Monday, September 28, 2015

ASILI YA ROHO (NAFSI) ZETU

Kuna umuhimu mkubwa wa kuzungumzia kuhusu roho (nafsi) zetu ambazo zinahitaji kutoharishwa  ili ziwe  katika hali   ya asili yake, (kama zilivyokuwa kabla ya kupulizwa katika mwili wa binaadamu)   na ambazo ndio zitakuwa sababu ya kufaulu  au kufeli kwetu duniani na akhera.  
((وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّن الْعِلْمِ إِلاَّ قَلِيلاً))
((Na wanakuuliza (ewe Muhammad)  khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu))   [Al-Israa::85] 

Roho   ni siri Yake kubwa Allaah سبحانه وتعالى  kwani hata  mtu awe  mtaalamu au hodari  wa hali ya juu kabisa, lakini  hatoweza kuumba hata chembe ya kidudu.   Allaah سبحانه وتعالى   Ametoa changamoto kubwa sana kwa wale wote ambao wanaabudu miungu isiyokuwa Allaah سبحانه وتعالى  kwa kuwapa mfano mdogo wa aina yake! Kuwataka kuwaonyesha kuwa hao miungu wanaowaabudu si lolote si chochote na hawawezi kuwasaidia wao wenye kuwaabudu bali hata kujisaidia wenyewe!! Na matokeo yake ni udhalili wa kudumu. 
((يَا أَيُّهَا النَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌ فَاسْتَمِعُوا لَهُ إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ))
((Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa)) [Al-Hajj:  73] 
Allaah سبحانه وتعالى alikusanya kizazi chote cha Adam عليه السلام  (kabla ya kuwaumba  duniani)  na  wakati huo  roho zao zilikuwa ni  safi kabisa zilizo katika "Fitrah" (maumbile ya asili ya Uislam).  Nasi (viumbe) tukashuhudia na kuchukua ahadi kwamba tutamtii Mola wetu.  
((وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَى أَنفُسِهِمْ أَلَسْتَ بِرَبِّكُمْ قَالُواْ بَلَى شَهِدْنَا أَن تَقُولُواْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ))
((Na pale Mola wako Mlezi Alipowaleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na Akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Ndiye! Tumeshuhudia (kuwa Wewe ndiye Mola wetu) (Allaah Akawaambie). Msije mkasema Siku ya Qiyaamah sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo))  [Al-A'araaf :172]
Hali hiyo ya 'Fitwrah' ina maana kwamba, Allaah سبحانه وتعالى Katuumba katika hali ya kuikubali dini Yake na kutupa Imani ya kuamini Tawhiyd,  (kuwa Yeye ni Mungu Mmoja pekee hana mshirika) Aayah hii ifuatayo, Anatuamrisha tuelekee katika hii dini tukufu ya Kiislamu iliyo na muongozo kamili kwa viumbe wote.
((فأقم وجهك للدين حنيفا فطرة الله التي فطر الناس عليها لا تبديل لخلق الله))
((Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Allaah Alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Allaah. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui)) [Ar-Ruum:30]
Mtume صلى الله عليه وسلم ametuthibitishia haya kwa kubainisha kuwa ni wazazi wa mtoto ndiyo  wanaobadilisha Fitrah hiyo:
عن أبا هريرة رضي الله عنه كان يحدث : قال النبي صلى الله عليه وسلم : ((ما من مولود إلا يولد على الفطرة، فأبواه يهودانه أو ينصرانه أو يمجسانه، كما تنتج البهيمة بهيمة جمعاء، هل تحسون فيها من جدعاء)). ثم يقول أبو هريرة رضي الله عنه :  ((فطرة الله التي فطر الناس عليها))   أخرجه البخاري و مسلم
 Imetoka kwa Abu Hurayrha رضي الله عنه ambaye alisema : Mtume صلى الله عليه وسلم amesema; ((Kila kizazi (mtoto mchanga) anazaliwa katika 'Fitwrah' kisha wazazi wake humbadilisha na kumuingiza katika dini ya Uyahudi, au Unasara au Umajusi, kama mfano  mnyama mwenye pembe anavyomzaa mnyama mwenye pembe kama yeye, je, mtaona (mtahisi) kuwa hana pembe (na hali anayo)?)) Kisha Abu Hurayrah akasoma Aayah isemayo: ((Ndilo umbile la Allaah Alilowaumbia watu))  [imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]     
Baada ya kutuumba Allaah سبحانه وتعالى kwa Rahma Yake  Akatutumia uongofu  (ambao ni Mitume Yake na vitabu Vyake)  uwe unatukumbusha kila mara tuimarishe Imani zetu na   kutuongoza  katika  njia iliyo nyooka sawasawa.   
))فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلا يَشْقَى((
((Na ukikufikieni Uongofu kutoka Kwangu basi atakayeufuata uongofu Wangu, hatapotea wala hatataabika)) [Twaahaa:122]
Kufuata uongofu huo vile vile ni kama mtihani kwetu  Apate kupambanua  Allaah سبحانه وتعالى  nani katika sisi atakuwa bora Kwake.
((الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا))
((Ambaye Ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi)) [Al-Mulk:2]
Lakini ni hiari ya mtu kuufuata huo uongofu au kuupuuza na kupotea katika njia mbaya.
((هَلْ أَتَى عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا)) ((  إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا)) ((إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورً))
((Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa)) ((Hakika Sisi Tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika, Tumfanyie mtihani. Kwa hivyo Tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona)) ((Hakika Sisi Tumembainishia njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru)) [Al-Insaan:  1 – 3]   
 Baada ya kutuumba kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika, yaani mwanamke anaposhika mimba na inapofika   miezi minne Allaah سبحانه وتعالى humtuma Malaika wake kupuliza roho ya huyo kiumbe akawa sasa ni binaadamu, na Malaika huyo huamrishwa kumuandikia mambo manne:  
عن أبي عبد الرحمن عبد الله بن مسعود -رضي الله عنه- قال حدثنا رسول الله -صلى الله عليه وسلم- وهو الصادق المصدوق:  ((إن أحدكم يُجمع خلقه في بطن أمه أربعين يوماً نطفة، ثم يكون علقة مثل ذلك، ثم يكون مضغة مثل ذلك، ثم يرسل إليه الملك فينفخ فيه الروح، ويؤمر بأربع كلمات: بكتْبِ رزقه، وأجله، وعمله، وشقي أو سعيد، فوالله الذي لا إله إلا غيره إن أحدكم ليعمل بعمل أهل الجنة حتى ما يكون بينه وبينها إلا ذراع فيسبق عليه الكتاب فيعمل بعمل أهل النار فيدخلها، وإن أحدكم ليعمل بعمل أهل النار حتى ما يكون بينه وبينها إلا ذراع فيسبق عليه الكتاب فيعمل بعمل أهل الجنة فيدخله))ا   رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwa Abu 'Abdur-Rahmaan 'Abdullaah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Ametuelezeza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa ((Hakika kila mmoja hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. WaLlaahi naapa kwa Yule Ambaye hakuna mungu isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye vitendo vya watu wa Peponi hadi ikawa baina yake na pepo ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya vitendo vya watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa peponi akaingia peponi.)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hapa tena itakuwa ni vitu viwili vimekusanyika,  nafsi na mwili na ndio maana mtu anapokufa tunasema 'fulani amefariki'.  Neno la kufariki ina maana kutengana, yaani roho imetengana na mwili na kila kitu kinarudi kule kwenye asili yake.  Roho inarudi juu kwa Muumba wake na mwili unarudi ardhini kwenye udongo ambapo ndio chanzo cha kuumbwa kwake. 

KWA MSAADA WA www.alhidaaya.com

No comments: