Masiku ya kumi
la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani, yana fadhila na khususia nyingi
kathiri, miongoni mwake ni pamoja na kwamba:
i. Ndani ya masiku
hayo umo usiku wa cheo/heshima, ambao huo ni bora kuliko miezi alfu moja. Na ye
yote atakaye simama kufanya ibada katika usiku huo, kwa kumuamini Allah kikweli
na kwa kutaraji ujira kutoka kwake, huyo atasamehewa dhambi alizokwisha
zitenda.
ii. Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akijitahidi sana kufanya amali ndani ya
masiku hayo kuliko siku nyingine. Kama alivyosema Bi. Aysha-Allah amuwiye
radhi-alikuwa akiyahuisha masiku haya kwa kusoma Qur-ani, kuleta dhikri,
kuswali na kuomba dua halafu ndipo hula daku. [Rejea SAHIH MUSLIM]
iii. Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-alikuwa linapoingia kumi la mwisho, hufunga kibwebwe (yaani
hujitenga na wakeze ili apate faragha ya ibada). Akauhuisha usiku wake na
akawaamsha wakeze kufanya ibada pamoja nae. Mtume alikuwa akisimama kufanya
ibada katika kumi hili bila ya kulala, zoezi hili hakupata kulifanya katika
masiku mengine. Alikuwa akifanya hivyo kwa lengo la kuvuna ujira unaobubujishwa
ndani ya masiku hayo na kuiwania Laylatul-Qadri.
iv. Katika
jumla ya khususia (mambo pweke yapatikanayo humo) ni kwamba Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikaa itikafu msikitini ndani ya kumi
lote hili la mwisho bila ya kutoka ila kwa haja/dharura kuu.
Fadhila/ubora wa Laylatul-Qadri:
Allah Taala ameujaalia usiku huu kuwa ndio bora ya masiku yote na akautaja vema
katika kitabu chake kitukufu, akasema: "HAKIKA TUMEKITEREMSHA (kitabu
hicho) KATIKA USIKU ULIOBARIKIWA. HAKIKA SISI NI WAONYAJI. KATIKA USIKU HUU HUBAINISHWA
KILA JAMBO LA HIKIMA". [44:3-4] Usiku mbarikiwa unaotajwa na aya hii ni
usiku wa Laylatul-Qadri upatikanao ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Usiku
huu umebarikiwa kwa sababu ya kheri, baraka na fadhila zipatikanazo humo. Na
katika jumla ya baraka za usiku huo ni kushushwa kwa Qur-ani Tukufu ndani yake.
Halafu tena Allah Taala akausifia usiku huo kwamba linabainishwa ndani yake
kila jambo la hekima. Yaani mambo hupambanuliwa na kugurishwa kutoka katika
"Lauhul-Mahfuudh" uliohifadhi mambo yote hapo. Wakapewa malaika
waandishi kuandika mambo yote yatakayotokea ndani ya mwaka mzima, tokea masuala
ya riziki, vifo na kadhalika.
Na katika kuonyesha ubora wa usiku huu, Allah Taala
ameshusha sura nzima kwa jina la usiku huu, sura inayosomwa mpaka siku ya Kiyama,
akasema: "HAKIKA SISI TUMEITEREMSHA QUR-ANI KATIKA LAYLATUL-QADRI; USIKU
WA CHEO KITUKUFU. NA NINI KITAKACHO KUJULISHA NINI LAYLATUL-QADRI?
LAYLATUL-QADRI NI BORA KULIKO MIEZI ELFU. HUTEREMKA MALAIKA NA ROHO KATIKA
USIKU HUO KWA IDHINI YA MOLA WAO MLEZI KWA KILA JAMBO. AMANI USIKU HUO MPAKA
MAPAMBAZUKO YA ALFAJIRI". [97:1-5] Allah akazitaja fadhila za usiku huu
ndani ya sura hii, kwamba:
i. Huo ndio usiku
ulimoshushwa ndani yake Qur-ani Tukufu kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu.
ii. Huo ni usiku
bora kuliko miezi elfu moja (miaka themanini na tatu).
iii. Malaika hushuka
ndani ya usiku huo wakileta kheri, baraka na rehema za Allah kwa waja wake.
iv. Usiku huo ni
usiku wa amani tupu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema kuhusiana
na usiku huu mtukufu: "Atakayesimama (kufanya ibada katika) usiku (wa)
Laylatul-Qadri, kwa imani na kutarajia ujira kutoka kwa Allah. Atasamehewa
dhambi zake zilizotangulia". Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
Wakati wa Laylatul-Qadri:
Usiku huu mtukufu wa Laylatul-Qadri unapatikana ndani ya mwezi mtukufu wa
Ramadhani kila mwaka mpaka kusimama kwa Kiyama. Umo ndani ya kumi la mwisho la
mwezi huu na hutarajiwa zaidi katika nyusiku za witri; yaani mwezi 21, 23, 24,
25 ,27 na 29. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: "Izengeeni
Laylatul-Qadri katika kumi la mwisho la Ramadhani". Bukhaariy-Allah
amrehemu.
Na katika hilo kumi la mwisho, inatarajiwa zaidi
kupatikana ndani ya mwezi ishirini na saba, hili ni kwa mujibu wa kauli ya
Mtume-Rehema na Amani zimshukie: "...Basi ye yote atakaye kuizengea na
aizengee katika saba ya mwisho". Bukhaariy & Muslim-Allah
awarehemu.
Allah Taala ametufichia kujua usiku maalumu wa
Laylatul-Qadri kwa ajili ya kutuonea rehema ili tukithirishe amali njema katika
kuutafuta. Na kwa kufanya hivyo, mja huzidi kuwa karibu mno na Mola wake. Na
kumesuniwa katika usiku huu wenye baraka, kukithirisha dua na dua njema ya
kuombwa ndani yake ni ile Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliyo
mfundisha mkewe; Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi: "ALLAAHUMMA INNAKA `AFUWUN
TUHIBBUL-`AFWAA FA'AFU `ANNAA". Tirmidhiy-Allah amrehemu.
Source : http://www.uislamu.org/nasaha/ramadhani6.htm
No comments:
Post a Comment