Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze
kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza
nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. Leo
ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais
wa China Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Jambo
la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China
aliyoifanya nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. Lengo la ziara yake
ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na
Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii
kuwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe
wake. Wameondoka wakiwa na kumbukumbu
nzuri ya nchi yetu na watu wake.
Kwa niaba yenu, nimepokea salamu za shukrani kutoka kwa
Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa na mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba
tuendelee kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni wetu wengine mashuhuri
watakaotutembelea siku za usoni.
Ndugu wananchi;
Nami pia,
nimemshukuru sana Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya
ziara ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa
na kumbukumbu isiyosahaulika. Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu baada ya
kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake. Na,
kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya
China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi wake.
Tumefarijika sana
kusikia kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi
wapya wa China. Pia, kuwa China
itaendelea kukuza biashara na uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa
Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000 za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi zetu mbili zilitiliana
saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya
kipaumbele nayo imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais Xi Jinping
alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti
cha China ya kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na
China. Kama mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi
zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa
Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na Waziri
Mkuu wake Chou En Lai.
Rais wa China
aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya
kimataifa na kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza
misaada ya maendeleo. Katika miaka 49 ya
uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo ikiwemo
Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na Rais
Xi Jinping wakati wa ziara yake.
Ndugu wananchi;
Kuna miradi kadhaa
mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa
Serikali ya China. Wakati wa ziara yake,
Rais Xi Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo kama
tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku
ile.
Ajali ya Kuporomoka Jengo la
Ghorofa
Jijini Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Jambo la
pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la
Dar es Salaam. Ajali hiyo iliyotokea
juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana. Watu 17
waliweza kuokolewa, wanne kati yao
bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na
sasa inakaribia kufikia ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Mimi na viongozi
wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona pale imenihuzunisha
sana. Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba
nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na
wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum
kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake
madhubuti. Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya
ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote
walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza
pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali
nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa,
ndugu na jamaa zao katika ajali hii.
Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea
marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi.
Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno
mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile.
Alimradi kila mtu ana dhana yake.
Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza
sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua zipasazo. Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa
kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila
ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni
kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo
wajibu wake. Naamini kama mamlaka hizo
zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika. Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu
maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao.
Watimize wajibu wao. Yaliyotokea
Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote.
Ndugu Wananchi;
Ni
matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa
Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane. Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na
Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe kwa
ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe. Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha
ajali za aina hiyo siku za usoni.
Uhusiano wa
Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
Jambo la
tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo
nchini. Jambo hili nimeshalizungumzia
mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali
ilivyo sasa. Tumefikia mahali ambapo
kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili
muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya.
Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na
Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana
itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa
cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali
zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini
haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo
zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba
kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo
viovu dhidi ya dini yake. Kauli na
mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma
moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini
ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali
kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya
kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao
kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali
imeshindwa kulinda uhai wa raia wake.
Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa
kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa,
kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yo yote ya
maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa
sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo.
Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi
wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo
kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga Makanisa na shule za
Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi
kushiriki maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu
hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife.
Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said
Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza,
hatupendelei upande wo wote. Hatufurahishwi
na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa
dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa
mashtaka kwa nyakati mbalimbali. Vyombo
vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu
katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya
Serikali. Mtakumbuka kuwa mara kadhaa
nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha
ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi binafsi sibagui,
hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose
nafasi kwa sababu nyinginezo.
Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume
Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo
mengi. Nimeshashiriki mazishi ya
Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na
Wakristo. Pale ambapo sikushiriki
mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli
nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika
mara mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es
Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda
pengine siyo nyepesi. Wakristo hawana
utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa
Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi wa dini na
nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo,
tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za
ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini
hivyo sivyo. Nawasihi sana ndugu zangu
Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji
Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule Zanzibar,
au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa
risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala,
Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza
wajibu wake.
Kila tukio lina mazingira
yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali kuzembea. Hakuna ushahidi wa matukio hayo
kuunganika. Mpaka sasa hatujapata
ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na
kuchoma moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo
Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati ya
Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo
iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa nyama
iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi
na vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji
kupoteza maisha. Si tukio unaloweza
kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la
pale pale Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa
Buseresere kwa sababu zao.
Hivi kama kusingekuwepo na
mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale yangetokea?
Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina
yao. Walikuwa wanaishi kidugu na
kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja
akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake.
Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa
Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa Wakristo wote nchini kulikofanywa na
Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili.
Busara ituongoze kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa
Buseresere wazungumze, waelewane na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa
awali. Hata mzozo wa kuchinja wanaweza
kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo
na watu hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya
Wakristo na Waislamu nchi nzima si sawa.
Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa
Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la Buseresere,
Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu nani
achinje. Bado uchunguzi wake unaendelea
na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje vishirikiane na vyetu kufanya
uchunguzi. Tumefanya hivyo kwa sababu ya
ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla yake. Yaani ile la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa
Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh
Fadhili Soroga. Bado hakuna mafanikio ya
kutia moyo. Na bado tunajiuliza kama
matukio hayo matatu yanahusiana. Je,
Makanisa kuchomwa moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale
matatu? Uchunguzi unaoendelea unaweza
kufumbua fumbo hilo.
Kuna watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu
nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya
kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika.
Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama vya
nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje.
Katika mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu ye yote na
kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo,
na haina sababu ya kufanya hivyo. Ndiyo
maana tunahangaika usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es
Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba,
2012 nalo lina mazingira yake maalum.
Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja
Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu. Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi wa
kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu. Kijana huyo alifikishwa kituo cha
Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo
mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi
na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale, wakaenda
kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
Baada ya tukio la Mbagala
hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika
la watu kutaka kuchoma Kanisa popote.
Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia
mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe
wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na
hata hatua za tahadhari kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja
iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli.
Hata dalili hazijakuwepo.
Tulichojifunza ni kuwa ujumbe
na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu. Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao
Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo
wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba mtanabahi na
mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka
kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa faida
yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la
kutaka Wakristo na Waislamu wagombane.
Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili
ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake.
Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu
mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu
kati ya Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu.
Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na
kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa
na kesi zao zinaendelea Mahakamani. Kwa
upande wa tukio la Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo
Kachila, watu 17, wakiwemo waumini
wa dini ya Kikristo na Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo
walioshitakiwa kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu
wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa
Zanzibar, watu 10 wanaotuhumiwa
kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la
kuchoma Kanisa baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa kwa
Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika pamoja na kuwapo taarifa kadhaa
zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu
uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni
pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya aina hii,
hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu mmoja
amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kanda na vituo
vya redio nako pia Serikali imechukua hatua.
Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika maeneo
mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na kusambaza kanda zinazochochea chuki na
vurugu za kidini. Wapo Waislamu na
Wakristo. Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia
nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani
Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha
Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui
ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali
inajali usalama wa raia wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa
yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kuhakikisha
kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi zote na mahali po pote
walipo wako salama. Tunataka kuona watu
wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama
tulivyokuwa tunaishi siku zote.
Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza
yale yanayowaunganisha. Tujiepushe
kuyapa kipaumbele yale yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
Athari za
mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si ndwele,
tugange yajayo. Hebu tufikirie maisha
yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe,
harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na
Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo pawe na majiko mawili au labda hata
mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko
na mabwalo ya Waislamu na Wakristo. Hali
iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine yenye huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka
kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini
tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na kila
jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena. Huko tunakoelekea siko, ni kubaya.
Tubadilike, na wakati ni huu. Viongozi
wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na janga hili.
Ndugu Wananchi;
Bado
narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa mbili kukutana na
kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi.
Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya matatizo haya. Ni masuala yanayohusu imani za dini na
yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao. Serikali ina wajibu wa kulinda amani. Kazi
yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo vitakavyosababisha
uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi baya ni viongozi wa
dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa madhehebu
na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo
hilo. Nimepata faraja kuona kuwa wote
wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi wa
dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza. Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya
kawaida kwa Tanzania na Watanzania. Kuna
upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa
kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake
katika maisha tuliyoyazoea. Maisha
ambayo waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano
na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo
Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi wa dini
mapema mwezi ujao. Ni matumaini yangu
kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya kutuma wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa
letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu
napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari wasaidie
kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na
kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu.
Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au
kuzitangaza. Wawe makini na maneno
wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa
lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa
Watanzania wa dini zote. Wasipofanya
hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna msingi kama
ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba
wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo
vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na
Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba
kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha umoja na mshikamano
wetu. Tuishi kwa upendo, umoja,
mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu, kabila, rangi au
mahali atokako mtu. Hizo ndizo tunu za
taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na kuzidumisha.
Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini yo yote na wala haina
mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini wao. Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama
itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama
inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu
anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi. Hatua zipasazo zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema
ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na
utulivu. Tusherehekee pamoja.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment