Saturday, February 23, 2013

MWENYEZI MUNGU HUPOKEA TOBA ZA WANADAMU USIKU NA MCHANA


Hadiyth Ya 2, Katika kitabu cha Hadithi za Mtume (s.a.w.): LU-ULU-UN MANTHUWRUN 
Allaah Hupokea Tawbah Za Waja Usiku Na Mchana

عَنْ أَبِي مُوسَى عَبْدِ الله بنِ قَبَسٍ الأَشْعَرِيِّ  (رضي الله عنه) عن النَّبيّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قال: ((إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abu Muwsaa ‘Abdillaah bin Qays Al-Ash‘ariyy (رضي الله عنه)  kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Anakunjua Mkono Wake usiku ili Apokee tawbah ya mkoseaji mchana. Na Anakunjua Mkono Wake mchana ili Apokee tawbah ya mkoseaji usiku mpaka jua lichomoze Magharibi [mahali linapokuchwa]))[1]

Mafunzo Na Hidaaya:
  1. Umuhimu wa mja kukimbilia kutubu anapofanya maasi mchana au usiku. [At-Tahriym 66: 8, An-Nuwr 24: 31].
وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ
Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Mola wenu na Jannah upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye taqwa[2]
  1. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake kuwapa muda wa kutubia maasi, lau sivyo Angeliwaadhibu na kuwaangamiza hapo hapo wanapotenda maasi. [Faatwir 35: 45, An-Nahl 16: 61].
  1. Rahma ya Allaah kwa waja Wake kutokutofautisha wakati wa tawbah japokuwa maasi mengine yanazidi mengineyo. 
  1.  Tawbah inaendelea kupokelewa hadi milango ifungwe: [Hadiyth: ((Hakika Allaah Huikubali tawbah ya mja Wake kabla ya roho kufika kwenye mkoromo wa mauti))[3] ((Atakayetubu kabla ya kuchomoza jua upande wa Magharibi, Allaah Atamkubalia tawbah yake)).[4]
  1. Hii inaonyesha mahaba makubwa ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuwapatia fursa hii ya dhahabu ambayo haifai kupotezwa na waja wenyewe.
  1. Hadiyth inatoa mafunzo kwa Muislamu kutokumhukumu mwenziwe kuwa hatoghufuriwa madhambi yake. [Rejea Hadiyth namba 99].
  1. Mja hata afanye madhambi makubwa vipi, asikate tamaa na Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى), kwani Yeye Hughufuria madhambi yote. [Az-Zumar 39: 53]



[1]  Muslim.
[2]  Aal-‘Imraan (3: 133).
[3]  At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad, na imepewa daraja ya Swahiyh na Al-Albaaniy.
[4]  Muslim.

No comments: