iyd.
Kwa hiyo inapasa kujipamba kwa nguo nzuri, na manukato mazuri. Ama
wanawake hawapasi kujipamba na kudhihirisha mapambo yao ikiwa ni mavazi au
kujipaka vipodozi na pia hawapaswi kujitia manukato na kutoka nje. Wanaweza
kudhihirisha yote hayo mbele ya Maharimu zao tu.
Kula
Tende Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ كَانَ رَسُولُ
اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لا يَغْدُو يَوْمَ الْفِطْرِ حَتَّى
يَأْكُلَ تَمَرَاتٍ .. وَيَأْكُلُهُنَّ وِتْرًا . البخاري
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu
‘anhu) ambaye amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuwa hatoki kwenda kuswali Swalah ya ‘Iyd ila baada ya kula tende… na akila
kwa hesabu ya witr. [Al-Bukhaariy]
Hii ni kwa sababu haifai kufunga siku hii
ya ‘Iyd. Asiyepata
tende anaweza kula kitu chochote.
Ama katika 'Iydul-Adhwhaa ni Sunnah
kutokula kabla ya kwenda Msikitini, na anaposhuka baada ya Swalah ni bora kitu
cha kwanza kula ni ile nyama ya Udhwhiyah (mnyama aliyechinjwa) ikiwa
itapatikana.
Kuleta
Takbiyrah Kwa Sauti
Sunnah kuu katika ‘Iyd kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa
Ta'ala):
((وَلِتُكْمِلُواْ
الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ((
((na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongoeni
ili mpate kushukuru)) [Al-Baqarah: 185]
Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam) alikuwa akileta Takbirah mpaka anamaliza Swalah. [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Matamshi Ya Takbiyrah
الله أكبر الله أكبر لا إله إلا الله والله أكبر الله أكبر ولله الحمد
Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa Allaah,
WAllaahu Akbar Allaahu Akbar wa Lillaahil Hamdu
Wakati wa Takbiyrah
Unaanza usiku wa ‘Iyd mpaka anapoingia Imaam kuswalisha Swalah ya
‘Iyd
Kupongezana
Ni vizuri kupongezana siku ya ‘Iyd baina ya Waislamu, kuzidisha
mapenzi baina yao. Na ilivyo Sunnah ni kusema kama walivyokuwa wakiambiana
Maswahaba wanapokutana siku ya ‘Iyd ni kusema:
'Tuqubbila Minna wa Minka’ au ‘Taqabbala Allaahu Minnaa wa Minkum’.
Kuelekea Katika Muswallaa Kwa kutembea Na Kurudi Kwa Njia Nyingine
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ رَضِيَ اللَّهُ
عَنْهُمَا قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا كَانَ يَوْمُ عِيدٍ خَالَفَ الطَّرِيقَ . رواه البخاري
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambaye
amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akibadilisha njia
siku ya ‘Iyd”
[Al-Bukhaariy]
Hikmah yake ni kwamba njia hiyo itashuhudia siku ya Qiyaamah na
ardhi itazungumza yote ya kheri na shari anayotembelea mja juu yake. Pia
kudhihirsiha Uislamu katika njia mbili, pia kukutana na watu tofauti na
kuwasaidia kwa njia yoyote.
Kuswali Swalah ya ‘Iyd Katika Muswallaa
Ni Sunnah bali, ni waajib kwani Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliamrisha watu wote watoke kwenda kuswali:
عَنْ أُمِّ عَطِيَّةَ رضي الله عنها قَالَتْ "أَمَرَنَا تَعْنِي النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نُخْرِجَ فِي الْعِيدَيْنِ الْعَوَاتِقَ وَذَوَاتِ الْخُدُورِ وَأَمَرَ الْحُيَّضَ أَنْ يَعْتَزِلْنَ مُصَلَّى الْمُسْلِمِينَ" مسلم
Kutoka kwa Ummu ‘Atwiyyah (Radhiya Allaahu
‘anhaa) kwamba: “Ametuamrisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) tutoke katika ‘Iyd mbili vijana na vikongwe na kaamrisha wanawake wenye
hedhi wajitenge katika Muswallaa” [Muslim]
b) Yaliyo Bid’ah Katika ‘Iyd
Kuleta Takbiyrah Kwa Pamoja Katika
Misikiti Na Muswallaa
Inavyopasa ni kila mtu kuleta Takbiyrah
pekee.
Kutembelea Makaburi
Imekuwa ni ada ya baadhi ya watu
kutembelea makuburi siku za ‘Iyd. Jambo hili halikufanywa na Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa sallam) wala Maswahaba zake. Mtu anaweza uzuru makaburi siku
yoyote na si kutenga siku ya ‘Iyd kwa jambo hilo na hadi kugeuka kuwa ni katika
Sunnah za ‘Iyd hivi leo.
Maamkizi Ya Kuiga Makafiri
Kupelekeana kadi na zawadi kama wafanyavyo
makafiri, haipasi kuwaiga kwani ni jambo tulilokatazwa katika dini na tuwe na
fakhari na mila na desturí zetu.
c) Yaliyo Maasi
Kunyoa Ndevu
Kunyoa ndevu hasa kwa makusudi ya
kukusudia ‘Iyd kwa kudhani mtu anapendeza akifanya hivyo ilihali anavunja
shari'ah na kupingana na Sunnah za Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam).
Wanawake Kutokutimiza Hijaab zao za kishari'ah na kudhihirisha mapambo yao mbele
ya wasio Maharimu wao.
Sherehe Za Maasi
Kuchanganyika wanawake na wanaume (party)
na kuwekwa muziki, vyakula na vinywaji vya haraam na kupeana mikono wanawake na
wanaume.
((لأَنْ
يُطْعَنَ فِي رَأْسِ أَحَدِكُمْ بِمِخْيَطٍ مِنْ حَدِيدٍ خَيْرٌ لَهُ مِنْ
أَنْ يَمَسَّ امْرَأَةً لا تَحِلُّ لَهُ))
Mtume (swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) amesema:
“Ni bora kwa mwanaume kupigwa sindano katika kichwa chake kuliko
kuushika mkono wa mwanamke ambaye si halali yake.” [Silsilat
Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh
Al-Albaaniy]
Wanawake wanaruhusiwa kuimba Nashiyd siku
za ‘Iyd wakiwa peke yao au mbele za Maharimu wao.
Kufanya Israaf ya chakula na mali badala ya kuwasaidia masikini na mafakiri
3- SWAWM YA SITATUSH SHAWWAAL
Swawm hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa
Ramadhaan na siku ya 'Iyd ul Fitr. Ni Sunnah iliyo na fadhila kuu kwani thawabu
zake ni sawa na thawabu za mtu kufunga mwake mzima kama alivyosema Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
((
من صام رمضان ثم أتبعه ستًّا من شوال كان كصيام الدهر)) أرجه مسلم في صحيحه،
((Atakayefunga Ramadhaan kisha akafuatiliza na
siku sita za mwezi wa Shawwaal itakuwa kama ni funga ya mwaka)) [Muslim]
Hesabu ya kuwa mwaka mzima ni kutokana na kauli ya Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala):
((مَن
جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ
يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا وَهُمْ لاَ يُظْلَمُون))
((Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi.
na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa)) [Al-An'aam:160]
Na kauli ya Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((إن
الله كتب الحسنات والسيئات , ثم بين ذلك , فمن هم بحسنة فلم يعملها كتبها الله له
عنده حسنة كاملة فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له عنده عشر حسنات , إلى سبعمائة
ضعف , إلى أضعاف كثيرة , ومن هم بسيئة فلم يعملها , كتبها الله عنده حسنة كاملة ,
فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له سيئة واحدة )) متفق عليه ،
((Allaah Ameandika mema na mabaya. Kisha
Akayabainisha. Basi atakayetia nia kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa
jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi
kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia nia kufanya kitendo kibaya kisha
asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya ataandikiwa
dhambi moja))
[Al-Bukhaariy ya Muslim]
Maulamaa wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka mzima
kwa atakayefunga Ramadhaan na siku sita hizo za Shawwaal, kwa kusema: Jambo
zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhaan
atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za
Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300 + 60 = 360, mtu
atapata hesabu ya mwaka mzima.
Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga
Swawm hii ndugu zangu.
Tunawaombea Waislamu wote wajaaliwe kumaliza mwezi Mtukufu wa
Ramadhaan kwa kheri na mafanikio, watakabaliwe Swawm zao, na madhambi
kughufuriwa, waweze kutoa Zakaatul-Fitwr za kutakasa Swawm, Wawe na ‘Iyd ya
furaha na uwezo wa kufunga Sitatush Shawwaal.
Taqabballa Allaahu Minna wa Minkum
Kwa msaada wa: www.alhidaaya.com
No comments:
Post a Comment