SWALI:
Bibi na Bwana wameelewana kutumia
koil kukinga kupata mtoto kwa mda. Kisha bwana ameamua koil bibi akaitowe. Bibi
akamwambia bwana haya. Ikapita mdaa. Bwana akamuuliza bibi kama ile koil
ameitoa? Bibi akadaganya mumewe kwamba koil kesha itowa. Baadae siku kadha
bwana akamwambia bibi nafikiri kua koil hujaitoa umenidaganya. Na kama
umenidaganya jua nishakuwacha. Bibi ana watoto watatu. WA miaka mitatu, na
miwili na mmoja. Kazi ya ulezi pekee yake. Sababu bwana anafanya kazi kuazia
jumatatu hadi ijumaa. Swala langu ni, jee huyu mwanake kishawachika?
Swala la pili kwa kua anahakika kua anatumia koil kutokupata mimba jee. Jee
akiachika anakaa edaa? Insha’Allah nitapata majibu ya
kuniridhisha. Asalaam aleikum.
JIBU:
Sifa zote njema
Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu
zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum) na
waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Shukran ndugu yetu kwa swali lako hilo
na kwa hakika haya maswali ya talaka ni mengi na ni nyeti. Kama tulivyokariri
mara kadhaa ya kwamba katika halali inayochukiza sana mbele ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni talaka. Hivyo, tunawanasihi
wanaume wasiwe ni wenye kufanya haraka au mzaha au kuegemeza masharti au sharti
katika mas-ala hayo ya talaka. Kwani Allah (Subhaanahu
wa Ta'ala) Anatuelezea umuhimu wa kukaa na wake zetu vizuri kama
Alivyosema:
“Na kaeni
nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Allaah
Ametia kheri nyingi ndani yake” (4: 19).
Talaka amepatiwa mume kwa ajili ya
utulivu wake na kuweza kusubiri na kuzingatia kabla ya kuchukua hatua yoyote
kama hiyo ambayo inaathiri familia na kizazi kijacho. Inabidi mume apatiwe
ushauri nasaha katika jambo la kuishi kwa wema na mkewe la sivyo basi matatizo
haya yataendelea kuwepo, nyumba kama hiyo itavunjika hivyo kuwaletea matatizo
watoto walioruzukiwa.
Inatakiwa kwamba mume na mke
wanapopeana ahadi iwe kila mmoja afanye juhudi kutekeleza upande wake na kama
panakuwa na matatizo ni lazima warudi tena katika meza na kushauriana na
kufikia suluhisho muafaka. Talaka katika hilo lililopitika katika suala la mume
na mke halikuwa ni suluhisho na inatakiwa mume aangalie maslahi ya mke ili
kusiwe na matatizo.
Uongo katika Uislamu ni mbaya na ni
miongoni mwa sifa za unafiki kwa mwenye kulifanya hilo. Na ni kosa ambalo Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa Muumini hawezi
kuwa ana sifa hiyo japokuwa anaweza akafanya kosa jengine. Kwa kosa hilo
anatakiwa mke aombe msamaha kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na atubie
Kwake na asirudie tena kosa hilo na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasamehe
madhambi yote. Lakini mbali na kusema hayo swali la talaka katika hili suala
lako bado limebakia pale pale na hili haliwezi kuondolewa kwake yeye kutubia.
Kama ulivyoashiria katika swali lako
kuwa tayari mume amempatia talaka ya sharti na hivyo hiyo ni talaka moja tu
ambayo bado ina fursa ya wao wawili kurudiana.
Katika talaka hii ambayo imetolewa
na mume ni kuwa imeekewa sharti – “Bwana
akamuuliza bibi kama ile koil ameitoa? Bibi akadaganya mumewe kwamba koil kesha
itowa. Baadae siku kadha bwana akamwambia bibi nafikiri kua koil hujaitoa
umenidaganya. Na kama umenidaganya jua nishakuwacha”. Hapa tunapata sharti moja:
1.
Ikiwa umenidanya jua nishakuacha.
Kwa muhtasari ni kuwa mke
keshaachika na inabidi akae eda yake ya tohara tatu ambayo ni takriban miezi
mitatu kufuata miandamo ya mwezi. Katika kipindi hiki cha eda, mume ikiwa hiyo
ni talaka ya kwanza au ya pili anaweza kumrudia mkewe lakini ni nasaha yetu
kuwa mtu au watu wenye uzoefu wazungumze na huyu bwana ili asiwe ni mwenye
kuweka masharti kama hayo bali wawe ni wenye kushauriana na mkewe pindi
anapoona kuna haja ya jambo fulani kufanyika katika njia fulani. Na pia mke
anasihiwe asiwe ni mwenye kudanganya bali awe wazi kwa mumewe ili matatizo kama
hayo yasiwe ni yenye kutokea tena katika maisha yao ya unyumba.
Tunamuomba Allah (Subhaanahu
wa Ta'ala) Awape maelewano na masikilizano ili watu hao wawili warudi
katika hayo yao ya awali kama mume na mke, na pia Awape hamu ya kushauriana
katika mas-ala yote nyeti ili matatizo hayo yasiwe ni yenye kutokea tena.
Na Allaah Anajua
zaidi.
No comments:
Post a Comment