Anasema Allaah سبحانه وتعالى:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ
عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ
تَتَّقُونَ)) (( أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَى
سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ
طَعَامُ مِسْكِينٍ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ وَأَن تَصُومُواْ
خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ)) ((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ
أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى
وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا
أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ
الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ
وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ
تَشْكُرُونَ))
((Enyi
mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama waliyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu
ili mpate kumcha Allaah))(([Mfunge] siku maalumu za kuhisabika. Na atakayekuwa
miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku
nyengine. Na wale wasioweza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na
atakayefanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu,
kama mnajua)) ((Mwezi wa Ramadhaan
ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi
za uongofu na upambanuzi. Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na
mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine.
Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala Hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize
hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate
kushukuru)) [Al-Baqarah: 183-185]
Inatupasa tumshukuru Allaah
سبحانه وتعالى kwa Kutujaalia
uhai na afya mpaka tunakaribia kufika mwezi mtuku wa Ramadhaan na hii ni fursa
nyingine Anayotupa katika maisha yetu kushuhudia mwezi huu na
kupata fadhila zake.
Na
hii ni neema ya Allaah سبحانه وتعالى Ambaye
Ametujaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au siku bora au
masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu zake za mema yanayotendeka humo huwa
ni zaidi ya nyakati nyingine. Mfano wake ni kama kunapokuwa na mauzo
yaliyopunguzwa bei dukani (sale), ambayo kawaida yake huwekwa kwa muda
mdogo tu maalum. Na muda huu mtu huweza kununua vitu vingi kwa malipo
kidogo tu. Hali kadhalika Ramadhaan, ni mwezi mmoja tu, lakini malipo yake huwa
ni mengi kuliko hata malipo ya miezi yote mingine. Ikiwa mtu
atatimiza Swawm yake inavyopaswa na kufanya mema mengi, na akawa katika Twa'a
(utiifu) kamili na kuomba maghfira, basi hutoka katika mwezi huu akiwa
ameghufuriwa madhambi yake.
Amesema
Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
:
(( من صام رمضان
إيماناً واحتساباً ، غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه
البخاري ومسلم
((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo,
ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ramadhaan ni mwezi ambao tunatimiza
Fardhi mojawapo ya Kiislamu. Ni mwezi uliojaa baraka, kheri na Rahma za
Allaah سبحانه وتعالى. Kila Muislamu inampasa aukaribishe mwezi huu
kwa furaha na matumaini kamili.
Zifuatazo ni njia kumi za
kujitayarisha kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan na kupata manufaa makubwa pindi
utakapotimiza:
1.
Du'aa
Anza kwa kuomba
Du'aa kwamba mwezi huu ukufikie wakati umo katika hali ya siha nzuri na usalama
hata uweze kufunga na kufanya ibada zako kwa hamu kubwa na wepesi.
2. Mazoezi
katika mwezi wa Sha'abaan
Funga Sunnah nyingi katika mwezi wa
Sha'abaan, soma Qur-aan Juzuu moja kila siku au chini yake, amka usiku uswali
japo Raka'ah mbili, kisha zidisha kidogo kidogo hadi inapoingia Ramadhaan uwe
tayari umeshapata mazoezi mazuri.
3. Shukurani
Mshukuru Allaah سبحانه وتعالى Kukupa uhai
na siha hata uifikie Ramadhaan nyingine. Imaam An-Nawawy alisema, kwamba
shukurani inapasa kwa kila jambo jema unalojaaliwa kubwa au dogo na vile vile
shukurani inapasa kwa kila jambo baya Analokuepusha nalo Allaah سبحانه وتعالى. Kwa hivyo
fanya 'Sajdatush-Shukr' [Sajda ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)] kwa
neema hii tukufu.
4. Furaha
Furahia kukufikia mwezi wa Ramadhaan
kama unavyomfurahikia mgeni mpenzi anapokuja kwako na kumuandalia mazuri
yote. Maswahaba رضي الله عنهم, walikuwa wakiamkiana unapoingia mwezi wa Ramadhaan
na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
alikuwa akisema hivi anapowapa habari nzuri za mwezi wa Ramadhaan:
((جاءكم شهر مبارك افترض عليكم صيامه تفتح فيه أبواب الجنة وتغلق فيه أبواب الجحيم وتغل فيه
الشياطين فيه ليلة خير من ألف شهر من حرم خيرها فقد حرم)) رواه أحمد
((Umekujieni mwezi wa
Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh,
milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytaan hufungwa.
Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu. Atakayenyimwa
kheri zake hakika kanyimwa [yote ya
kheri] )) [Ahmad]
5. Jipangie
wakati na weka maazimio
Ni jambo la kusikitisha kuona watu
wengi wanafurahia kuingia mwezi
wa Ramadhaan kwa
kujiandaa kupanga
mambo ya kidunia badala ya mambo ya Akhera. Wengi hukimbilia kwenda
sokoni kununua nguo za 'Iyd, na kufurahikia vipindi vya Ramadhaan katika
televisheni ambavyo sio vya dini kama 'misalsal' (maonyesho ya
sinema yanayoendelea [series]), na pia kuanza
kukusanya video za filamu, mipira, na mambo ya kupotezea muda usiku wa
Ramadhaan. Pia wengine kunua
karata, dhumna, meza ya mchezo wa keram kwa maandalizi ya vipumbazo na vipoteza muda katika
mchana wa Ramadhaan ili wasiihisi Swawm au kuupeleka muda haraka kama
wanavyoamini wao. Badala ya kufanya maandalizi ya kununua misahafu ya ziada,
kanda za mawaidha, Qur-aan, kukusanya video za mawaidha na mafunzo mbalimbali
ya Dini, vitabu vya Dini kwa lugha wanayoifahamu kwa wepesi na kadhalika.
Huu ni mwezi wa kufanya ibada na fursa
ya kujichumia mema mengi yamfaayo mtu Akhera. Kwa hiyo ndugu Waislamu,
tujitahidi kuutumia wakati wetu wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na
muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo:
·
Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda
wako wa mchana na usiku. Weka maazimio ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati
wote wa mwezi huu.
·
Weka mpango maalum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila
kipindi, kusoma Qur-aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja hapa chini.
·
Kama ni mwanafunzi na kama unakuwa ukisoma usiku, lala
mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Llayl na usome masomo yako baada ya hapo.
·
Anza mpango wako kwa siku chache na kama unahitaji kurekebisha
kuboresha nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua nidhaam ipi itakayowafikiana na hali yako.
Nasaha kwa kina Mama na kina Dada:
·
Fanyeni maandalizi mapema ya kununua
vyakula vya mwezi wa Ramadhaan na kuviandaa vyenye kuandalika mapema kabla
Ramadhaan haijaanza, kama vile; sambusa, madonge ya chapati, maji ya matunda
n.k. na kuweka kwenye mashine ya kugandisha barafu (freezer) au jokofu
ili ikifika Ramadhaan muwe na kazi chache za jikoni na muweze kupata nafasi
kubwa ya kushughulika na Ibaadah mbalimbali kama kusoma Qur-aan, kusikiliza
mawaidha na hata kuhudhuria Darsa za Dini.
6.
Tawbah na Maghfirah
Omba Tawbatun-Nasuuha kwa Mola
wako na waombe msamaha wale uliowakosea. Kufanya hivi kutanufaisha
zaidi Swawm na Swalah zako na pia kukupa imani kuwa huna haki ya
mtu.
7.
Jifunze Fiqhi ya Swawm
Jifunze elimu ya mambo yanayohusu Swawm
(Fiqhi ya funga), hiyo ni muhimu ili usije kufanya jambo la kuharibu Swawm
yako. Jifunze Swawm kama aliyokuwa akifunga Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ndio mfano
bora kabisa wa kuufuata.
Swawm haifunguliwi kwa kula na kunywa
tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama
kusengenya, kutukana, kugombana. Mtume صلى
الله عليه وآله وسلم amesema:
((من لم يدع قول الزور والعمل
به والجهل فليس لله حاجة في أن يدع طعامه وشرابه)) البخاري
((Yeyote
asiyeacha kusema maneno mabaya? Na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula
chake na maji)) [Al-Bukhaariy]
8. Jitayarishe
kuchuma mema mengi
Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu,
huruma, rahma na mapenzi.
·
Panga kabisa na
kuweka kiwango fulani cha kutoa Sadaka na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa
ndugu na jamaa.
·
Kama inakupasa kutoa
Zakah, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhaan fanya hima uitimize Fardhi hii
pia.
·
Weka 'azma ya
kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu
ni thawabu.
((قال صلى الله عليه وسلم : من فطر
صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألباني
((Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
"Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua
chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy na kasahihisha Imaam Al-Albaaniy]
·
Kama unaye jirani
asiye Muislamu, mjulishe kuhusu Ramadhaan, faida na Fadhila zake. Hii ni njia na fursa mojawapo ya kufanya da'awah kwa jirani yako.
9.
Hitimisha Qur-aan, Hifadhi na jifunzeTarjama
Jipangie wakati
uweze kuhitimisha Qur-aan kwani Ramadhaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan na
hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Jibriyl عليه
السلام kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kusoma naye Qur-aan yote
((عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: "كان
رسول الله صلى الله عليه وسلم أجود الناس، وكان أجود ما يكون
في رمضان حين يلقاه جبريل، وكان يلقاه في كل ليلة من رمضان فيدارسه القرآن؛ ((رواه البخاري
((Kutoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu,
lakini alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa
akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy]
Hadiyth hii inatufundisha yafuatayo:
- Kusoma Qur-aan katika Ramadhaan;
- Kukutana kwa ajili hiyo;
- Kupima hifdh yako ya Qur-aan kwa kukaa na Mwalimu au mwenye elimu nzuri ya Qur-aan kwa kukusikiliza au kukufundisha;
- Kuongeza juhudi za kusoma Qur-aan zaidi katika mwezi wa Ramadhaan:
Katika muda wa
masaa 24 weka saa moja au mbili khaswa iwe ya Qur-aan kusoma na kujifunza maana
ya maneno ya Mola wako uonje ladha ya Qur-aan. Vile vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo sura
ndogo ili ukitoka katika Ramadhaan uwe una surah zaidi za kusoma katika Swalah
zako.
10.
Darsa
Hudhuria Darsa
katika mwezi huu au soma vitabu vya dini, au sikiliza mawaidha. Jambo
hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na bora kabisa
katika kuzidisha imani yako. Kwa hakika unahitaji saa tu kuweza kutimiza
jambo hili muhimu kila siku. Kama huwezi kuhudhuria msikitini,
Alhamdulillah, ALHIDAAYA imewatayarishia mawaidha
mengi ya kusikiliza na ya VIDEO. Kwa hiyo badala ya kutazama televisheni
na kusikiliza muziki jambo ambalo ni haramu ni bora utazame na kusikiliza
mawaidha ujipatie manufaa, thawabu na kuongeza elimu yako. Kumbuka kwamba kama
vile mwili unavyohitajia chakula, hali kadhalika Moyo na Nafsi zinahitaji
chakula chake nacho ni kumkumbuka Allaah سبحانه
وتعالى kwa kila aina ya
ukumbusho, na mawaidha na darsa za dini ni mojawapo ya chakula kizuri kabisa
cha kutakasa Moyo na Nafsi kwa kuzijaza iymaan na mapenzi ya Mola Wako
Mtukufu.
Kwa kumalizia, tunasema:
Fungua 'Swafha'
(Ukurasa) mpya katika maisha yako
Baada ya kuweza kuyatimiza hayo
yote, bila ya shaka hali yako ya iymaan imekuwa bora kabisa na utakuwa
umejibadilisha na kuwa mtu tofauti na ulivyo. Kwa hivyo weka maazimio ya
kuendelea hata baada ya Ramadhaan kuwa katika twa'a na ibada, na kuendeleza
Qiyaamul-Layl (Swalah za usiku), kusoma Qur-aan japo kidogo KILA SIKU, na iwe
umefungua UKURASA MPYA wa maisha yako na kumuomba Allaah سبحانه وتعالى
Akuendeleze katika hali hii.
Tunachukua Fursa hii ya kuwaombeeni
Ramadhaan yenye baraka na kheri nyingi, tutoke katika mwezi huu tukiwa
tumesafishwa madhambi yetu yote, na wenye kubeba thawabu nyingi ziwe nzito
katika Miyzaan ya Hasanaat (mizani ya amali njema) Siku ya Qiyaamah.
اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنّأ وَ مِنْكُم صَالح الأّعْماَل
Allaahumma Taqabbal Minnaa wa Minkum Swaalih al-A'amaal.
Aamiyn
CHANZO: http://alhidaaya.com/sw/node/1839
No comments:
Post a Comment