1. Kutia nia kwa kutamka: Baadhi wanaamini kuwa nia usipoitamka basi haijawa
nia. Na pia huwafunza watoto kutamka maneno ya kutia nia, au kuwaamrisha
wasikose kwenda kunuizwa msikitini na mashekhe. Itambulike kuwa nia mahali pake
ni moyoni na kutamka ni uzushi.
2.
Kufunga bila kuswali: Baadhi ya watu wanafunga bila ya kuswali au
kutimiza Swalah ipasavyo. Watu kama hawa Swawm zao hazifai kwani Swalah ni
nguzo ya Dini ya Kiislamu.
3.
Kudhani kwamba Swalah ya Taarawiyh inaanzwa siku ya kwanza ya Ramadhaan:
Hali inaanza usiku ule unaoandama mwezi. Sunnah ni Waislamu waanze kuswali
usiku huo na sio baada ya kufunga siku ya kwanza.
4.
Kuchelewa kufuturu/kufutari:
Baadhi ya watu husubiri hadi adhana imalizike na wengine husubiri hadi kiza
kiingie na hali tumehimizwa tukimbilie kufuturu. Matokeo yake ni kukiuka Sunnah
ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia huenda kufanya
hivyo wakachelewa Swalah ya Magharibi. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) anasema:
لا تزال
أمتي بخير ما عجَّلوا الإفطار –
رواه
الإمام أحمد .
((Ummah
wangu utabakia katika kheri watakapokimbilia kufuturu)) [Imaam Ahmad]
5.
Kuomba du'aa zisizo sahihi wakati wa kufuturu: Wengi wameizoea du’aa hii
na kuisoma wakati wa kuanza kufuturu, ingawa ni du’aa yenye mapokezi dhaifu
yasiyo sahihi: “Allaahumma Laka Swumtu wa 'alaa Rizqika aftwartu”.
6.
Kuacha du’aa sahihi: Du’aa hii ifuatayo ndiyo sahihi iliyohibiti wakati
wa kufuturu:
“Dhahabadh-Dhwama-u
Wabtallatil-'Uruuq, Wathabbatal-Ajru Insha-Allaah”.
Na hii ni
nyingine iliyo sahihi:
“Allaahumma
Inniy As-aluka Birahmatikal-latiy Wasi'at Kulla Shay'in An Taghfiraliy”.
7.
Kufuturu kwa vitu vya haraam kama kuvuta sigara n.k. Wanakosa kutambua
kwamba hii fursa kubwa kwa waliozoea kuvuta sigara kuacha moja kwa moja kuanzia
mwezi wa Ramadhaan, kwani ikiwa wameweza kufunga siku nzima na kujizuia kuvuta,
vipi washindwe kujizuia na usiku?
8.
Kula Futari kupita kiasi: Utakuta mtu akifuturu huwa anafanya kisasi,
anataka ale kulipiza ile njaa ya siku nzima, matokeo yake anashiba kiasi
kushindwa hata kwenda kuswali Taarawiyh.
9.
Kukithirisha Michezo na Upuuzi: Utakuta watu wakati uingiapo mwezi wa
Ramadhaan, ndio wanaanza kutoa ile michezo waliyoiweka pembeni mwaka mzima, au
kwenda kununua michezo mipya kama karata, carrum (keram), drafti, domino
(dhumna) n.k. wakicheza mchana kutwa ili kupitisha muda uende haraka. Na kisha
ifikapo usiku badala ya kwenda kuswali Taarawiyh. Wanakesha kwa kuangalia
televisheni, filamu na mipira. Na wengine wakiyaambatanisha hayo kwa kula
mirungi na kuvuta sigara. Hayo ni mambo ya haramu na yenye kuwapotezea fadhila
na baraka za Ramadhaan, wakati ambapo wangeutumia mchana wao kuchuma kwa kusoma
Qur-aan sana na kuhudhuria darsa za Dini au kusoma vitabu vya Dini, kusikiliza
mawaidha, Qur-aan au kutazama video za mawaidha n.k. Na ifikapo jioni
wangeutumia muda wao kusimamisha Swalah za usiku (Taarawiyh), na pia kupumzika
ili waweze kuwahi Swalah ya alfajiri. Gumzo lisilokuwa katika mas-ala ya Dini
jambo lililochukizwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama
usimulizi ulivyopokelewa kutoka kwa Abdullah bin Mas-uud (Radhiya Allaahu
'anhu)
((Hakuna
kupiga gumzo la usiku isipokuwa kwa mwenye kuswali au msafiri)) [As-Silsilat
Asw-Swahiyha – Al-Muhaddith Al-Albaaniy]
Na kutoka
kwa Abu Barzah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuwa akichukia kulala kabla ya 'Ishaa na gumzo baada yake) [Al-Bukhaariy na
Muslim]
10.
Kusengenya, kudanganya, kupiga porojo na kukaa mabarazani kupoteza
wakati: Wanajisahau wengi wetu kwa kupiga soga zisizo na maana na pia kusema
wenzao, kutukana, kulaani na kuongea mambo ya uongo n.k. Pia wengi wetu
wakifunga huwa na hasira sana. Huko kunapelekea mtu kupoteza ujira wa funga
yake na pia hata kuibatilisha (kwa maoni ya Maulamaa wengine), Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Ambaye hatoacha maneno ya uongo
na matendo yake, basi ajue kwamba Mwenyeezi Mungu hana haja ya yeye kuacha
chakula chake na kinywaji chake)) [ameisimulia Imaam al-Bukhaariy]
11.
Kuwachukua watoto wadogo misikitini ambao wanafanya fujo na kusababisha
kushawishi Maimaam na Maamuumiyn (wanaoswali) washindwe kupata khushuu
(unyenyekevu) katika Swalah. Mwanamke mwenye kuswali nyumbani kwa nia ya kuzuia
watoto wake wasilete madhara haya atapata thawabu zaidi kuliko kwenda msikitini
na kuleta madhara hayo. Kuwazoesha watoto msikiti ni jambo zuri kabisa, lakini
panapoonekana kuna matatizo kama hayo, basi ni bora kuwaepusha ili wasiharibu
Swalah za wengi.
12.
Kutokukamalisha Swalah ya Taarawiyh na Imaam ili kupata fadhila za
Qiyaamul-Layl kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( مَنْ
قَامَ مَعَ الإِمَامِ حَتَّى يَنْصَرِفَ كَتَبَ اللَّهُ لَهُ قِيَامَ لَيْلَةٍ))
رواه
الترمذي وصححه الألباني في صحيح الترمذي
((Atakayesimama
(kuswali) na Imaam hadi amalize ataandikiwa (fadhila za) Qiyaamul-Layl))
[Imesimuliwa na at-Tirmidhiy na kaipa daraja ya Swahiyh al-Albaaniy katika
Swahiyh at-Tirmidhiy]
13.
Kushika Mus-haf na kumfuatiliza Imaam anaposwalisha: Kufanya hivyo,
kunamkosesha mtu kuipata Sunnah ya kufunga mikono yake na pia kupoteza fadhila
za kuisikiliza Qur-aan kutoka kwa Imaam ambayo tumeamrishwa kuisikiliza
inaposomwa, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
(وَإِذَا
قُرِىءَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُواْ لَهُ وَأَنصِتُواْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ)
(Na
isomwapo Qur-aan isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa)
[Al-A'araaf:204]
14.
Kusoma tasbiyh fulani kila baada ya rakaa nne ya mapumziko: Hakuna dalili
ya kufanya hivyo. Lililothibiti ni kusoma tasbiyh mwisho kabisa unapomaliza
Swalah ya Witr kwa kusema mara tatu: “Subhaanal-Malikul-Qudduus” Kisha kwa
sauti ya juu unavuta “Rabbul-Malaaikati War-Ruuh”.
15.
Kuharakisha kula Daku: Utakuta baadhi ya watu wanawahisha Daku na kuila
saa sita za usiku au hata baada tu ya Taarawiyh, ima kwa kutaka walale moja kwa
moja hadi alfajiri au kwa sababu ya uvivu wa kuamka kwa ajili ya Daku. Kufanya
hivyo ni makosa kwa sababu kunakwenda kinyume na mafunzo ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na pia kunapelekea kuikosa ile baraka ya
Daku. Na Daku si lazima kula mlo mzito, japo tende au maji yatosha. Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((Harakisheni
kufuturu na chelewesheni daku)) [Swahiyh al-Jaami' na kaipa daraja ya Swahiyh
Shaykh Al-Albaaniy]
16.
Kudhani mwisho wa kula daku ni dakika kumi kabla ya adhana ya Alfajiri:
hivyo mtu akichelewa kula daku na ikawa karibu na dakika chache tu kabla ya
Alfajiri hujinyima daku kwa khofu kuwa Swawm yake itabatilika. Wengine wameweka
mipaka ya dakika kumi, hivyo si sawa. Mtu anaweza kula daku hadi karibu na
Alfajiri hata kunapoadhiniwa. Na pindi Muadhini akiadhini ndipo unapoanza
kufunga na Swawm yako inasihi. Na hata Muadhini akiadhini na kama una tonge au
fundo la maji mdomoni usiliteme, kamilisha kulimeza kisha ndio uanze kufunga.
Haya yamethibiti katika Sunnah kama inavyoonyesha Hadiyth ifuatayo:
Kutoka kwa Sufyaan bin ‘Uyaynah kutoka Az-Zuhriy, naye kutoka kwa Saalim
naye kutoka kwa baba yake, kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) anasema: ((Hakika Bilaal anaadhini usiku (adhana ya mwanzo), basi
kuleni na mnywe hadi aadhini Ibn Ummi Maktuum)) [At-Tirmidhy).
17.
Kudhani kwamba mtu anapoamka na janaba huwa Swawm yake haifai: Dhana hiyo
si sahihi, bali sahihi ni kuwa mtu anaweza kujitwaharisha hata baada ya kuingia
Alfajiri mradi tu aiwahi Swalah ya alfajiri isije kumpita. Na Swawm yake ni
sahihi.
18.
Kufunga ukiwa safarini: Walioko safarini kujikalifisha na kujitia
katika mashaka ya kufunga na kuacha kuchukua rukhsa iliyotolewa kufuturu; sio
jambo jema kufanya hivyo kama ilivyo dalili ya Hadiyth:
Kutoka kwa
Jaabir bin 'Abdillaah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) alimuona mtu akiwa amewekwa chini ya kivuli hali yake taabani
baada ya kudhoofika kutokana na Swawm akamwambia: (Sio katika wema (ucha Mungu)
kufunga katika safari)
[Swahiyh
Abiy Daawuud]
19.
Kutokujua Hukmu za Swawm: Baadhi ya watu hawajui Hukmu sahihi za funga
kisha huwa hawaulizi, ima kwa kuona hayaa au wakidhani wanajua. Ni vizuri mtu
aulize lile asilo na hakika nalo kwa wale wenye elimu, ile asije akakosa
fadhila na kheri hizi zipatikanazo kwa nadra mno. Na hali ya kutokujua Fiqh ya
Swawm, kama kujua mambo yenye kufunguza na yale yasiyofunguza, kunaweza
kumpelekea mtu kushinda na njaa bure huku Swawm yake ishabatilika, au kumfanya
mtu afungue na hali Swawm yake bado ni sahihi. Mfano wa mambo yasiyobatilisha
Swawm ni; kudungwa sindano, kung'oa jino, kujipulizia dawa ya pumu, wanawake
kufanyiwa ukaguzi sehemu zao za siri na daktari (gynaecology checkup) - mtu
ahakikishe anampata daktari wa kike na akiwa Muislam ndio bora zaidi, na
akikosa kabisa hapo ni dharura tena na halaumiwi - na hili si katika Ramadhaan
tu, bali ni wakati wowote mwanamke anapokwenda Hospitali awe anafanya jitihada
na kuuliza apatiwe daktari wa kike.
20.
Kumjua Allaah katika Ramadhaan pekee: Baadhi ya watu humkumbuka Allaah
katika mwezi huu tu, utakuta wanafunga na kuswali katika Ramadhaan kisha baada
ya Ramadhaan kila kitu kinasimama kana kwamba Allaah Hayupo tena! Ni vyema watu
wajue kuwa Allaah ni wa miezi yote na si mwezi wa Ramadhaan pekee.
21.
Kutamani Ramadhaan iishe: Baadhi ya watu wanahesabu masiku na wakiwa
wanaomba Ramadhaan imalizike upesi ili warejee katika hali yao ya kawaida
ambayo wanaiamini kuwa ina uhuru wa kufanya wanayoyataka. Lau angelijua mja
fadhila na kheri zilizo katika mwezi huu, hakika angetamani usiishe.
Katika
mwezi ambapo tendo dogo lakuingizia ujira zaidi ya maradufu.
Katika
mwezi huu kuna usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu.
Katika
mwezi huu vishawishi na balaa za Shetani vimewekwa mbali.
Katika
mwezi huu Malaika wametapakaa kukusanya amali zako za kheri hata za udogo wa
sisimizi
Tunamuomba
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Atuongezee elimu ya Dini Yake Tukufu ili tuzidi
kutoka katika kiza na kuingia katika mwanga utuongoze katika
Swiraatwul-Mustaqiym.
No comments:
Post a Comment