Makala hii muhimu itagusia sana umuhimu wa Muislamu
kuchunga muda wake na kutokuuangamiza kwa kufanya mambo ya kipuuzi ambayo
hayatomsaidia si duniani wala Akhera. Waislamu wengi tunashinda siku kutwa na kujishughulisha
na mambo ya kipuuzi ambayo mengi katika hayo hayamridhishi Allaah.
Kwanza kabla ya kuendelea tungelipenda kurudi nyuma
kidogo tukumbushane lengo la sisi kuwa hapa duniani ni lipi, kwa nini
MwenyeZimungu ametuumba. Allaah anasema katika Qur-aan:
”Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi”
Hapa tumeona kuwa lengo kubwa la Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) kutuumba ni sisi kumuabudu Yeye, na kama tunavyosimuliwa na Wanachuoni
wetu maana ya ”Ibaadah” kijumla ni kila Anachokipenda Allaah na kukiridhia basi
hiyo ni Ibaadah bila shaka.
Moja kwa moja tukirudi katika mada yetu ya kuhusu
umuhimu wa kuchunga wakati, tutaona kwamba wengi wetu tumeghafilika na kupuuzia
risala hii ambayo ndio lengo kuu la Allaah kutuumba. Na tumesahau kwamba kila
Muislam hatopiga hatua moja mpaka mbili siku ya Qiyaamah mpaka ajibu maswali
manne, na moja kati ya hayo ni ”Muda wako uliutumia katika mambo gani.”
Ndugu Muislamu tuzingatie kuwa kila mmoja wetu
ataulizwa kwa kila dakika yake moja aliitumia katika mambo ya kheri au ya
shari. Utamkuta Muislamu amekaa tu na kulalamika kwamba anahisi uvivu kisa hana
la kufanya. Inashangaza sana kwa Muislamu kulalamika kwamba anahisi uvivu kana
kwamba hana Qur-aan aweze kusoma Aayah kadhaa katika Mus-haf ambapo endapo
atasoma Aayah moja tu katika Qur-aan basi atapata ujira kumi kwa kila herufi
moja.
Muislamu kana kwamba hana vitabu vya Dini ambavyo
anaweza kusoma na kujikurubisha zaidi kwa Mola wake. Mambo muhimu sana kwa
Muislamu ni mengi endapo tutayataja basi hatuwezi kuyamaliza yote, ndo maana
haifai hata kid ogo Muislamu kusema kwamba anahisi uvivu au hana cha kufanya.
Waislamu wengi sana takriban asilimia hamsini
tunapoteza muda wetu katika mambo ya kipuuzi na kilichochangia zaidi ni
mitandao hii ya kisasa ya kiteknolojia ambayo imetengenezwa na Mayahudi kwa
lengo kubwa la kumshuhulisha Mwanaadamu kutokufanya mambo yake yenye faida na
yeye hapa duniani na huko Akhera. Inasikitisha sana kuona Waislamu wengi tunaangamiza
muda wetu mwingi katika kuangalia filamu za kipuuzi, wengine tunapoteza muda
wetu mwingi kwenye kompyuta na kufanya mambo ya kipuuzi, wengine tunapoteza
muda katika kuangalia video za muziki na kusikiliza nyimbo za taarabu na
michezo ya kuigiza ambazo zinapoteza muda na zisizo na maadili wala faida, na
wengine tunapoteza muda wetu katika mambo fofauti ambayo hayaafikiani hata
kidogo na Dini yetu wala hayachangii hata kidogo katika kuueneza Uislamu
duniani.
Ndugu yangu Muislamu, tujue kwamba kuchunga muda ni
katika mambo muhimu sana katika Uislamu, na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala) kaapa mahali pengi sana kwa muda katika Qur-aan kutuonyesha umuhimu wa
muda. Na Allaah Anapotueleza jambo fulani katika Qur-aan basi linakuwa na
umuhimu na faida kubwa sana kwa Mwanaadamu. Tukiangalia Kitabu kitukufu cha
Allaah chatueleza nini kuhusu wakati, basi tutaona kwamba Allaah Kaapia kuhusu
muda kuanzia asubuhi mpaka pale usiku unapoingia, na lengo ni kutuonyesha
umuhimu na na utukufu wa muda kwa Muislam.
Tuangalie Allaah Anatuambia nini kuhusu
muda:
Allaah Ameapia muda wa asubuhi kwa kusema:
1. Naapa
kwa alfajiri
Baada ya hapo Ameapa muda wa mchana kwa kusema:
2. Naapa
kwa nyakati za mchana
Baada ya hapo Ameapa kwa mchana unapofunuka wazi.
3. Na
kwa mchana unapolidhihirisha!
4. Naapa
kwa usiku unapofunika!
Viapo vyote hivi haina maana Allaah Amependa tu Kuapa
bila sababu au maana, Amependa kutuonesha umuhimu na utukufu wa wakati. Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) hajaapa kwa kitu chochote mara nyingi sana kuliko
wakati. Allaah Kaapa mara nyingi sana na zile tulizotaja ni baadhi ya viapo tu
katika Qur-aan, ila viapo ni vingi sana Kaapia juu ya wakati. Ameapa kwa kila
wakati kuanzia asubuhi mpaka usiku wakati wenyewe Amekuumbia umfanyie Ibada na
si vinginevyo au kuangamiza bure tu.
Tukumbuke kwamba kila dakika moja inapotoweka basi
hairudi nyuma na wakati wako wa maisha unazidi kupunguka. Kwahio inafaa
tuzingatie sana na kutumia mda wetu katika mambo mema na mazuri tu ambayo
yatatukurubisha zaidi kwa Mola wetu.
Tusipoteze mda wetu kwa mambo ya kipuuzi ilihali tuko
na mambo mengi ambayo yanaweza kutushughulisha yenye faida na sisi hapa Duniani
na huko Akhera. Panga muda wako vizuri kwa siku usikose kusoma Qur-aan, usikose
kuongea na watoto wako na mama watoto, usikose kujifunza moja au mawili ambayo
yatakusogeza zaidi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).
Tupunguze kazi zetu na shuhuli zetu fulani na
tupangilie muda fulani kudumisha malezi na tarbiyah ya Kiislamu katika majumba
yetu ili tuweze kuisogeza mbele jamii yetu ya Kiislam.
Kumbuka kwamba Malaika wa kutoa roho (Malakul Mawt)
atapokuja na kuchukua roho yako, utatamani akupe angalau dakika chache ili
uweze kuswali rakaa mbili, muda wako utakuwa umekwisha na hutopewa hata dakika
moja. Kwa hiyo chunga sana Muislamu na acha kuangamiza na kuponda muda wako,
ikiwa ni ujana wako na nguvu zako ndizo unazojivunia, wangapi wameiaga dunia
hii huku wakiwa na nguvu na uwezo wa kukushinda.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atujalie tuwe
miongoni mwa wale wenye kusikia machache na kuyazingatia. Na Atujalie katika
umri wetu wote uliobakia tuweze kutumia muda wetu kwa yale Anayoyapenda na
Kuyaridhia.
Chanzo: Alhidaaya.com
No comments:
Post a Comment