Sifa njema zote Anastahiki
Allaah Mola wa viumbe wote na rehma na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Jamaa na Swahaba zake wote.
Hivi unajua ndugu yangu
Muislam, Allaah Akulinde na Akuhifadhi, kwamba 'amali iliyo bora zaidi na
inayopendwa na Allaah Mtukufu na Mtume wake ni tabia njema?
Katika Hadiyth sahihi: Kutoka kwa
Sa'ad bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika Allaah Anapenda
tabia njema na Anachukia tabia mbaya"
Na tabia njema
tumefahamishwa kuwa ni ukunjufu wa uso kutenda wema na kujizuia na
maovu."
Hakika sisi Waislam wa zama
hizi tumo katika tatizo kubwa la tabia, tabia za Kiislam ambazo watu
wengi wa kheri wamezikosa, na zimekua kwa baadhi yao ni kama
mazungumzo ya kawaida na wala hazihitaji kutekelezwa.
Tabia njema zinauweka
Uislam kwenye daraja ya juu kabisa. Je, Hujui kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kwa hakika nimeletwa
ili nikamilishe tabia njema" kulingana na
maneno haya inaonyesha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) amekusanya umuhimu wote alIokuja nao kwa jambo la tabia njema na Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) Akamsifu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) katika Qur-aan Tukufu: Amesema:
"Kwa hakika una tabia
njema mno" Qur-aaan 68:4
Kwa hakika yamethibiti
mambo matukufu makubwa kutokana na tabia njema, baadhi ya mambo hayo ni:
1- Wema haupatikani ila kwa
tabia njema, kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika
hadithi ilyopokelewa na Nawwaas bin Sam'aan (Radhiya Allaahu 'anhu): "Wema ni
tabia njema na dhambi "uovu" Ni ile iliyojificha kwenye
moyo (inakutia wahka) ukachukia watu wajue. (Imepokelewa na Muslim)
2- Na tabia njema ni 'amali
itakayo mpelekea mtu kuingia peponi kwa wingi kama aliyvosema Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyopokewa na Abu
Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) Amesema: Na aliulizwa ni kitu gani
kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi? Akasema: "Kumcha
Allaah na tabia njema" Na
akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni?
Akasema "kinywa (mdomo) na utupu. (Imepokelewa na
At-Tirmidhiy na akasema Hadiyth nzuri na sahihi)
3- Tabia njema ni katika
'amali nzito atakayoikuta Muislam katika miradi ya matendo yake siku ya Qiyaama.
Katika Hadiyth
iliyopokelewa na Abu Dardaa (Radhiya Allaahu 'anhu), Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Hakuna kitu kizito
katika mizani ya Muumin siku ya Qiyaama kuliko tabia njema. Hakika Allaah
Humchukia mtu muovu mwenye tabia mbaya." (Imepokelewa na
At-Tirmidhiy, na ni Hadiyth Hasan)
4- Mwenye kujipamba na
kusifika na tabia njema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) amemdhamini nyumba katika pepo ya juu kabisa.
Kama ilivyopokewa kutoka
kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema: "Mimi ni mdhamini wa nyumba
"iliyopo" katikati ya pepo kwa yule mwenye kuacha mijadala (ubishani)
japo akiwa ana haki, Na nitakua mdhamini wa nyumba katika pepo ya juu kwa
mwenye Tabia njema."
5- Imepokelewa kutoka
kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) akisema,
nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakika
Muumin hupata kwa tabia yake njema daraja za aliyefunga na anayesimama usiku
kufanya ibada."
6- Katika Hadiyth
waliyoafikiana ma-Imaam Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa 'Abdullaah bin Amru
bnil-'Aaswi (Radhiya Allaahu 'anhuma) amesema, alikuwa Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema "Hakika aliye bora kati
yenu ni yule mwenye tabia njema"
Hakika mwenye tabia mbaya
ni mwenye kuzungumza maneno mabaya na vilevile Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) anasema: "Hakika Allaah Huwarehemu waja wake wenye huruma,
basi wahurumieni walio katika ardhi na Atawahurumia aliye mbinguni"
Hivyo basi, tabia njema
inafuatana na kuhurumiana na Iymaan iliyokamilika.
Mwenye kuangalia hali ya
hivi sasa utakuta ni mtihani kwetu na mbele ya Allaah (Subhanahu wa
Ta'ala), utaona mambo ya ajabu, utaona uongo badala ya ukweli, utaona nguvu
zikitumika badala ya upole, utaona khiyana badala ya uaminifu, utaona
ghadhabu badala ya subira na kuondosha ghadhabu na kusameheana baina ya watu,
utaona maudhi badala ya hisani, utaona ubakhili badala ya ukarimu, utaona
uchoyo katika kuchukua sehemu ya kukaa au kufanya ibada, au katika
vinywaji au chakula, badala ya kuathirika na kuwatanguliza wengine kabla
yake, utaona kiburi badala ya unyenyekevu, kisha mtu atajiuliza katika nafsi yake
hivi hawa ni Waislam kweli? Uko wapi uchaji Allaah? Iko wapi Iymaan? Kuko
wapi kuoneana hayaa? Iko wapi huruma kwa maskini, yako wapi mapenzi na
huruma kati ya Waislam???
Je, tuwafanye nini watu
hawa? Tuwalipe uovu kwa uovu tukawaadhibu hapo hapo? Tukifanya hivyo
hatutowazuia kitu, bali tutakuwa tumeshirikiana nao katika kueneza tabia mbaya.
Lililo wajibu kwetu mimi na wewe juu ya watu hawa ni kufuata muongozo wa Allaah
Mtukufu, nao ni; kuwasamehe na kufuta kabisa nyoyoni mwetu yale wanayotufanyia,
na kubadilisha baya kwa kutenda jema na Allaah Mtukufu Anasema:
Na wazuiao ghadhabu zao na
kuwasamehe watu na Allaah Anawapenda wafanyao hisani"
Qur-aan 3:134
Na Akasema tena Allaah
Mtukufu kuwasifu waumini:
"Na wakayaondoa maovu
kwa mema, hao ndio watakaopata malipo "mema" ya nyumba ya Aakhirah" Qur-aan
13:22
Na
Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
“Na wala haulingani sawa wema na uovu.
Lipiza (uovu ulilotendewa) kwa ambalo ni zuri zaidi; tahamaki yule ambaye baina
yako na baina yake kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani. ." Qur-aan 41:34
Na Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: katika Hadiyth iliyopokewa
na Abu Dharr Jundub bin Junaadah na Abu Abdur-Rahmaan Mu'aadh bin Jabal
(Radhiya Allaahu 'anhum) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) kuwa kasema " Muogope Allaah popote ulipo, na lifutishe ovu (baya)
kwa jema, na tangamana na watu kwa tabia zilizo njema.
Na hakika Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema: "Hakika ya mema yanaondosha
mabaya". Qur-aan 11:114
Pamoja na hayo yote Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakulipiza kisasi kwa maudhi
aliyofanyiwa yeye binafsi, ila yatakapovunjwa maamrisho ya Allaah au makatazo
(maharamisho) Basi huadhibu kwa ajili ya Allaah.
ALLAH ATUWAFIQISHE KWA ANAYOYAPENDA NA
KUYARIDHIA NA AJAALIE TUWE WENYE KUYAFANYA YALIO MEMA. AAMIIN.
WA ALLAHU A'LAM
Kwa hisani ya alhidaaya.com
Kwa hisani ya alhidaaya.com
No comments:
Post a Comment