Saturday, April 6, 2013

Watuhumiwa Kesi ya Sheikh Ponda‘wawakaanga’ Polisi mahakamani

 
 
Gazeti la ANNUUR Na. 1061
RABBIUL THAN 1434,
IJUMAA MACHI 8 - 14, 2013
Na Bakari Mwakangwale

Watuhumiwa Kesi ya Sheikh Ponda‘wawakaanga’ Polisi mahakamani

Wadai walivamiwa msikitini wakiwa katika ibada.
Waikana BAKWATA na kudai hawazijui kazi zake.
Wasema kiongozi wao ni Qur’an na Sunna za Mtume

MASHAHIDI wa upandewa utetezi katika kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda, wamedai askari Polisi waliwavamia na kuwapiga wakiwa katika ibada ya Itiqafu, ndani ya Msikiti wa MarkazChang’ombe, jijini Dar esSalaam, usiku wa Oktoba16, 2012.

 
Mashahidi hao ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo namba 145/2012, walitoa madai hayo mbele ya HakimMkazi wa Mahakama yaKisutu, Bi. Victoria Nongwa, walipokuwa wakitoa ushahidi wao mahakamani hapoJumatano wiki hii, na kueleza kuwa wanakana mashtaka yote yanayo wakabili. Mbali na madai hayo, washtakiwa hao ambao kila mmoja alipanda kizimbani kutoa utetezi wake, kwa ujumla walilikana BAKWATA, wakidai wanaisikia tu lakini hawaitambui pamoja na Mufti Sheikh Shaaban Simba.Wakiongozwa na Wakiliwao Bw. Juma Nassoro, mashahidi hao walisemakwamba walifika katika Msikitiwa Markaz Chang’ombe kwa lengo la kufanya ibada ya Itiqafu, yenye fadhila nyingi miongoni mwa ibada za Kiislamu. Walidai pamoja na kujiandaa na ibada hiyo, hawakuweza kuitekeleza kwani ilipofika majira ya saa tisa usiku, muda ambao ndio muafaka kwa ibada hiyo, walisikia vishindo, geti kuvunjwa na kisha mlango na madirisha ya Msikiti kuvunjwa na askari kuingia ndani na viatu vyao na kuanza kuwashambulia. Shahidi namba moja Bi. Kulthumu Mfaume, ambaye pia ni mshtakiwa namba mbili, akiwa kizimbani aliiambia Mahakama kuwa alisikia kuna ibada ya Itiqafu katika Chuo Cha Kiislamu Markazi, ndipo alipolazimika kwenda kwa ajili ya Ibada hiyo. “Usiku tulishtuka baada ya kusikia geti likivunjwa na mara mlango wa Msikiti nao ulibamizwa na kuvunjika, kasha niliona askari wakiingia ndan ina mabuti yao, walitupiga sana na walikuwa wanaume tupu, kisha walituingiza katika magari yao” Alisema Bi. Kulthumu. Bi. Kulthumu alisema pamoja na kujitetea kwamba wapo katika ibada ya Itiqafu na kuhoji kosa lao ni nini, alidai askari hao hawakuwaelewa na walizidisha kipigo. Akijibu maswali ya Wakili wa Serikali, Bw. Tumaini Kweka, kwamba alipataje taarifa za ibada hiyo ya Itiqafu, Bi. Kulthumu alisema akiwanjiani alisikia wakitangaza Msikitini, na kwa kufahamu umuhimu wa ibada hiyo alilazimika kwenda. Alipoulizwa ni nani kiongozi wake, Bi. Kulthumu alijibu hana kiongozi bali yeye huongozwa na Qur’an na Sunna za Mtume Muhammad(s .a .w). Kwa upande wake, shahidi namba mbili Bi. Zainab Mohammed (50), ambaye katika kesi hiyo ni mstakiwa namba tatu, akitoa ushahidi wake alisema alikamatwa na askari Polisi akiwa katika Ibadaya Itiqaf ndani ya Msikiti waChuo Cha Kiislamu Markazi Chang’ombe, na alipata kipigo kutoka kwa askari hao. Kuhusu ni wapi alipata taarifa za ibada hiyo, alisema alipata kupitia kwa muumini mwenzake, ambapo baadaya kufika hapo Markaz, hakufanya shughuli yoyote zaidi ya kufanya ibada ndani ya Msikiti huo. Alipoulizwa ni nani mmiliki wa eneo alilokamatiwa, alisema kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, anafahamu kuwa Misikitiyote ni mali ya Waislamu na kila Muislamu ana haki ya kufanya ibada yoyote. Shahidi namba tatu Bi.Zaidani Yusuph (66), aliieleza Mahakama kuwa wakati alipokuwa ndani ya Msikiti Markaz Chang’ombe kwa ajili ya ibada ya Itiqaf Oktoba 16 mwaka jana, aliona askari wanaume wakiingia upande wa wanawake usiku baada yakuvunja geti na mlango wa Msikiti na kuanza kuwapiga. Shahidi huyo ambaye ni mshatakiwa namba nne, alisema kipigo alichopata kutoka kwa Polisi, alijeruhiwa kidole cha mguuni huku askari hao wakitoa maneno yakejeli. “Kwa umri wangu huu sikufanya ubishi wowote, lakini walinipiga licha ya kuwauliza kosa langu ni nini, walizidisha kipigo na walifanya unyama mkubwa.”Alisema Bibi huyo.Wakili wa Serikali Bw.Tumaini Kweka, alipomuuliza ni nani kiongozi wake akiwakama Muislamu, Bi. Zaidan alijibu kwa kujiamini kuwa kiongozi wake ni Qur’ an na Sunna na hata alipoulizwa nani msimamizi wake alisema hana zaidi ya Qur’ an. Wakili Kweka alipomuuliza kama anaifahamu BAKWATA, Bi. Zaidani, alisema, “Siijui, sitaki kuijua wala sitakikuisikia, hata huyo Mufti, simjui.” Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakim Bi. Victoria Nongwa, shahidi namba tano, Juma (22), alisema ilimlazimu kuacha ibada zake majira ya saa tisa usiku mara baada ya kusikia vishindo nje, kwani geti lilivunjwa ukafuatia mlango wa msikiti na kasha aliona askari Polisi wakiingia ndani ya msikiti. Alisema mara baada yakuingia msikitini walianza kuwapiga na kuamuru wafanye wanavyotaka wao. Aliongeza kuwa Walivamia bila kutoa tangazo lolote na kwamba, vurugu zao ndizo zilizokuwa ishara kuwa eneo hilo kwa muda huo halikuwa shwari.” Alisema Juma. Naye alipoulizwa kama anaifahamu BAKWATA, alisema anaifahamu kuwa ni Taasisi ya Kiislamu kama zilivyo taasisi zingine za dini. Baada ya kuulizwa kama ana mahusiano na chombo hicho alijibu kuwa haimuhusu. “Tukiwa ndani ya msikiti majira ya saa nane usiku kwenda tisa, tulisikia kishindo nje, kabla hatujakaa sawa tulisikia mlango wa msikiti ukibamizwa na mara waliingia askari kama wale (akionyesha baadhi ya askari FFUwaliokuwa mahakamanihapo) na waliingia na viatu vyao Msikitini.” Alisema shahidi huyo namba tano, Bi. Farida Lukoko (53). Bi. Farida ambaye ni mshitakiwa namba 7, alionyesha Mahakamani hapo alama za majeraha mikononi mwake, alisema kuwa alipigwa marugu mikononi na mgongoni, jambo ambalo alidai kuwa hadi sasa bado anasikia maumivu makali katika sehemu hizo. Alisema kipigo hicho kilimfanya asijitambue baadaya kuanguka chini. Baadaye alielezwa na wenzake kuwa alinyanyuliwa na askari haokwa kushikwa miguu na mikono kisha kurushwa ndani ya gari. Shahidi mwingine ambaye ni mshitakiwa namba tisa Athumani Salim, alipoulizwa kama anaifaham Bakwata, alisema anaisikia tu, lakini inajishughulisha na nini, hajui. Alipoulizwa ni wapi anapta taarifa za kuandama kwa mwezi, alisema Waislamu wanafunga na kufungua kwa mujibu wa Qur’an na Sunna, popote unapoandama au kwa kukamilika kwa idadi ya siku katika mwezi huo. Naye shahidi namba nane Adama Ramadhani (40), aliulizwa na mwendesha mashtaka wa Serikali Bw. Kweka, kama anafahamu kazi za Bakwata, alisema anachojua kazi yakekubwa ni kuwatangaziaWaislamu mwezi wa Ramadhani unapoandama na pindi unapomalizika na sivinginevyo. Kwa ujumla Mashahidi wote walidai Mahakamani hapo kuwa, hakuna shahidi yeyote upande wa mashtaka aliyewataja kuwa ni wavamizi wa kiwanja wanachoshutumiwa kuvamia. Washtakiwa hao wameanza kutoa utetezi wao Jumatano wiki hii kufuatia Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Bi. Victoria Nongwa, Jumatatu wiki hii kusema Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49, wana kesi yakujibu.Washitakiwa wote wanakabiliwa na makosa manne, isipokuwa mshtakiwa namba moja (Sheikh Ponda) na mshtakiwa namba tano (Ust. Mukadam), ambao wanakabiliwa na mashtaka matano. Hakimu Nongwa alisema pamoja na Mawakili wa upande wa utetezi kutoa maelezo ya kina katika utetezi wao juu ya shauri hilo, Mahakama imeona ni vyema iwape nafasi washitakiwa waweze kupanda kizimbani kutoa utetezi wao. “Mahakama inaona washtakiwa wote waliokamatwa katika kiwanja kile, ni vyema wapande kizimbani ili watoe utetezi wao, waseme sababu zilizofanya waingie pale.”Alisema Hakimu Nongwa. Kwa mujibu wa Wakili wa upande wa utetezi Bw. Juma Nassoro, ameieleza mahakama hiyo kuwa jumla ya mashahidi sitini watafika mahakani hapo kutoa ushahidi wao upande kwa upande wa utetezi.

No comments: