Laylatul-Qadr- Vipi Uweze Kuupata
Usiku Huu?
Tunakaribia
kuingia kumi la mwisho, kumi ambalo ndani yake kuna usiku unaojulikana kama
ni: Laylatul-Qadr. Ibaada yoyote itakayotendwa usiku huo, ni bora kuliko ibaada
ya miezi elfu.
Anasema Allaah (Subhaanahu
wa Ta'ala):
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ. إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي
لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ ﴿٢﴾ لَيْلَةُ
الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾ تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ
فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ ﴿٤﴾ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ
الْفَجْرِ ﴿٥﴾
BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym
(Kwa Jina la Allaah Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu). Hakika Sisi
Tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatil-Qadr (usiku wa cheo). Na nini
kitakachokujulisha ni nini huo (usiku wa) Laylatul-Qadr? (Usiku wa)
Laylatul-Qadr ni (usiku) mbora kuliko miezi elfu. Wanateremka humo Malaika na Ruwh
(Jibriyl) kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri (jambo). (Usiku huo ni) Amani
mpaka kuchomoza Alfajiri (Al-Qadr: 1-5)
Hadiyth mbali mbali
zimethibiti kuhusu fadhila za usiku huu mtukufu na pia hali ya Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilivyokuwa masiku kumi ya mwisho ya
Ramadhaan.
Hesabu ya thawabu za usiku
huo ni kama ifuatavyo:
Miezi elfu ni sawa na
miaka themanini na tatu na miezi mitatu takriban. (1000 ÷ 12 = 83.3)
Utakapokuwa umo katika
ibaada usiku huo wa Laylatul-Qadr, basi utaandikiwa thawabu za miaka 83! Juu ya
hivyo, ibaada ya usiku huo ni bora zaidi kuliko ibaada ya miaka themanini na
tatu.
Mazingatio kuhusu
Laylatul-Qadr:
Mwenye kukosa Laylatul-Qadr
atakula hasara kwa dalili ya Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَة
رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : لَمَّا حَضَرَ رَمَضَان قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى
اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ (( قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضَان شَهْرٌ
مُبَارَكٌ اِفْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ صِيَامَهُ تُفْتَح فِيهِ أَبْوَاب
الْجَنَّة وَتُغْلَق فِيهِ أَبْوَابُ الْجَحِيم وَتُغَلُّ فِيهِ الشَّيَاطِين
فِيهِ لَيْلَة خَيْرٌ مِنْ أَلْف شَهْر مَنْ حَرُمَ خَيْرهَا فَقَدْ حُرِمَ)) وَرَوَاهُ النَّسَائِيّ
Kutoka kwa Abu Huraryah
(Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba ilipofika Ramadhaan, Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa sallam) amesema: ((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa
Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni fardhi, milango ya Pepo hufunguliwa
na milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Katika mwezi huu, kuna
usiku ulio bora kuliko miezi elfu. Atakayenyimwa kheri zake, basi hakika
amenyimwa!)) [An-Nasaaiy]
Siku hiyo ni siku
iliyoteremeshwa Qur-aan. Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala):
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ. حم ﴿١﴾ وَالْكِتَابِ
الْمُبِينِ ﴿٢﴾ إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ ﴿٣﴾ فِيهَا يُفْرَقُ
كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ ﴿٤﴾ أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا ۚ إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ ﴿٥﴾
BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym
(Kwa Jina la Allaah Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu). Haa Miym. Na Kitabu
kinachobainisha. Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku uliobarikiwa,
(Laylatul-Qadr), hakika Sisi Tumekuwa Waonyaji. (Usiku) Huo hupambanuliwa kila
jambo la hikmah. (Ad-Dukhaan: 1-4).
Maana ya: “(Usiku) Huo
hupambanuliwa kila jambo la hikma” ina maana: Usiku huo wa
Laylatul-Qadr, majaaliwa yanahamishwa kutoka katika Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao
Uliohifadhiwa) kwenda kwa waandishi (Malaika) wanaoandika majaaliwa ya mwaka
unaokuja; kuhusu uhai, rizki na yote yatakayomtokea binaadamu mpaka mwisho wa
mwaka [Imesimuliwa na Ibn 'Umar, Mujaahid, Abu Maalik, Adh-Dhwahaak na
wengineo katika Salaf – Ibn Kathiyr: 8:671]
Kufanya juhudi kubwa katika
ibaada masiku haya:
Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa sallam) alikuwa inapoingia kumi la mwisho akijikaza kwa kufanya
ibaada kuliko siku zozote zingine:
عن عائشة رضي الله
عنها قالت: " كان رسول الله صلى الله
عليه وسلم يجتهد في العشر الأواخر ما لا يجتهد في غيره" مسلم
Imepokewa kwa 'Aaishah
(Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
alikuwa akijitahidi katika kumi la mwisho kuliko alivyojitahidi katika siku
nyingine zozote" [Muslim]
Na katika Al-Bukhaariy na
Muslim:
عن عائشة رضي الله عنها،
قالت: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلّم إذادخل العشر شذ مئزره، وأحيا
ليله، وأيقظ أهله (وفي رواية:) "أحيا الليل، وأيقظ أهله، وجدّ، وشدّ
المئزر" رواه البخاري ومسلم.
Imepokewa kwa 'Aaishah
(Radhiya Allaahu 'anhaa): "Ilipokuwa inaingia kumi (la mwisho) Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikaza izaar (shuka) yake, akikesha usiku,
na akiamsha ahli zake" (Na katika riwaaya nyingine) "Akikesha usiku,
akiamsha ahli zake, akijitahidi na akikaza izaar yake"
[Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwa Nini Umeitwa
Laylatul-Qadr?
Shaykh Ibn 'Uthaymiyn
(Rahimahu-Llaah) Amesema:
Kwanza: Kutokana
na uwezo; nao ni utukufu kama vile kusema “fulani mwenye uwezo mkubwa"
yaani mwenye hadhi au utukufu.
Pili: Ni usiku
ambao una majaaliwa ya mwaka mzima na huandikwa yote yatakayotokea mwaka huo,
na hii ni Hikma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kuonyesha usanifu wa
utengenezaji Wake na Uumbaji Wake.
Tatu: Usiku
huo una uwezo mkubwa kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam):
((من قام ليلة القدر إيمانا واحتسابا غفر له ما
تقدم من ذنبه)) متفق عليه
((Atakayesimama usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy
na Muslim]
Sababu Ya Kupewa Waislamu
Laylatul-Qadr:
Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa sallam) aliona umri wa Ummah za mwanzo ni mrefu, na umri
wa Ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi
elfu. [Muwatw-twaa 1/321 (Muhammad Fuad 'Abdul-Baaqy]
Ibaada Za Kufanya Masiku
Kumi Ya Mwisho:
1-Qiyaamul-Layl: (Kisimamo
cha usiku kuswali):
((من قام رمضان إيماناً واحتساباً غفر له ما
تقدم من ذنبه)) متفق عليه
((Atakayesimama (Kuswali)
Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake
yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
2-Kuosma Qur-aan:
Hasa kwa vile usiku wa
Laylatul-Qadr ndio usiku ulioteremeshwa Qur-aan kama tulivyoona katika Aayah
hizo za juu katika Suratul-Qadr na Suratud-Dukhaan. Pia Muislamu inampasa
aisome Qur-aan Ramadhaan nzima kwa sababu ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama
Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ
Mwezi wa Ramadhaan ambao
imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe Hidaaya kwa watu na hoja bayana za Hidaaya na
Al-Furqaan (Upambanuzi). [Al-Baqarah: 185]
Jibriyl ('Alayhis-Salaam)
alikuwa akimteremkia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kila usiku wa
Ramadhaan akimsomesha na kumsikiliza Qur-aan:
"كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدُ مَا
يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ
وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ
الْقُرْآنَ" رواه البخاري
Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo
mema) wa watu, na alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl
alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy]
3- I'tikaaf
Msikitini:
Kutia niyyah kubakia
Msikitini kwa kufanya ibaada humo kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
sallam) alikuwa akifanya hivyo:
عن عائشة رضي الله عنها قالت "كان
النبي يعتكف في كل رمضان عشرة أيام؛ فلما كان العام الذي قبض فيه اعتكف عشرين يوماً - أخرجه البخاري
Imepokewa kwa ‘Aaishah
(Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba: Mtume (swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)
alikuwa akifanya I'tikaaf kila Ramadhaan siku kumi, ulipofika mwaka wake wa
kuaga dunia alifanya I'tikaaf siku ishirini" [Al-Bukhaariy]
4-Kuomba Maghfirah:
Kwa sababu ni hatari mtu
atokea Ramadhaan bila ya Allaah kumghufuria madhambi!
عَنْ أَنَس وَغَيْره أَنَّ
النَّبِيّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَمَّا صَعِدَ الْمِنْبَر ثُمَّ
قَالَ (( آمِينَ آمِينَ آمِينَ)) " قِيلَ يَا رَسُول اللَّه عَلَامَ
مَا أَمَّنْت ؟ قَالَ (( أَتَانِي جِبْرِيل فَقَالَ يَا مُحَمَّد
رَغِمَ أَنْف رَجُل ذُكِرْت عِنْده فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيْك قُلْ آمِينَ فَقُلْت
آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل دَخَلَ عَلَيْهِ شَهْر رَمَضَان ثُمَّ
خَرَجَ فَلَمْ يُغْفَر لَهُ قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف
رَجُل أَدْرَكَ وَالِدَيْهِ أَوْ أَحَدهمَا فَلَمْ يُدْخِلَاهُ الْجَنَّة قُلْ
آمِينَ فَقُلْت آمِين)) صحيح الترمذي و قال الشيخ الأباني حسن
صحيح
Imepokewa kwa Anas na
wengineo kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alipopanda juu ya
minbar aliitikia ((Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn)). Alipoulizwa kwa nini ameitikia
hivyo akasema: ((Amenijia Jibriyl akasema: “Ee Muhammad, ole wake yule ambaye
unapotajwa hakuswalii, hivyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: “Ole
wake yule ambaye umeingia mwezi wa Ramadhaan kisha akatoka bila ya kughufuriwa,
kwa hiyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: “Ole wake yule ambaye
amewakuta wazazi wake au mmoja wa wazazi wake lakini wasimuingize Peponi. Hivyo
sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na kasema Shaykh
Al-Albaaniy kuwa Hadiyth hiyo ina daraja ya Hasan Swahiyh]
5-Du'aa Ya Kuomba Katika
Siku Kumi Hizi za Mwisho:
عن عائشة رضي الله عنها أنها قالت يا رسول
الله أرأيت إن وافقت ليلة القدر ما أدعو قال: ((تقولين:
اَللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌ تُحِبُّ الْعَفْو فَاعْفُ عَنِّي)) ابن ماجه و صححه الألباني
Imepokewa kwa 'Aaishah
(Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba alisema "Ee Mtume wa Allaah je,
nitakapojaaliwa kufika usiku wa Laylatul-Qadr niombe nini?" Akasema,
((Sema: Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa fa'afu 'anniy - Ee Allaah
Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe)) [Ibn
Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy]
6-Kumkdhukuru Allaah Kwa
wingi:
Kwa Tasbiyh (Kumsabbih kwa kusema;
Subhaanah Allaah) kwa Tahmiyd (kumsifu kwa
kusema; AlhamduliLLaah), Tahliyl
(kumpwekesha kwa kusema; Laa ilaaha illa-Allaah),
Takbiyr (Kumtukuza kwa kusema: Allaahu Akbar).
7- Kuomba Du'aa:
Ramadhaan ni mwezi wa
kuomba kwa sababu Aayah za kuomba du’aa zipo kati ya Aayah za kuhusu Swawm:
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ
الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ
يَرْشُدُونَ
Na watakapokuuliza waja Wangu
kuhusu Mimi, basi Mimi ni Qariyb (Yu karibu daima kwa elimu Yake); Naitikia
maombi ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate
kuongoka.
[al-Baqarah: 186]
Usiku Gani Unapatikana
Laylatul-Qadr?
Hadiyth kadhaa zimetaja
kuhusu usiku wa Laylatul-Qadr. Imetajwa kuwa ni katika masiku kumi ya mwisho;
siku ya ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano au ishirini
na saba kwa dalili zifuatazo:
عائشة أن رسول الله صلى
الله عليه وسلم قال: ((تحروا ليلة القدر في الوتر من العشر الأواخر)) رواه البخاري
Hadiyth ya 'Aiashah
(Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)
amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku za witiri kwenye siku
kumi za mwisho)) [Al-Bukhaariy]
حديث ابن عباس رضي الله
عنهما أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((التمسوها في العشر الأواخر من رمضان
ليلة القدر في تاسعة تبقى ، في سابعة تبقى ، في خامسة تبقى)) رواه البخاري
Hadiyth ya Ibn 'Abbaas
(Radhiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)
amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku kumi za mwisho za
Ramadhaan; katika (usiku wa) tisa, saba, na wa tano utakaobakia [mwisho
wa Ramadhaan])) [al-Bukhaariy]
Imaam Ahmad amepokea kutoka
kwa 'Ubaydah bin As-Swaamit kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
sallam) kuhusu usiku wa Laylatul-Qadr akasema:
((فِي رَمَضَان فَالْتَمِسُوهَا فِي الْعَشْر
الْأَوَاخِر فَإِنَّهَا فِي وِتْر إِحْدَى وَعِشْرِينَ أَوْ ثَلَاث وَعِشْرِينَ
أَوْ خَمْس وَعِشْرِينَ أَوْ سَبْع وَعِشْرِينَ أَوْ تِسْع وَعِشْرِينَ أَوْ فِي
آخِر لَيْلَة ))
((Katika Ramadhaan,
utafuteni siku kumi za mwisho, hakika umo katika siku za witiri; siku ya
ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano, au ishirini na
saba, au ishirini na tisa, au usiku wa mwisho)) [Ahmad]
Alama Zinazobainisha
Laylatul-Qadr:
1. Usiku
huo unakuwa na mwanga zaidi.
2. Upepo
siku hiyo hutulia, yaani siku hiyo hautokei upepo mkali.
3. Hali
ya hewa huwa nzuri.
4. Nyoyo
za Waumini usiku huo huwa zina utulivu kuliko siku nyingine.
5. Baadhi
ya watu wema huoteshwa usiku huo kama walivyokuwa wakioteshwa Maswahaba na
Salafus-Swaalih (wema waliotangulia)
Asubuhi Yake:
حديث أبي بن كعب رضي الله
عنه أنه قال: "أخبرنا رسول الله صلى الله عليه وسلم أنها تطلع يومئذ ٍ لا
شعاع لها" رواه مسلم
Hadiyth ya ‘Ubay bin Ka'ab
(Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)
ametuambia kuwa, jua siku hiyo hutoka likiwa halina mishale (mikali)"
[Muslim]
Pia,
((ليلة القدر ليلة طلقة لا حارة ولا باردة
، تُصبح الشمس يومها حمراء ضعيفة)) صحيح ابن خزيمة
((Laylatul-Qadr ni usiku
ulio katika hali ya ukunjufu, usio na baridi wala joto, asubuhi yake jua huwa
jekundu na dhaifu)) [Swahiyh Ibn Khuzaymah]
ليلة القدر ليلة
بلجة (أي مضيئة) لا حارة ولا باردة ، لا يرمى فيها بنجم)) (أي لا ترسل
فيها الشهب) رواه الطبراني
ومسند أحمد
((Laylatul-Qadr usiku wa
kung'aa [yaani wenye mwanga] sio joto wala baridi, na vimondo (nyota za
kufyatuliwa) havitotumwa)) [At-Twabaraaniy na Ahmad]
Tunamuomba Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kukesha masiku kumi ya Ramadhaan ili
tujaaliwe kuupata usiku huu mtukufu, tutoke katika Ramadhaan tukiwa
tumeghufuriwa madhambi yetu yote. Aamiyn
No comments:
Post a Comment