Tuesday, February 26, 2013

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAM - MAUAJI YA PADRI



TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR KULAANI MASHAMBULIZI NA MAUAJI YA VIONGOZI WA DINI PAMOJA NA KUPINGA KAULI ZA UCHOCHEZI DHIDI YA ZANZIBAR
Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu Mlezi wa Viumbe. Sala na salamu zimfikie Mtume wetu Mtukufu Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake waongofu na wote wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya Malipo.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar lililokaa Jumapili tarehe 23/2/2013 katika kikao cha kutathmini matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini yakiwemo ya karibuni ya kupigwa risasi na kuuliwa Padri Mushi pamoja na kupigwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje na kuendelea kutolewa kwa kauli za uchochezi dhidi ya Zanzibar linatamka ifuatavyo:
1. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani vikali na kwa nguvu zote matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini likiwemo tukio la karibuni la kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi kulikofanywa na wahalifu wasioitakia mema Zanzibar.

2. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linapenda kuweka wazi kuwa uhai ni tunu kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyotunukiwa binaadamu hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiondoa haki hiyo isipokuwa yeye mweyewe Mwenyezi Mungu. Kutokana na ukweli huu ndio maana Sheria za Kiislamu zimeweka wazi mtu mwenye kumuuwa mwenziwe naye auliwe kama inavyoelezwa katika Kitabu kitufu cha Quran kama ifuatavyo:

“Na humo (katika Taurati) tuliwaandikia ya kwamba mtu (huuwawa kwa sababu ya kuuwa mtu) kwa mtu, ……….” (5:44)

Hivyo, vitendo vya kiharamia vya kushambuliwa viongozi wa Dini kulikoanzia kwa kumwagiwa tindi kali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje kwa dhulma kulikofanywa na wahalifu ni jambo lisilokubalika na Uislamu na Waislamu wenyewe. Aidha wahusika wa matendo haya wawe wafuasi wa Dini yoyote ile bado watahesabika ni wahalifu kwani vitendo vya kihalifu na kiharamia kamwe haviwezi kunasibishwa na Dini fulani.
3. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo husika kufanya upelelezi wa kina kuhusu matukio haya kwa kuzingatia uadilifu na misingi ya kazi zao ili kuwabaini wahalifu na kufikishwa katika vyombo vya kisheria. Aidha Baraza linavitahadharisha vyombo hivyo kuepuka kufanya kazi yao kwa kusukumwa na matashi binafsi, jazba, chuki, matashi ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Dini pamoja na shindikizo la baadhi ya vyombo vya habari.
4. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani na kupinga kwa nguvu zake zote kauli aliyoitoa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania na baadhi ya vyombo vya habari kuihusisha Zanzibar na ugaidi kutokana na tukio la kuuliwa Padri Mushi. Kauli hii inaonesha kuwa Mheshimiwa Waziri anaibagua Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu tunavyoelewa sisi suala la usalama wa nchi ni suala la Muungano hivyo huwezi kuihusisha Zanzibar pekee na suala la ugaidi. Hivyo, Baraza linaona kuwa kauli hizi zinazotolewa ni mbinu za makusudi za kuichafua Zanzibar katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na chuki binafsi dhidi ya Zanzibar na watu wake.
5. Aidha Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linamtaka Mheshimiwa Waziri kwa kulinda heshima yake kuwajibika kwa Watanzania kwa kujiuzulu kutokana na kushindwa kulinda usalama wa wananchi wakiwemo viongozi wa Dini ambao ndio walezi wa jamii.
6. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani kauli za uchochezi zinazoendelea kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari zinazochochea chuki, uadui, hasama na mtafaruku kati ya Waislamu na Wakristo na kusahau kuwa Waislamu wameishi na Wakristo kwa amani, mapenzi na mashirikiano hapa Zanzibar karne na karne. Baraza linaona kuwa vyombo hivyo vya habari vinatekeleza ajenda ya kuivuruga Zanzibar kwa kuchochea vita vya kidini ili kufikia malengo yao wanayoyajua wenyewe. Hivyo, Baraza linaiomba Serikali kuvidhibiti kwa kuvichukulia hatua vyombo vyote vinavyotumia matukio haya kuchochea uadui na chuki kati ya Waislamu na Wakristo.
7. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo vya habari vya Zanzibar kuwajibika kwa Wazanzibari wanaolipa kodi kwa kuwapasha taarifa sahihi juu ya matukio muhimu yanayotokea katika jamii yao badala ya wananchi kutegemea kupokea taarifa za upotoshaji na uchochezi kutoka katika vyombo vya habari visivyotutakia mema.
8. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaziomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kuwasilisha kwa Watanzania taarifa ya wazi ya matokeo ya uchunguzi wa matukio haya kwa kuanzia na lile la kumwagiwa tindi kali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje.
9. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linawaomba Wazanzibari wote kuwa watulivu katika kipindi hichi ambapo upelelezi wa matukio haya ukiendelea. Aidha Baraza linawasihi Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti zao za kidini kulinda umoja wao na kudumisha amani pamoja na kukataa kugawanywa ili kuwatoa katika ajenda yao ya msingi ya kudai Mamlaka Kamili ya Zanzibar katika Muungano.

MOLA WETU MTUKUFU TUNAKUOMBA UINUSURU ZANZIBAR NA WATU WAKE DHIDI YA MAADUI WA NDANI NA NJE WASIOITAKIA MEMA NCHI YETU
Imesainiwa na:

Sheikh Ali Abdalla Shamte

Amir wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar


Saturday, February 23, 2013

MWENYEZI MUNGU HUPOKEA TOBA ZA WANADAMU USIKU NA MCHANA


Hadiyth Ya 2, Katika kitabu cha Hadithi za Mtume (s.a.w.): LU-ULU-UN MANTHUWRUN 
Allaah Hupokea Tawbah Za Waja Usiku Na Mchana

عَنْ أَبِي مُوسَى عَبْدِ الله بنِ قَبَسٍ الأَشْعَرِيِّ  (رضي الله عنه) عن النَّبيّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قال: ((إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abu Muwsaa ‘Abdillaah bin Qays Al-Ash‘ariyy (رضي الله عنه)  kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Anakunjua Mkono Wake usiku ili Apokee tawbah ya mkoseaji mchana. Na Anakunjua Mkono Wake mchana ili Apokee tawbah ya mkoseaji usiku mpaka jua lichomoze Magharibi [mahali linapokuchwa]))[1]

Mafunzo Na Hidaaya:
  1. Umuhimu wa mja kukimbilia kutubu anapofanya maasi mchana au usiku. [At-Tahriym 66: 8, An-Nuwr 24: 31].
وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ
Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Mola wenu na Jannah upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye taqwa[2]
  1. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake kuwapa muda wa kutubia maasi, lau sivyo Angeliwaadhibu na kuwaangamiza hapo hapo wanapotenda maasi. [Faatwir 35: 45, An-Nahl 16: 61].
  1. Rahma ya Allaah kwa waja Wake kutokutofautisha wakati wa tawbah japokuwa maasi mengine yanazidi mengineyo. 
  1.  Tawbah inaendelea kupokelewa hadi milango ifungwe: [Hadiyth: ((Hakika Allaah Huikubali tawbah ya mja Wake kabla ya roho kufika kwenye mkoromo wa mauti))[3] ((Atakayetubu kabla ya kuchomoza jua upande wa Magharibi, Allaah Atamkubalia tawbah yake)).[4]
  1. Hii inaonyesha mahaba makubwa ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuwapatia fursa hii ya dhahabu ambayo haifai kupotezwa na waja wenyewe.
  1. Hadiyth inatoa mafunzo kwa Muislamu kutokumhukumu mwenziwe kuwa hatoghufuriwa madhambi yake. [Rejea Hadiyth namba 99].
  1. Mja hata afanye madhambi makubwa vipi, asikate tamaa na Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى), kwani Yeye Hughufuria madhambi yote. [Az-Zumar 39: 53]



[1]  Muslim.
[2]  Aal-‘Imraan (3: 133).
[3]  At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad, na imepewa daraja ya Swahiyh na Al-Albaaniy.
[4]  Muslim.

Wednesday, February 20, 2013

PICHA KATIKA MAZISHI YA PADRE ALIYEUAWA KWA RISASI ZANZIBAR


  Wanafunzi wa skuli ya Kikristu wakihudhuria ibada ya Mazishi ya Mchungaji Evaristus.G.Mushi iliofanyika katika Kanisa la Minara Miwili liliopo Shangani Mjini Zanzibar,Mchungaji alifariki Dunia Baada ya Kupigwa Risasi na Watu wasiojulikana huko Beitrasi Mjini Zanzibar.



    Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akisalimiana na Askofu wa Kanisa katoliki Zanzibar Augustino Shao mara alipowasili katika Kanisa la Minara Miwili liliopo Shangani Mjini Zanzibar ili kuuwaga Mwili wa Marehemu Mchungaji Evaristus.G.Mushi aliefariki kwa kupigwa Risasi na watu wasiojulikana huko Beitrasi Mjini Zanzibar.




   Waumini wa Madhebu mbalimbali wakimiminika katika Kanisa la Minara Miwili liliopo Shangani Mjini Zanzibar ili kuuwaga Mwili wa Marehemu Mchungaji Evaristus.G.Mushi aliefariki kwa kupigwa Risasi na watu wasiojulikana huko Beitrasi Mjini Zanzibar.




Jeneza lililobeba Mwili wa Marehemu Mchungaji Evaristus.G.Mushi likipelekwa katika kaburi kwa ajili ya mazishi ambayo yalifanyika huko katika kijiji cha Kitope wilaya ya Kaskazini B Zanzibar.   

    Mazishi ya Mchungaji Evarist Mushi yamefanyika leo tarehe   
     20/02/2013 Zanzibar.
  
    Picha na Zanzibar Daima Blog.