Toleo la 280
6 Feb 2013, RAIA MWEMA
- Nyama zadoda buchani, wanunuzi wapungua.
ULE usemi wa Kiswahili kwamba mbuyu
ulianza kama mchicha unaonekana kusadifu katika mgogoro unaohusisha haki ya
kuchinja wanyama na ndege kwa ajili ya kitoweo unaoendelea Mwanza na Geita kati
ya waislamu na wakristo.
Tayari Umoja wa Makanisa ya Kikristo
Jijini Mwanza umetoa tamko la kupinga msimamo wa serikali kuwa wenye haki ya
kuchinja kwa ajili ya kuwauzia wananchi ni waislamu na wakristo wanaweza
kuchinja majumbani mwao tu.
Kwa mujibu wa tamko hilo, kitendo
cha serikali inayosema haina dini kuwalazimisha wakristo kufuata ibada ya dini
isiyokuwa ya imani yao ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ibara ya 19 kifungu cha 1 na 2, inayotoa uhuru wa kila mtu kuwa na uhuru wa
kuabudu na kwamba suala la imani ya dini ni jambo binafsi na hiari ya mtu
kulifuata.
Tamko hilo limewataka wakristo
kutokula nyama zilizochinjwa kinyume na imani yao, kwa kuwa tendo la kuchinja
ni sehemu ya ibada kwa waumini wa dini ya kiislamu tofauti na walivyokuwa
wakifiriki mwanzoni kwamba tendo hilo halina uhusiano wowote na ibada na hivyo
hawaoni sababu ya kuendelea kushirikishwa katika ibada isiyokuwa ya imani yao.
“Kwa
kuwa sasa imebainika kuwa tendo la kuchinja kwa wenzetu waislamu ni sehemu ya
ibada kwa mujibu wa imani yao, tofauti na tulivyokuwa tukidhani hapo awali kuwa
tendo la kuchinja halina uhusiano wowote na mambo ya ibada. Sisi wakristo
hatuoni sababu ya kuendeea kushirikishwa katika ibada ya imani isiyotuhusu.
Tunatoa wito kwa wakristo wote kuanzia sasa kutokula nyama zilizochinjwa
kinyume na imani ya kikristo” ilisema
sehemu ya tamko hilo lililotiwa saini na Askofu Charles Sekelwa ambaye
ni mwenyekiti wa Umoja huo na katibu Mchungaji wake Jacob Kituu.
Katika kuonyesha uthabiti wa msimamo
wao wachungaji na maaskofu walikutana Jumamosi iliyopita katika Parokia ya
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Kirumba chini ya kamati ya Ulinzi na Mwasialiano ya
Umoja huo na kuazimia kuwatangazia waumini wao katika makanisa yote kususia
kununua nyama kwenye mabucha katika kipindi chote ambacho watakuwa hawajapata
machinjio yatakayowawezesha kuchinja kwa imani yao.
Tangazo hilo ambalo lilitolewa
Jumapili iliyopita limeanza kuathiri biashara hiyo, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa
Umoja wa wenye Mabucha Jijini Mwanza, Joshua Machage, biashara yao
imeathirika sana kwa kuwa hata waislamu wanaogopa kununua kwenye mabucha ya
wakristo kwa kuhisi kwamba watakuwa wamejichinjia.
“Tatizo hili ni
kubwa, kuna wanachama wangu wameleta taarifa hapa kuwa biashara haiendi kabisa
kwa sababu ya mvutano huu, wakristo jana (Jumapili) wametangaziwa kutonunua
nyama zinazochinjwa na watu wasiokuwa wa imani yao sasa hali ni mbaya sana
kwenye biashara yetu, nyama zimesimama kabisa hali ni mbaya,” alisema Machage.
Mgogoro huo umeendelea kushika kasi
pamoja na serikali kumtuma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uratibu na Sera, Steven
Wassira, kusuluhisha mgogoro huo, ambaye katika kikao chake na viongozi wa
dini hizo mbili alisisitiza msimamo wa serikali ambao ulikuwa umetolewa awali
na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo huko Nyehunge, Sengerema
ambako ndiko mgogoro huo ulikoanzia.
Sheikh wa Wilaya ya Sengerema, Ahmed
Jaha Ally aliliambia Raia Mwema kwamba kwa mtazamo wa wengi na imezoeleka
katika jamii kwamba muislamu hali asichochinja na kwamba mkristo akichinjia
nyumbani kwake akala mwenyewe hilo haliwasumbui lakini akafafanua zaidi.
“Hilo la kuchinja
nyumbani halina tabu, lakini wakichinja na kuanza kuweka kwenye mabucha hapo
kunakuwa na shida kwa sababu wanaweza kununua watu wenye hoteli na kwenda
kuuza, sasa akila muislamu kwenye hoteli hiyo itakuwa siyo haki, kwa sababu kwa
mujibu wa maelekezo ya dini yake hapaswi kula kisichochinjwa na muislamu, ” alisema.
Akijibu kuwa kuchinja ni ibada na
hivyo wasiokuwa waislamu wanashiriki ibada isiyo ya imani yao alisema kuwa
hawawashirikishi wakati wa ibada na kwamba kula nyama ile si kushiriki ibada
hiyo kwa kuwa hiyo inamhusu mchinjaji.
“Kwa kula tu hushiriki hiyo ibada
kwa sababu inamhusu mchinjaji, kwa hiyo hatuwashirikishi lakini ndugu zetu pia
wakumbuke tunavumiliana katika mambo mengi, Ijumaa ni siku ya kazi lakini
Jumamosi na Jumapili ni siku za mapumziko na sisi tumekaa kimya, kwa hiyo haya
mambo yanahitaji kuvumialiana” alisema Sheikh Ally.
Mwandishi wetu alipotembelea Ofisi
ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza kutaka kujua msimamo wa Baraza hilo katika hali
inayooendelea hivi sasa mkoani hapa kiongozi aliyemkuta ofisni hapo alisisitiza
kuwa wao hawana cha kuongeza wala kupunguza kwa kuwa msimamo ulishatolewa na
Waziri Wassira.
“Sisi hatuna cha kuongeza wala
kupunguza, msimamo ulikwishatolewa siku ile, wewe si ulikuwapo? Ehee! Kama
ulikuwapo basi sisi hatuongezi wala kupunguza kwenye hilo, na wala usininukuu,
kama wao wakristo wanalo la kusema ni wao na serikali” alisema kiongozi huyu
ambaye alikataa kunukuliwa gazetini.
Hayo yakiendelea mkoani Mwanza, hali
si shwari pia mkoani Geita ambako uchunguzi wetu umebaini kuwa maaskofu wa Mkoa
huo walikaa kikao siku ya Jumamosi wiki jana katika ofisi ya Jimbo Katoliki
Geita ili kujadili suala hilo.
“Kikao hicho kilikuwa na dhamira ya
kutoa tamko la kuwataka wakristo kutokula nyama zinazochinjwa na watu wasiokuwa
wa imani yao na kulikuwa na mkakati wa kukubaliana kuwa na bucha au machinjio
yao kwa kuwa wanaamini serikali imeamua kuegemea upande mmoja wa suala hilo,”
kilisema chanzo chetu kuhusu kikao hicho cha maaskofu.
Imeelezwa kuwa hata viongozi wa
kikristo walioungana na msimamo wa serikali wakati wa ziara ya Wassira
walishawishiwa na serikali mkoani humo ili kuwasaliti wenzao.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Said Magalula, alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba katika kikao hicho na
Waziri Wasirra viongozi wote wa dini walikubaliana na wakatoa tamko hilo.
“Kile kikao kile kilikuwa kati ya
waziri na viongozi wa dini zote na si maaskofu tu, wale waliosema ni watu
wazima na wana heshima zao na ni viongozi wazito, wanawezaje kuhujumiwa? Lakini
hoja hapa ni kwamba walikubaliana wakaelewana kama walishawishiwa hilo si hoja”
alisema mkuu huyo wa Mkoa.
Maslahi ya Uchumi yahusishwa
Pamoja na kuhusishwa na imani, suala
hilo pia limekuwa likitazamwa kwa mtazamo wa kiuchumi hasa kwa kuzingatia kuwa
hiyo ni sehemu ya ajira kwa watu wanaohusika na shughuli ya uchinjaji kwa hiyo
upo uwezekano mkubwa wa hilo kuchangia katika sintofahamu hii inayoendelea.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu hoja
hiyo iliibuka katika kikao cha wachungaji Jumamosi wiki iliyopita jijini Mwanza
ambako inaelezwa kuwa mtoa hoja mmoja alisema kuwa suala hilo limekuwa
likiwanufaisha waislam kiuchumi wakati wamekuwa mstari wa mbele kuutukana na
kuikashafu imani ya kikristo.
“Iliibuka hoja humo kwamba kila
ng’ombe anayefugwa na mkristo anamuhakikishia muislamu shilingi elfu tano
wakati wa kuchinja na katika hizo, shilingi elfu moja inachangwa msikitini na
kwamba pamoja na yote hayo imani ya kikristu imekuwa ikikashfiwa bila serikali
kufanya kitu, mtoa mada akasisistiza kuwa kuendelea kuchinjiwa na waislamu ni
kuendelea kufadhili kukashifiwa kwa imani yao na kwa kuwa serikali imechukua
upande katika hili ni bora wajisimamie,” kieleleza chanzo chetu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wenye
Mabucha Mwanza Machage anasema kuwa zamani kuchinjiwa ilikuwa ni kama huduma na
ilikuwa ni bure pengine ndiyo maana hakukuwa na kelele za namna hii lakini sasa
hivi imekuwa ni biashara.
“Chama change, kwa mfano, tunalipa
karibu shilingi milioni moja au zaidi kwa mwezi kwa ajili ya kuchinjiwa, sasa
hii ni biashara kubwa ndiyo maana hata serikali inatakiwa kuliangaliwa kwa
umakini mkubwa suala hili si kulichukua juu juu tu kama inavyofanya, kwa sababu
yakiingia masuala ya kibiashara inakuwa si haki kusema wengine wana haki na
wengine hawana haki” alisema.
Ndikillo, Wassira wanyooshewa kidole
Mtazamo wa wengi ni kwamba suala
hili limefikishwa hapa lilipo na serikali yenyewe hasa kauli zilizokuwa
zikitolewa na Mkuu wa Mkoa Ndikillo huko Nyehunge wakati wa sakata hilo na
kitendo cha Waziri Wassira kuunga mkono ikaonekana anakubaliana na kila kitu
alichosema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
“Hili suala limekuzwa na Mkuu wa
Mkoa na kauli zake za kejeli na dharau, alipokuja Nyehunge wakati wa mazungumzo
ya mvutano ule, badala ya kutulia na kulichunguza jambo kwa undani alipoona
hakuna maelewano alitoa amri tu kwa Polisi kuwa mkristo yeyote akichinja tia
ndani, hilo liliwakwaza viongozi wa kikristo, uhalali wa amri hiyo ulikuwa
unatokana na sheria ipi?” anahoji Mwinjilisti Ernest Charles wa Kikundi cha
Biblia ni Jibu ambaye alishiriki katika kikao hicho.
Akizungumza na Raia Mwema mzee mmoja
kutoka Nyehunge ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kuwa tangu aanze
kujitambua hajawahi kuona kiongozi anashughulikia suala la mgogoro wa dini kwa
jinsi alivyofanya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
“Mwanangu mimi sasa nina miaka 74,
viongozi huwa wanakuwa na hekima na busara. Watu wakifarakana kwenye mambo ya
dini yanatakiwa mazungumzo ya muda mrefu.
“Mkuu wetu alipokuja kwa kufoka na
kutoa amri hapo aliharibu. Mambo haya yanatakiwa watu wakae na kuyazungumza
tena na tena,” alieleza mzee huyo.
Chimbuko la mgogoro
Pengine Mwezi Mei mwaka jana ndiyo
unaweza kuelezwa kuwa ndipo vuguvugu hili lilipoibuka wakati wa mazishi ya mzee
Kamuli ambaye alikuwa muumini wa Kanisa la African Inland Church of Tanzania
(AICT) Nyehunge.
Inaelezwa katika msiba huo ya kuwa
mchungaji wa eneo hilo, James Lutambi, alichinja ng’ombe kwa ajili ya msiba
huo.
Inaelezwa ya kuwa waislamu
waliohudhuria msiba huo walipofika walihoji nani amechinja, wakaambiwa ni
mchungaji. Wakataka kujua kwanini amechinja, yakatokea majibizano kidogo lakini
waislamu hao waliondoka na kisha wakamwandikia mtendaji wa kijiji barua ya
kutangaza kujitenga kushirikiana na wakristo katika misiba na sherehe, baada ya
tangazo hilo, wakristo nao wakaamua kuwa na bucha yao.
Agosti 27, 2012 Umoja wa Wakristo
Nyehunge ulimwandikia barua Afisa Mifugo wa Wilaya yenye kumbukumbu namba UMK/
NY/01/05 wakiomba idhini ya kuchinja katika machinjio ya Nyehunge.
Katika kujibu barua hiyo Afisa
Mifugo alimwandikia mtendaji wa kijiji cha Nyehunge barua yenye kumbukumbu
namba VYE/SENG/V.10/11/131 ya tarehe 02, Oktoba 2012 akimtaka kuitisha vikao
vitakavyosaidia kupatikana muafaka juu ya uchinjaji wa wanyama katika machinjio
ya Nyehunge, ambayo iliambatana na ufafanuzi mbalimbali wa kisheria kuhusu
uchinjaji.
“Uchinjaji na ukaguzi wa wanyama kwa
ajili ya kuuza kwa wananchi unafanyika chini ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama
ya mwaka 2003 pamoja na kanuni ya mwaka 2007. Kifungu cha 7 sheria inatamka
kuwa uchinjaji wa wanyama kwenye machinjio zilizoidhinishwa na serikali
unafanywa kwa misingi ya imani za kidini inayokubalika na jamii husika. Sheria
na kanuni zake haitamki wazi muumini wa dhehebu gani aruhusiwe kuchinja wanyama
kwa lengo la kuuzia wananchi, kwa mantiki hiyo hakuna muumini wa dhehebu fulani
aliye na haki ya kisheria kuchinja isipokuwa pale jamii husika inapokubaliana”
ilieleza sehemu ya barua hiyo iliyotiwa saini na Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo
Dk. Yohana Sagenge.
Katika kile kinachoonyesha kikao
hicho kutozaa matunda wakristu waliendelea kwenda kuchinja lakini walikutana na
kikwazo machinjioni ambako afisa aliyekuwa anahusika na kukagua nyama
machinjioni alikataa kukagua iliyochinjwa na wakristo na hivyo wakaamua kuiuza
hivyohivyo. Baada ya wakristo kuanza kuchinjia huko waislamu wakasusa kutumia
machinjio hayo wakwa wanachinjia nje.
Ilipofika hapo Mkuu wa Wilaya ya
Sengerema akaingilia kati na kutangaza wenye haki ya kuchinja kwenye machijio
hayo ni waislam, wakristo wakaweka msimamo wa kuendelea kuchinja hali hiyo
ikiwalazimu Polisi kuingilia kati na kufunga machinjio hayo kwa muda wa mwezi
mmoja.
Baada ya wafanyabiashara ya nyama
kulalamika, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema akaitisha kikao kingine na wachungaji
ambacho kilikaa kwa zaidi ya saa kumi lakini hakikupata muafaka.
Katika kikao hicho akasisitiza kuwa
kwa sasa wenye haki ya kuchinja ni waislam na kama wakristo wakitaka kuchinja
wasubiri katiba mpya.
Mgogoro ulipoendelea ndipo
alipolazimika kwenda Mkuu wa Mkoa ambaye ni kama alikwenda kuwasha moto zaidi
badala ya kuutuliza.
Inaelezwa na baadhi ya wananchi wa
Nyehunge kwamba Desemba 31, 2012 mchungaji Paul Range wa kanisa la EAGT
alikamatwa na Polisi na kuwekwa mahabusu kwa kosa la kuchinja ng’ombe
machinjioni na mwenye ng’ombe aliyechinjwa naye aliwekwa mahabusu kwa kosa hilo
hilo.
Tukio hilo lilisababisha pia Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza kuamuru Mtendaji wa Kijiji cha Nyehunge kufukuzwa kazi kwa
kushindwa kudhibiti uchinjaji huo.
“Ndiyo maana ninakwambia Mkuu wa
Mkoa amechangia sana kulikuza hili. Mchungaji alikamatwa kwa sababu ya
maelekezo aliyotoa siku ya mkutano na hili likaibua hisia kali kwa watu ndiyo
maana tuko hapa leo,” anasema Mwinjilisti Charles.
Habari ni kwa hisani ya Mungu ni Mkubwa Blog.
No comments:
Post a Comment