Wednesday, May 1, 2013

HOTUBA YA MH. JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA SHEREHE YA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI



Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA),
Ndugu Ayoub Omari Juma;
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Mheshimiwa Gaudensia Kabaka (Mb) Waziri wa Kazi na Ajira;
Mhe. Col Issa Machibya, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;
Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge Mliopo Hapa;
Ndugu Alexio Musindo, Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO)



Kanda ya Afrika Mashariki;
Kaimu Katibu Mkuu, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi ,
Ndugu Nicholaus Mgaya;
Waheshimiwa Mabalozi Mliopo Hapa;
Mwenyekiti wa, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE),
Dr. Aggrey Mlimuka;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa na Serikali;
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi Wenzangu;
Mabibi na Mabwana:
Nakushukuru sana ndugu Ayoub Omari Juma, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika sherehe za mwaka huu za kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani. Hongereni kwa maandalizi mazuri ya sherehe hii ambayo naambiwa yamesimamiwa na Chama cha Walimu Tanzania. Si ajabu yamefana kiasi hiki kwani tusingetegemea kitu pungufu kuliko hiki kutoka kwa Walimu.
Napenda pia kutoa shukrani na pongezi kwa wenyeji wetu, viongozi na wananchi wa mkoa wa Morogoro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huu Lt. Col. Issa Salehe Machibya. Tunawashukuru kwa mapokezi mazuri na kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kufanikisha sherehe hizi. Waswahili wanasema “usione vinaelea vimeundwa“ na waundaji si wengine bali ni viongozi na wananchi wa Manispaa ya Morogoro. Tunawashukuru na kuwapongeza sana.


Poleni kwa Msiba
Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Narudia tena kuwapeni pole kwa msiba mkubwa uliowakuta tarehe 4 Aprili, 2011 kutokana na kifo cha Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli marehemu Sylvester Rwegasira. Kifo chake cha ghafla ni pigo kubwa siyo tu kwa familia yake iliyopoteza mlezi na wafanyakazi waliopoteza kiongozi mahiri, bali pia kwa taifa letu kwa jumla. Sote tumepoteza mtu muhimu. Tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema. Amin.




Pongezi kwa Wafanyakazi Bora
Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Niruhusuni nitumie fursa hii, pia, kuwapongeza wafanyakazi waliotunukiwa tuzo za ufanyakazi bora siku ya leo. Wahenga wamesema, “Chanda chema huvishwa pete”. Wenzetu leo wamevishwa pete ya ushindi inayotambua uchapakazi wao, ufanisi wao na nidhamu yao kazini. Wakati tunawapongeza kwa ushindi nawaomba, wao wenyewe, wachukulie tuzo walizopata kuwa ni changamoto ya kuwataka waongeze bidii zaidi kazini ili waendelee kuwa wafanyakazi wa mfano kwa wengine. Naomba waelewe kuwa wapo wenzao wengi wazuri ambao hawakubahatika kwa sababu nafasi ni moja tu. Kwa wafanyakazi wengine tuzo walizopata wenzenu iwe kichocheo kwenu kuongeza bidii na nidhamu kazini ili mwaka ujao nanyi muwe wapokea tuzo. “Inawezekana, timiza wajibu wako”.


Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Waajiri;
Utaratibu huu wa kutambua na kutunuku utendaji kazi mzuri wa wafanyakazi ni jambo jema. Unasaidia kuongeza ari ya kazi na ufanisi kazini. Aidha, huhamasisha wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Lazima tuudumishe na kuuboresha hasa kwa aina ya zawadi wanazopata wafanyakazi bora.
Kauli Mbiu ya Mwaka Huu
Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;
Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Gaudencia Kabaka kwa maelezo yake ya utangulizi. Yameweka msingi mzuri kwa mimi kuweka lami. Aidha, nakushukuru sana Rais wa TUCTA kwa maneno yako ya hekima ya kunikaribisha kuzungumza na hadhara hii. Nawashukuru sana kwa risala yenu iliyosomwa kwa ufasaha na Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Ndugu Nicolas Mgaya. Risala yenu imejitosheleza kwa hoja na ina ushauri mwingi mzuri kuhusu mikakati ya kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi. Napenda kuwahakikishia kuwa tumeupokea kwa mikono miwili ushauri huo na tutaufanyia kazi.
Nakubaliana na ujumbe wa kauli mbiu yenu ya mwaka huu kwamba “Serikali isipojali haki zenu, wafanyakazi watakuwa watumwa ndani ya nchi yao”. Ni ukweli uliowazi kwamba Serikali inao wajibu wa kulinda haki za wafanyakazi nchini. Lakini ni kweli pia kwamba wajibu wa kulinda haki za wafanyakazi hauko mikononi mwa Serikali pekee. Upo pia kwa waajiri na wafanyakazi wenyewe kupitia au kwa kuongozwa na vyama vyao. Mimi naamini, wote tukitimiza wajibu wetu ipasavyo, tutaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wafanyakazi hapa nchini.
Ndugu Rais wa TUCTA;
Napenda kuwahakikishieni kuwa Serikali inatambua ukweli huo na wajibu wake huo. Serikali yetu na zile za awamu zilizopita zimekuwa zinachukua hatua za kulinda na kuendeleza maslahi ya wafanyakazi. Viwango vya mafanikio vimekuwa vinapishana. Yapo mambo ambayo tumeweza kupata mafanikio makubwa na yapo ambayo mafanikio yake si makubwa sana. Hata hivyo, juhudi zimekuwa zinaendelea. Hakuna upuuzaji na wala hakuna upungufu wa utashi wa kisiasa wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wafanyakazi. 


Ndugu Wafanyakazi,
Utashi wa Serikali katika kutekeleza wajibu wake wa kulinda haki za wafanyakazi nchini umejidhihirisha wazi kupitia hatua za kisheria na za kiuchumi ambazo imekuwa inatekeleza. Kwa upande wa sheria, napenda kutambua sheria tatu ambazo zipo kwa ajili ya kulinda na kuendeleza haki na maslahi ya wafanyakazi nchini. Sheria hizo ni: Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2001, Sheria ya Taasisi za Kazi ya mwaka 2004 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.


Ninyi viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi mnatambua vyema kuwa katika sheria hizi haki na wajibu wa wafanyakazi na waajiri vimeainishwa vizuri. Aidha, utaratibu na mifumo ya kulinda haki hizo na uhusiano na mawasiliano baina yao imefafanuliwa vyema. Vile vile, vyombo vya utekelezaji vimetajwa pamoja na majukumua ya kila chombo.


Ndugu Rais wa TUCTA;
Wakati tunaingia madarakani tulijikuta tunalo jukumu la kihistoria la kuhakikisha kuwa sheria hizo zinatekelezwa kama ilivyokusudiwa. Sheria ya Utumishi wa Umma tuliifanyia marekebisho mwaka 2008 kwa lengo la kuweka utaratibu wa haki zaidi wa ajira na kuwapandisha vyeo watumishi wa umma na kutambua kanuni za mahusiano bora kazini (Code of good conduct). 


Kwa sheria ya Taasisi za Kazi na ile ya Ajira na Mahusiano Kazini tulitengeneza Kanuni zake na hivyo kuwezesha kuanza kutumika. Kwa ajili hiyo, mfumo wa ushirikishaji wafanyakazi kuhusu masuala ya mishahara yao na maslahi mengineyo ukaanzishwa rasmi. Miongoni mwa hayo ni kuundwa kwa Baraza la Majadiliano kwa upande wa sekta ya umma, Baraza la Ushauri la Masuala ya Kazi, Uchumi na Kijamii (LESCO), Baraza la Usuluhishi na Upatanishi na Bodi za Mishahara za Kisekta kwa upande wa sekta binafsi. Serikali yetu imekamilisha jukumu lake la kuhakikisha kuwa vyombo hivyo vinaundwa na kufanya kazi yake ipasavyo. 


Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Haya ni mapinduzi makubwa katika kulinda haki na kuendeleza maslahi ya wafanyakazi nchini. Wafanyakazi wameongezewa fursa ya kutoa maoni yao na kauli yao kusikika katika kujadili viwango vya ujira wao na waajiri wao. Inawezekana si kila wanachotaka wafanyakazi kikatekelezwa au wakakipata kwa kiwango kile walichotaka, lakini hawatoki mikono mitupu. Pia, hoja zao zinakuwa zikisikika na wao wamewasikia waajiri wanachosema. Hakika hatua tuliyofikia si ndogo hata kidogo. Kwa upande wa LESCO, naambiwa kuwa katika Bara la Afrika pengine ni sisi na Afrika ya Kusini tu ndiyo wenye chombo cha namna hiyo.
Wajibu wa Waajiri na Serikali


Ndugu Wafanyakazi;
Katika kulinda na kuendeleza haki za wafanyakazi, waajiri nao wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanafuata matakwa ya sheria za kazi za nchi. Aidha, wanao wajibu wa kudumisha mahusiano mema kazini kwa manufaa yao wenyewe na wafanyakazi wao. Nimesikia kilio cha wafanyakazi kwamba pamoja na kuwepo sheria na mifumo ya kulinda haki za wafanyakazi, wapo baadhi ya waajiri wanapuuza yote hayo. Wapo ambao hawaheshimu sheria zihusuzo ajira wala mishahara na maslahi ya wafanyakazi wao. Wapo pia wanaokataza wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi na hawaruhusu matawi ya vyama hivyo kufunguliwa katika maeneo yao ya kazi.


Ni vyema waajiri wote wakatambua kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai na wanastahili adhabu kali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, Msajili wa Vyama Huru vya Wafanyakazi na Kamishna wa Kazi msimamie sheria kwa ukamilifu. Wabaneni kisawasawa waajiri wote ili waheshimu sheria za kazi za nchi. Wasiotii wachukuliwe hatua na kuwajibishwa ipasavyo. Mamlaka mnayo, yatumieni. Asiwatishe mtu ye yote kwani sheria zinawalinda. Aidha, wabaneni Maafisa wa Kazi na Wakaguzi wa Kazi watimize ipasavyo wajibu wao. Baadhi yao wanalalamikiwa kuwa hawatendi haki na wanaonekana kuegemea sana upande wa waajiri wanaowakandamiza wafanyakazi.


Mheshimiwa Waziri;
Sisemi kuwa maafisa hao wasiwe wakweli kama wafanyakazi hawana haki. Ninachosema ni kuwa lazima hisia hizi hasi za kuwa wanawapendelea waajiri zifutike kwa wao kutenda haki na waonekane wanafanya hivyo. Msichelee kuwawajibisha wanaopindisha sheria. Si vibaya mkafanya uhamisho wa maofisa wenu waliokaa kituo kimoja kwa muda mrefu. Wahenga wanasema: “mazoea yana taabu”


Wajibu wa Wafanyakazi
Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Kwa upande wenu, yaani vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi wenyewe, nanyi mnao wajibu muhimu katika juhudi za kulinda na kuendeleza haki za wafanyakazi. Wajibu wenu wa msingi ni ule wa kudai haki zenu bila woga huku mkizingatia sheria na kununi za kufanya hivyo. Ndiyo maana vyama vya wafanyakazi vipo. Timizeni ipasavyo wajibu wenu huo. Kila kilio kina wenyewe.
Ili malengo yenu yafanikiwe kwa urahisi ni muhimu sana kwenu kuhakikisha kuwa wanachama wenu wanazifahamu vyema sheria na kanuni za kazi zinazowahusu. Mfanyakazi anayejua sheria atafahamu vyema nini cha kudai na akidai vipi ili apate mafanikio. Atafanya hivyo kwa kujiamini na hatimaye atafanikiwa. Kamwe mfanyakazi huyo hatokuwa mtumwa.


Ndugu Wafanyakazi;
Pamoja na hayo lazima vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kutambua kuwa ulinzi wa haki za wafanyakazi huanzia kwa wafanyakazi kutekeleza vyema wajibu wao na majukumu yao katika kazi zao. Kwa kawaida waajiri huwapenda na kuwaenzi wafanyakazi hodari wa kazi na waaminifu na huchukia wavivu, wezi, wasiokuwa waadilifu na watovu wa nidhamu. 


Wafanyakazi wenyewe na Vyama vya wafanyakazi viwakumbushe wafanyakazi kujiepusha na vitendo vya uvivu, utoro, wizi, ubadhirifu na utovu wa nidhamu. Wasipojiepusha na hayo wanaifanya kazi ya kutetea na kulinda haki zao kuwa ngumu kwao na wadau wengine kama sisi. Lazima wakati wote tukumbuke kuwa kila haki ina wajibu.
Ajira na Utandawazi
Ndugu Rais wa TUCTA;
Katika risala yenu mmelizungumzia tatizo la ajira na kukumbusha umuhimu wa kulitafutia ufumbuzi. Nakubaliana nanyi kwamba lipo tatizo kubwa la ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana na ni tatizo linalozidi kukua mwaka hadi mwaka.


Tunalitambua tatizo hili na tunayo mikakati ya kukabiliana nalo. Tulifanikiwa katika lengo letu la kuongeza ajira milioni moja katika miaka mitano iliyopita. Na ukweli ni kwamba tulivuka lengo kwa zaidi ya ajira 330,000. Hata hivyo, tatizo ni kubwa sana kiasi kwamba mafanikio tuliyopata yamekuwa kama vile kuweka tone la maji baharini. Tunautambua ukweli huu na tumejipanga kuendelea kukabiliana na tatizo hili. Lengo letu ni kufanya maradufu ya safari iliyopita. Niruhusuni nielezee mtazamo wetu na hatua tunazokusudia kuchukua kukuza ajira nchini

.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Ajira zinaongezeka iwapo uchumi unakua. Yaani shughuli za uzalishaji mali na utoaji wa huduma zinapoongezeka ndipo watu zaidi wa kufanya kazi huhitajika na hivyo ndivyo ajira zinavyokuzwa. Ni muhimu tutambue pia kwamba kuongezeka kwa uzalishaji mali na utoaji wa huduma kunategemea kuongezeka kwa uwekezaji. Bila ya uwekezaji kuongezeka hakuna uzalishaji mali wala utoaji huduma utakaoongezeka na hivyo hakutakuwepo na ongezeko la ajira.


Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Ndiyo maana Serikali yetu imekuwa inatoa msukumo maalum wa kuhamasisha na kuvutia uwekezaji nchini. Tunafanya hivyo kwa upande wa Serikali na ule wa sekta binafsi. Serikali ikiwekeza katika ujenzi wa shule, zahanati, barabara na miradi mingineyo, ajira huzalishwa wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi. Kwa mfano, ujenzi wa sekondari za kata na upanuzi wa shule za msingi, licha ya kuajiri watu wengi wakati wa ujenzi, umewezesha walimu wapya 83,075 kuajiriwa katika miaka mitano iliyopita. Hivi sasa kuna nafasi wazi za walimu 74,996 zinazohitaji kujazwa.


Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Kwa upande wa sekta binafsi, mikakati yetu inahusu kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza vitega uchumi vyao nchini. Katika miaka mitano iliyopita miradi ipatayo 3,881 yenye thamani ya kiasi cha dola za Marekani milioni 27,330 ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji (TIC). Miradi hiyo ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji inategemewa kuzalisha ajira 444,343. Bado uwekezaji kutoka nje ni mdogo ukilinganisha na fursa za uwekezaji zilizopo nchini. Ni dhamira yetu kuongeza juhudi ya kuvutia wawekezaji zaidi kuja nchini na kuzalisha ajira. Madamu msukosuko wa uchumi wa mwaka 2009 na 2010 ulisababisha kasi ya uwekezaji kupungua duniani na nchini umekwisha, matumaini ya kufanikiwa yapo. Lazima tuchemke kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.


Ajira ya Wageni
Ndugu Rais wa TUCTA;
Katika risala yenu pia, mmelalamikia wageni kupata ajira zinazostahili kuwa za wananchi. Hayo ni makosa yanayosababishwa na watendaji katika mamlaka za utoaji wa vibali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri Gaudencia Kabaka na namuomba Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani kuhakikisha kuwa maofisa wahusika katika Wizara zenu wanatimiza ipasavyo wajibu wao kuhusu suala hili. Ni dhambi kuacha Watanzania hawana ajira na kuwapendelea wageni pale isipostahili. Nawaomba wafanyakazi msichoke kutoa taarifa ili makosa hayo yarekebishwe.
Wawakezaji Wazawa
Ndugu Wafanyakazi;
Kwa wawekezaji wa ndani, mikakati yetu inalenga kutengeneza mazingira mazuri kwa wajasiriamali wadogo, wakati na wakubwa kuvutika na kuwekeza nchini kwao. Miongoni mwa hatua ambazo tumekuwa tunachukua ni pamoja na kupunguza urasimu na kurahisisha taratibu za kupata leseni, kuanzisha miradi na kupata mikopo kutoka asasi za fedha. 


Kwa upande wa wajasiriamali wadogo, kwa sababu ya mazingira mazuri tuliyoyatengeneza yamekuwapo mashirika kadhaa yanayotoa mikopo midogo midogo (micro finance schemes). Wengi wamenufaika. Na sisi Serikalini tumeendelea kuimarisha mifuko inayotoa mikopo yenye masharti nafuu kama vile Mfuko wa Vijana na Mfuko wa Wanawake na tumeanzisha Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.


Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mifuko hii imekopesha fedha nyingi kwa Watanzania wengi ambao wamewekeza katika shughuli mbalimbali zilizozalisha ajira kwa watu wengi pamoja na wao wenyewe kujiajiri.
Kwa upande wa Mfuko wa Vijana, kwa mfano, SACCOS mbili katika kila Halmashauri na Manispaa zote za Tanzania Bara ziliainishwa na kukopeshwa. Kwa ajili hiyo, jumla ya SACCOS 238 zilikopeshwa shilingi bilioni 1.19 hadi Desemba, 2010. Mfuko wa Dhamana wa Mradi wa Usawa wa Jinsia na Ajira Bora kwa Wanawake ulitoa jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.23 kwa wajasiriamali 3,800 kupitia SACCOS za wanawake. Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi nao uliweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 45.44 ambapo wajasiriamali 72,113 walifaidika na SACCOS zipatazo 192 na vikundi vya uzalishaji mali na kiuchumi vipatavyo 86 vilifaidika na fedha hizo. Fursa nyingi za ajira zimezalishwa na mifuko hii, ndiyo maana ni sera ya Serikali kuiendeleza na kuongeza uwekezaji.


Ndugu Wananchi;
Tutaongeza fedha katika mifuko ya Serikali ili watu wengi zaidi wanufaike miaka ijayo. Aidha, tutaendelea kuboresha mazingira ili asasi za kutoa mikopo midogo ziongezeke, ziimarike na kunufaisha wengi. Hata hivyo, riba zinazotozwa na nyingi ya asasi hizi zinalalamikiwa kuwa kubwa mno kiasi cha kuwakwaza wakopaji. Badala ya juhudi zao kuwa za kujinasua na umaskini wanajikuta wanatumia muda wao mwingi na mapato yao mengi kuhangaikia kulipa riba ya mikopo. Nawaomba wenye asasi zinazokopesha wasikilize kilio hiki kwa moyo wa huruma. Waangalie viwango vya riba na taratibu za malipo. Mkopaji kulipa kila wiki hakumpi nafasi ya kujijenga na hivyo kushindwa kujikomboa na umaskini.


Wajasiriamali wa Kati na Wakubwa
Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa wajasiriamali wa kati na wakubwa wa Kitanzania, tulielekeza nguvu zetu katika kuwajengea fursa na uwezo wa kukua. Tuliendeleza mifuko miwili maalum kwa ajili hiyo yaani Small and Medium Enterprises Credit Scheme na Export Guarantee Scheme. Aidha, kuanzia mwaka wa jana tulianza kuchukua hatua thabiti za kuijenga upya Benki ya Rasilimali ili irejee kufanya kazi ya benki ya uwekezaji kama ilivyokusudiwa ilipoanzishwa. Tuliipa mtaji wa shilingi bilioni 50 na tutafanya hivyo mwaka huu mpaka 2015. Dhamira yetu ni kuwapatia wawekezaji wazawa taasisi ya fedha itakayowawezesha kupata mikopo ya muda wa kati na mrefu. Kwa ajili hiyo wataweza kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali na huduma kama vile viwanda, mahoteli, kilimo, utalii, uchukuzi n.k.

Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Tayari watu wameanza kunufaika na mikopo hiyo na uwekezaji unaendelea na ajira zinazidi kuzalishwa. Dhamira yangu ni kuona sekta nyingi na wajasiriamali wengi zaidi wananufaika na mikopo kutoka Benki ya Rasilimali. Naamini juhudi hizi na zile ambazo tunazozielekeza kukuza kilimo zitaongeza sana ajira nchini katika miaka michache ijayo. Kwa upande wa kilimo, pamoja na mikopo inayotolewa sasa kupitia TIB, tunategemea kukamilisha uanzishaji wa Benki ya Kilimo katika mwaka ujao wa fedha. 


Kuanzishwa kwa Benki hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha kuleta mapinduzi ya kilimo nchini. Kilimo ndiyo sekta inayowaajiri Watanzania wengi kuliko zote nchini ingawa watu hawaoni kama kujishughulisha na kilimo ni ajira. Hizi ni fikra potofu. Bahati mbaya sana vijana wengi hawapendi kujishughulisha na kilimo kwa sababu ya mazingira magumu ya kazi hiyo na kuwaachia wazee wao. Naamini mageuzi tunayoendelea kufanya chini ya mkakati wa Kilimo Kwanza yakisaidiwa na Benki ya Kilimo itakayoanzishwa yataibadili hali hiyo na kuvutia watu wengi pamoja na vijana kujishughulisha nayo. 


Ajira Katika Soko la Pamoja
Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi,
Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo inatoa fursa mpya za ajira kwa Watanzania. Utekelezaji wa Umoja wa Forodha umekuza mauzo ya Tanzania katika nchi wanachama na hivyo kuchochea uzalishaji na ajira kuongezeka nchini. Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki iliyoanza kutumika tarehe 1 Julai, 2010 inafungua milango kwa bidhaa, mitaji, ajira na huduma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya kutowekewa vikwazo vya kuvuka mipaka kwenda nchi nyingine.


Hatua hii inatoa fursa kwa Watanzania kuweza kupata ajira katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Hivyo hivyo na watu wa nchi hizo nao watapata fursa ya kuajiriwa katika nchi yetu. Tulichokubaliana kwa upande wa ajira ni kuwa kila nchi itaainisha ajira inazofungua kwa watu wa nchi wanachama kuweza kuajiriwa. Zoezi hili limeanza na linaendelea hivi sasa.


Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hii ni fursa nzuri kwa Watanzania kupata ajira, tunachotakiwa kufanya ni kujipanga vizuri ili tunufaike na soko pana zaidi la ajira katika nchi hizo. Tunatakiwa kuangalia mitaala ya shule zetu na vyuo vyetu ili wahitimu wetu waweze kuwa na sifa za kupata ajira katika nchi za Afrika Mashariki. Kadhalika tuzingatie sifa nyingine muhimu za kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uaminifu. Naamini tunaweza kabisa kuwa hivyo na kufanya hivyo. Watanzania tunayo sifa ya kumudu magumu mengi hata changamoto hii nayo tutaikabili na kushinda.
Maslahi ya Wafanyakazi


Ndugu wafanyakazi,
Kilio chenu cha kuboreshewa mishahara na kupunguziwa kiwango cha kodi tumekipokea kwa uzito unaostahili. Jambo hili mlishalileta siku za nyuma na tumechukua hatua, tunaendelea na tuaendelea kuchukua hatua. Tangu tuingie madarakani, Serikali yetu imekuwa inachukua hatua za makusudi za kuboresha mishahara ya watumishi wa umma na wale wa sekta binafsi. Kwa mfano, kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kimeongezeka kutoka shilingi 65,000 kwa mwezi mwaka 2006 hadi kufikia shilingi 135,000 kwa mwezi mwaka 2010. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 107.
Aidha, tumekuwa tunaboresha mishahara ya kada mbalimbali za utumishi wa umma kwa makundi yao. Hatua hizi zimepunguza kasi ya watumishi wa umma katika baadhi ya kada kuhamia sekta binafsi na hata wale waliohama kurudi. Mkakati huo tutauendeleza kwa kada ambazo hatujazifikia bila kusahau wale tuliokwishawafikia kuwaboresha zaidi. 


Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Kwa upande wa sekta binafsi, hatua yetu ya kuhakikisha kuwa Bodi za Mishahara za Kisekta zinaundwa na kufanya kazi imeanza kuzaa matunda. Kima cha chini kimepanda kutoka shilingi 48,000/= kwa mwezi hadi shilingi 80,000/= mpaka shilingi 300,000/= kutegemea na aina ya shughuli afanyayo mwajiri.
Vile vile, katika miaka mitano hii, kodi ya mapato imepunguzwa kutoka asilimia 18.5 hadi asilimia 14 na VAT imeshuka kutoka asilimia 20 hadi asilimia 18. Hatua zote hizo zimeleta nafuu ya kiasi fulani.
Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;


Pamoja na hatua hizo bado mishahara ya wafanyakazi nchini ni midogo ukilinganisha na gharama za maisha. Tunatambua hoja na haja ya kuendelea kuongeza mishahara mwaka hadi mwaka mpaka tufikie pale tunapotaka sote tufike, yaani mshahara wa kumudu gharama za maisha.
Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna upungufu wa dhamira wala utashi wa kisiasa wa kufanya hivyo, kwa upande wangu binafsi au wa wenzangu Serikalini. Yale tuliyoyafanya katika miaka mitano iliyopita ni uthibitisho tosha wa ukweli huo. Ahadi ninayopenda kurudia tena leo ni kuwa tutaiendeleza kazi tuliyoianza mwaka hadi mwaka. Hata hivi sasa katika mchakato unaoendelea wa kutayarisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha, wahusika wanaangalia namna ya kupandisha kima cha chini cha mashahara na nafuu nyinginezo.


Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;
Uwezo wa kimapato wa Serikali ndiyo kikwazo kinachotupunguzia kasi ya kuboresha mishahara ya watumishi wa umma. Wakati wote tumekuwa tunajikuta tupo katika mtihani kuhusu kuweka uwiano mzuri baina ya matumizi ya mishahara na matumizi kwa ajili ya shughuli nyinginezo za Serikali. Busara inaelekeza kuwa kiasi cha fedha zinazotumika kulipa mishahara kisiwe kikubwa mno na kubakiza kiasi kidogo kwa ajili ya Serikali kutekeleza majukumu yake mengine ya utawala, ulinzi na usalama, maendeleo na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi wake. 


Changamoto kubwa tuliyonayo ni jinsi ya kuongeza zaidi mapato ya Serikali ili tuwe na fedha za kutosha kuwalipa wafanyakazi mishahara inayokidhi gharama za maisha na kubaki na pesa nyingi zaidi kwa Serikali kuendesha shughuli zake na kuhudumia wananchi wake. Katika miaka mitano iliyopita tumefanya juhudi kubwa ya kuongeza mapato ya Serikali na tumepata mafanikio yanayotia moyo. Mapato yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 177.1 kwa mwezi mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 390.7 kwa mwezi mwaka 2010.


Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;
Mafanikio hayo ndiyo yaliyotuwezesha kuongeza mishahara kwa kiasi tulichofikia sasa. Hivyo basi, jawabu la tatizo lipo katika kuongeza zaidi mapato ya Serikali. Hiyo ndiyo dhamira yetu na tumejipanga kimkakati kufanya hivyo. Ndiyo maelekezo yangu ya msingi niliyoyatoa kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato nilipowatembelea mwezi Februari, 2011. Kinachotakiwa ni wafanyakazi wenzetu katika asasi hizo kufanya kazi kwa bidii na uaminifu na walipa kodi kuwapa ushirikiano. 


Ndugu Rais wa TUCTA;
Nafurahi kwamba katika risala yenu mmetoa mawazo mengi mazuri kuhusu namna ya kuongeza mapato ya Serikali, kubana matumizi na kuboresha mishahara ya wafanyakazi. Mawazo yenu yanashabihiana sana na mawazo yetu na baadhi ya mambo tunayofanya na tunayoyafikiria kuyafanya katika kuboresha mapato ya Serikali na maslahi ya watumishi wa umma. Tupeni nafasi tukayafanyie kazi. 


Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;
Nimeagiza pia kuwa Serikali yetu ianze kufikiria mambo mbalimbali yatakayowanufaisha wafanyakazi na kuinua hali zao za maisha. Hususan nimeagiza tuangalie uwezekano wa wafanyakazi kupata mikopo ya gharama nafuu watakayoitumia kununua au kujenga nyumba au kununua vyombo vya usafiri au vyombo vya nyumbani. Tumekuwa tunatoa mikopo kwa Waheshimiwa Wabunge, sasa tufanye hivyo kwa watumishi wa Serikali nao. Nafurahi kuwa Azimio la kuanzisha mfuko wa mikopo ya watumishi wa umma lilipitishwa na Bunge katika kikao kilichopita. 


Vile vile, nimeagiza tutoe kipaumbele kwa ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wa umma hasa wale wa vijijini na vyombo vya ulinzi na usalama ili tuboreshe mazingira yao ya kazi. Ni kazi ambayo tunaifanya hivi sasa ila tunataka tuipe msukumo mkubwa zaidi.


Wafanyakazi wa Sekta Binafsi
Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;
Kwa upande wa wafanyakazi katika sekta binafsi, tutaendelea kusimamia Mabaraza ya Mishahara ya Kisekta ili yafanye kazi zake ipasavyo na kuhakikisha kwamba maslahi ya watumishi katika sekta hiyo yanaboreshwa. Kwa hatua tulizokwishazichukua tangu yaundwe, mafanikio yake yameanza kuonekana. Hata hivyo, wafanyakazi wangeweza kunufaika zaidi. Naambiwa kwamba wafanyakazi wengi katika sekta binafsi wapo katika mazingira magumu. Wapo wengi ambao ni vibarua wa kutwa na wengine wako hivyo kwa maisha yao yote. Aidha, wanapata ujira mdogo. 


Waajiri wanakwepa wajibu wao stahiki kwa wafanyakazi wao ambao ndiyo wanaofanya watajirike. Kuwasaidia wafanyakazi kudai na kupata haki zao ni moja ya agenda muhimu za Serikali yetu. Naomba vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi tusaidiane na kushirikiana katika jambo hili. Haya ni mapambano yetu sote. Tukishirikiana na kusaidiana tutashinda.
Kuboresha Pensheni/Malipo ya Uzeeni
Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi, 


Nawashukuru sana kwa maneno yenu ya pongezi kuhusu hatua tulizochukua juu ya kurekebisha na kuboresha mafao ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii. Nami nafurahi kwamba, lile tatizo la mafao ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaaam waliokuwa katika mfumo wa SSSS tumelipatia ufumbuzi. Wafanyakazi hao sasa wameingizwa katika mfumo wa PPF kama wenzao wengine. Kwa ajili hiyo Serikali italipa shilingi bilioni 9.46 kufidia michango ambayo haikuwahi kulipwa ili ndugu zetu hawa waweze kulipwa mafao yao chini ya mfumo wa PPF.


Jambo la pili ni kuwa nafurahi Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekwishaundwa na imekwishaanza kazi. Tena wameanza vizuri. Kupitia mamlaka hii sasa masuala yahusuyo afya ya mifuko, uwianishaji wa mafao baina ya mifuko na uboreshaji wa mafao yatapatiwa ufumbuzi wa uhakika na kwa wakati. Chombo hiki ni kipya, lazima tukiunge mkono. Sisi katika Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kukilea. Naomba vyama vya wafanyakazi na mifuko ya hifadhi kukipa ushirikiano unaostahili ili kiweze kufanikisha majukumu yake ipasavyo.


Kuhusu mchakato wa Katiba, napenda kuwahakikishia kuwa hakuna atakayebaguliwa. Tunataka watu wote wapate fursa ya kushiriki. Jipangeni kushiriki kwa ukamilifu. Tusiruhusu watu wachache wanaotaka kuhodhi mjadala huu kwa kutaka maoni yao tu ndiyo yasikilizwe na kuwazuia wengine wasitoe maoni yao. Tukiruhusu tabia hiyo huenda tusipate Katiba ambayo itawakilisha maoni ya wengi bali kikundi fualni kilicho hodari kupiga kelele bila hoja.


Hitimisho
Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi na Ndugu Wafanyakazi;
Nimezungumza kwa muda mrefu. Nimejitahidi katika hotuba yangu kutoa maelezo ya ufafanuzi kwa takriban kila jambo lililotajwa katika risala yenu. Yapo baadhi ambayo sikuyazungumzia lakini siyo kwamba nimeyapuuza. Kila jambo mlilolitaja tutalifanyia kazi. Nia yetu ni kujenga nchi yetu na katika kufanya hivyo natambua kuwa wafanyakazi ni mhimili muhimu sana. Ni wajibu wetu kuwasikiliza, ni wajibu wetu kushirikiana nanyi na ni muhimu kushughulikia musuala yenu ipasavyo. Kila mmoja wetu anamuhitaji mwenzake. 



Narudia tena kuwahakikishia ushirikiano wangu binafsi na ule wa wenzangu wote Serikalini wakati wote.
Naomba nimalize kwa kusema kuwa kwa ushirikiano na mshikamano baina ya utatu wetu, yaani Wafanyakazi, Waajiri na Serikali hakuna litakalotushinda na hakuna mfanyakazi wa Tanzania atakayekuwa mtumwa katika nchi yake.
Nawashukuru tena viongozi wa TUCTA kwa kunialika kwenye sherehe hizi muhimu. Hongereni kwa sherehe zilizofana sana. 


Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania !
Asanteni kwa Kunisikiliza.

No comments: