Thursday, February 14, 2013

KIFO CHA SHEIKH NASSOR ABDALLAH BACHO

Marehemu Sheikh Nassor Abdallah Bacho
 
TAFAKURI   YA  KIFO  CHA SHEIKH   NASSOR BACHU KILICHOTOKEA  ZANZIBAR TAREHE 13/2/2013.

Na  PAZI  MWINYIMVUA 

 INNA  LILLAHI  WA INNA ILLAIHI  RAJI-UUN. 



Mfahamu sheikh Nassor Bachu
Sheikh Nassor Bachu ni miongoni mwa masheikh maarufu ambaye makazi yake yalikuwa katika visiwa vya zanzibar. Ni miongoni mwa walimu ambaye ana wanafunzi wengi mno ambao msimamo wao mkubwa ni kufuata na kuhuisha sunna za Mtume Muhammad,  Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, amin.
Mchango wake katika jamii 

Katika maisha yake alikuwa akitoa darsa zake katika msikiti uliopo Rahaleo na msikiti wa Kikwajuni Zanzibar. Alipitisha maisha yake yote katika kufundisha masomo mbalimbali ya dini kama vile tafsiri za quran, hadithi na pia alikuwa na kipaji cha ziada cha kuzungumza na kueleweka kwa ufasaha. Hivyo pia ni miongoni mwa watoa mawaidha wazuri sana ambaye  kanda zake za mawaidha za redio na za video zinapatikana katika maduka mingi wanayouza kanda za dini. Pia unaweza kupata mawaidha yake kwa kupitia www.sekenke.com au tafuta kwenye www.mawaidha.com
Kwa muda kidogo alipata fardhi ya ugonjwa na hadi kukamilisha safari ya maisha yake leo siku ya tarehe 13/2/2013.
Nini tutafakari?
Kwanza napenda kunukuu maneno ya Mtume SAW aliposema katika zama za mwisho wanazuoni  wengi watapungua na maasi yatazidi.
 Ni ukweli usiopingika si rahisi kupata watu wenye ilmu kubwa kama ya sheikh wetu.
Ni wangapi wako tayari kutumia muda wao kutafuta ilmu ya dini kwa manufaa yao wenyewe sembuse kupata muda wa kuwafundisha wengine?
Ni nani yuko tayari walau kutumia saa chache kwa ajili ya kutafuta ilmu na kuweza kutumia ilmu hiyo kwa ukweli namaanisha kwa ikhlasi.
  Ibada zetu zimekuwa za kubabaisha? Kwa kuwa hatuna ufahamu wa kutosha juu ya ibada mbalimbali. Hii ni kwa sababu hatujajipangia muda wa kuhudhuria katika madrasa na kuweza kupata ilmu sahihi.
Watoto wetu tumewapangia program ambazo hawapati hata muda wa kujifunza dini yao na kumjua mtume SAW. Matokeo yake  ni mmomonyoko wa maadili.
Digrii , Masters na PHD zetu zimekuwa ni bure kwani tunashindwa hata kufanya ibada ya kutafakari na kuweza kuona  na kuthibitisha neema za Allah ambazo amezitaja katika quran pamoja na  kuhofishwa na azabu zake. Tumekuwa mstari wa mbele  wa kutaja na kueneza aibu za watu kuliko kuangalia wapi tumekosea na turekebishe.
 Hatujiulizi kwa nini?  Na mambo haya mpaka lini? Tutaanza kuisoma dini yetu lini? Masheikh wetu ndugu zangu ndio hao wanamalizika. 
Naguswa na msiba huu  sana kwa sifa za kipekee alizonazo Sheikh Nassor Bachu. Machozi hayatasaidia japo nalo hili huwezi kulizuia.
Mtu mmoja maarufu alisema wakati wa kiza kinene ndio wakati wa kutafakari na kuweza kuona mwanga. Aristotle. Tafadhali TAFAKARI.
Martin Luther anasema "Laiti kama ningejua kuwa kesho dunia yote itakatika  kuwa vipande basi nisingeacha  kupanda mti wa mtufaha". Andaa maisha ya kesho  akhera hata kama u mgonjwa kitandani au upo kifungoni NA usichoke kupanda mti wa KUTAFUTA  ilmu kwani faida zake ni nyingi.
Mtume SAW amesema
Ishi duniani kama utaondoka kesho na ishi duniani kama utabaki milele. Mihangaiko ya kutafuta maisha ni miongoni mwa sehemu ya dini lakini iendane na kutafuta  maisha ya akhera.
Na Allah SW anasema
Natunawapa muda wa kutosha lakini watambue hakika nguvu yetu ni kali? Fanya ufanyavo lakini ujue huwezi kushindana na nguvu za Allah.
Pia anasema; Kila binadamu hufanya makosa lakini mbora ni Yule anaetubia. Tufanye haraka kuomba msamaha na kutorudia makosa.
Katika aya nyingine anasema waja wema wanapofikwa na msiba husema hakika sisi tunatoka kwa Allah na kwake yeye tutarejea.
Nasi tuseme INNA LILAHI WA INNALAYHI RAJIUN. 

1. Ombi langu kwako tafuta kanda yeyote ya  mawaidha ya Sheikh Nassor Bachu katika website nilizozitaja ukurasa wa kwanza ili thawabu ziendelee kumuendea sheikh wetu na pia uweze kufaidika na ilmu yake.
 
2.     Tumia walau dakika chache kumuombea dua na kumtakia msamaha kwa Allah na amfanyie wepesi  wa hesabu zake katika safari ya maisha mapya. Allah alitie nuru na harufu njema kaburi lake. Amin. Amin
 
3.     Nasi pia tujiombee Allah atupe maisha mema ya duniani na akhera na atupe mwisho mwema.

Habari ni kwa hisani ya
NYAMBONGONAMZILIMITI
http://nyambogonanzilimiti.blogspot.com/

1 comment:

Anonymous said...

Wallah umenifanya huzuni yangu irud upya,siku niliyoona mazishi yake nililia sana,huyu ni shekhe wangu natamani hata angekua wang peke angu,NINAMPENDA.nilianza kumrecognize alikua tayar marehem lait angekua hai basi ningemvisit,kwani NINAMPENDA. Kwa ajili ya ALLAH. Amenifundisha namna ya kupay attention kwenye swala ad leo najivunia swala zangu Alhamdulillah lakin pia amenifundisha azkar nzito nzito,wallah Alhamdulillah kupitia audio zake utube.Nimedownload karbun mawaidhayake yoote ya utube. Allah amrehem shekh wetu,na atukutanishe nae ktk viwanja vya peponi amiin.