Sunday, February 17, 2013

PADRI EVARIST MUSHI AUAWA ZANZIBAR

 Ni Padri Mushi ambaye alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Minara Miwili – Zanzibar
Amepigwa risasi na watu wasiojulikana leo mida ya saa moja asubuhi akielekea kanisani
Taarifa zilizopatikana sasa hivi ni kuwa Paroko wa Kanisa la Katoliki Minara Miwili Zanzibar, Evarist Mushi amefariki dunia baada ya kupigwa risasi saa 1.00 asubuhi na kufariki kabla hajafika hospitali ya Mnazi Mmoja. Paroko huyu amepigwa risasi akishuka katika gari lake wakati akienda kuendesha ibada ya saa 3.00 leo.
Padri Evarist Mushi amepigwa risasi kichwani na kufa papohapo na watu wasiojulikana akiwa njiani anaenda kuendesha misa katika Kanisa la Mt.Theresia eneo la Mtoni Zanzibar.
Msemaji wa Polisi Zanzibar, Inspekta Mohamed Mhina amethibitisha tokeo hilo.
SOURCES: Mzalendo.net, zanzibaryetu.wordpress.com na blogs mbalimbali za Kitanzania

Saturday, February 16, 2013

MVUTANO WA KUCHINJA NYAMA MKOANI MWANZA, TANZANIA WAENDELEA


Mwanza
 
Mwanza bado wavutania kuchinja
Toleo la 280
6 Feb 2013, RAIA MWEMA
  • Nyama zadoda buchani, wanunuzi wapungua.
ULE usemi wa Kiswahili kwamba mbuyu ulianza kama mchicha unaonekana kusadifu katika mgogoro unaohusisha haki ya kuchinja wanyama na ndege kwa ajili ya kitoweo unaoendelea Mwanza na Geita kati ya waislamu na wakristo.

Tayari Umoja wa Makanisa ya Kikristo Jijini Mwanza umetoa tamko la kupinga msimamo wa serikali kuwa wenye haki ya kuchinja kwa ajili ya kuwauzia wananchi ni waislamu na wakristo wanaweza kuchinja majumbani mwao tu.

Thursday, February 14, 2013

KIFO CHA SHEIKH NASSOR ABDALLAH BACHO

Marehemu Sheikh Nassor Abdallah Bacho
 
TAFAKURI   YA  KIFO  CHA SHEIKH   NASSOR BACHU KILICHOTOKEA  ZANZIBAR TAREHE 13/2/2013.

Na  PAZI  MWINYIMVUA 

 INNA  LILLAHI  WA INNA ILLAIHI  RAJI-UUN. 



Mfahamu sheikh Nassor Bachu
Sheikh Nassor Bachu ni miongoni mwa masheikh maarufu ambaye makazi yake yalikuwa katika visiwa vya zanzibar. Ni miongoni mwa walimu ambaye ana wanafunzi wengi mno ambao msimamo wao mkubwa ni kufuata na kuhuisha sunna za Mtume Muhammad,  Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, amin.
Mchango wake katika jamii 

Katika maisha yake alikuwa akitoa darsa zake katika msikiti uliopo Rahaleo na msikiti wa Kikwajuni Zanzibar. Alipitisha maisha yake yote katika kufundisha masomo mbalimbali ya dini kama vile tafsiri za quran, hadithi na pia alikuwa na kipaji cha ziada cha kuzungumza na kueleweka kwa ufasaha. Hivyo pia ni miongoni mwa watoa mawaidha wazuri sana ambaye  kanda zake za mawaidha za redio na za video zinapatikana katika maduka mingi wanayouza kanda za dini. Pia unaweza kupata mawaidha yake kwa kupitia www.sekenke.com au tafuta kwenye www.mawaidha.com
Kwa muda kidogo alipata fardhi ya ugonjwa na hadi kukamilisha safari ya maisha yake leo siku ya tarehe 13/2/2013.
Nini tutafakari?
Kwanza napenda kunukuu maneno ya Mtume SAW aliposema katika zama za mwisho wanazuoni  wengi watapungua na maasi yatazidi.
 Ni ukweli usiopingika si rahisi kupata watu wenye ilmu kubwa kama ya sheikh wetu.
Ni wangapi wako tayari kutumia muda wao kutafuta ilmu ya dini kwa manufaa yao wenyewe sembuse kupata muda wa kuwafundisha wengine?
Ni nani yuko tayari walau kutumia saa chache kwa ajili ya kutafuta ilmu na kuweza kutumia ilmu hiyo kwa ukweli namaanisha kwa ikhlasi.
  Ibada zetu zimekuwa za kubabaisha? Kwa kuwa hatuna ufahamu wa kutosha juu ya ibada mbalimbali. Hii ni kwa sababu hatujajipangia muda wa kuhudhuria katika madrasa na kuweza kupata ilmu sahihi.
Watoto wetu tumewapangia program ambazo hawapati hata muda wa kujifunza dini yao na kumjua mtume SAW. Matokeo yake  ni mmomonyoko wa maadili.
Digrii , Masters na PHD zetu zimekuwa ni bure kwani tunashindwa hata kufanya ibada ya kutafakari na kuweza kuona  na kuthibitisha neema za Allah ambazo amezitaja katika quran pamoja na  kuhofishwa na azabu zake. Tumekuwa mstari wa mbele  wa kutaja na kueneza aibu za watu kuliko kuangalia wapi tumekosea na turekebishe.
 Hatujiulizi kwa nini?  Na mambo haya mpaka lini? Tutaanza kuisoma dini yetu lini? Masheikh wetu ndugu zangu ndio hao wanamalizika. 
Naguswa na msiba huu  sana kwa sifa za kipekee alizonazo Sheikh Nassor Bachu. Machozi hayatasaidia japo nalo hili huwezi kulizuia.
Mtu mmoja maarufu alisema wakati wa kiza kinene ndio wakati wa kutafakari na kuweza kuona mwanga. Aristotle. Tafadhali TAFAKARI.
Martin Luther anasema "Laiti kama ningejua kuwa kesho dunia yote itakatika  kuwa vipande basi nisingeacha  kupanda mti wa mtufaha". Andaa maisha ya kesho  akhera hata kama u mgonjwa kitandani au upo kifungoni NA usichoke kupanda mti wa KUTAFUTA  ilmu kwani faida zake ni nyingi.
Mtume SAW amesema
Ishi duniani kama utaondoka kesho na ishi duniani kama utabaki milele. Mihangaiko ya kutafuta maisha ni miongoni mwa sehemu ya dini lakini iendane na kutafuta  maisha ya akhera.
Na Allah SW anasema
Natunawapa muda wa kutosha lakini watambue hakika nguvu yetu ni kali? Fanya ufanyavo lakini ujue huwezi kushindana na nguvu za Allah.
Pia anasema; Kila binadamu hufanya makosa lakini mbora ni Yule anaetubia. Tufanye haraka kuomba msamaha na kutorudia makosa.
Katika aya nyingine anasema waja wema wanapofikwa na msiba husema hakika sisi tunatoka kwa Allah na kwake yeye tutarejea.
Nasi tuseme INNA LILAHI WA INNALAYHI RAJIUN. 

1. Ombi langu kwako tafuta kanda yeyote ya  mawaidha ya Sheikh Nassor Bachu katika website nilizozitaja ukurasa wa kwanza ili thawabu ziendelee kumuendea sheikh wetu na pia uweze kufaidika na ilmu yake.
 
2.     Tumia walau dakika chache kumuombea dua na kumtakia msamaha kwa Allah na amfanyie wepesi  wa hesabu zake katika safari ya maisha mapya. Allah alitie nuru na harufu njema kaburi lake. Amin. Amin
 
3.     Nasi pia tujiombee Allah atupe maisha mema ya duniani na akhera na atupe mwisho mwema.

Habari ni kwa hisani ya
NYAMBONGONAMZILIMITI
http://nyambogonanzilimiti.blogspot.com/

Wednesday, February 13, 2013

TAARIFA YA AJIRA KWA WALIMU WAPYA TANZANIA BARA MWAKA 2012/13


Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb)
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU AJIRA YA WALIMU WAPYA WA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI NA VYUO VYA UALIMU TANZANIA BARA MWAKA 2012/13

Jumla ya walimu 26,537 wameajiriwa Serikalini kwa mwaka wa fedha 2012/13. Walimu wa ngazi ya cheti walioajiriwa ni 13,568. Kati yao walimu 13,527 wamepangwa kufanya kazi katika shule za msingi zil izopo kwenye Halmashauri na walimu 41 wamepangwa katika shule za msingi za mazoezi zilizo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Jumla ya walimu wa sekondari na vyuo vya ualimu walioajiriwa ni 12,973; wakiwemo walimu wa shahada 8,887 na wa stashahada 4,086.

Walimu waliopangwa kufundisha shule za sekondari zilizo chini ya Halmashauri ni 12,893, wakufunzi wa vyuo vya ualimu ni 59 na walimu 21 wamepangwa kufundisha katika shule za sekondari za mazoezi zilizo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Aidha, idadi hiyo inajumuisha walimu 188 wa Elimu maalumu wenye Shahada ambao wamepangwa katika shule za sekondari na vyuo vya ualimu vinavyotoa Elimu maalumu.

Idadi ya walimu walioajiriwa mwaka 2012/13 imeongezeka kwa asilimia 11 sawa na walimu 2,630 ikilinganishwa na walimu 23,907 walioajiriwa mwaka uliopita 2011/12.

Kati ya walimu wa sekondari na vyuo waliyoajiriwa, jumla ya walimu 1,286 (shahada 862 na stashahada 424) ni wale walioomba ajira Serikalini kutoka soko la ajira. Hawa ni tofauti na wale waliotoka vyuoni moja kwa moja. Aidha, walimu walioajiriwa ni pamoja na walimu wa ngazi ya stashahada 841 wa mwaka 2011 waliorudia mtihani mwaka 2012 na kufaulu. Kwa upande wa walimu wa elimu ya msingi, walimu 200 kati ya walioajiriwa ni waliokuwa katika soko na kuomba ajira serikalini.

Naagiza kuwa walimu wahitimu ambao ni waajiriwa(inservice) wanatakiwa kurudi katika vituo vyao vya kazi walikokuwa wakifanya kazi kabla ya kwenda masomoni.

Orodha ya walimu na Halmashauri walikopangwa itapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (United Republic Of Tanzania - Ministry of Education and Vocational Training) na tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa–TAMISEMI (www.pmoralg.go.tz). Orodha hiyo pia itatumwa kwenye Mikoa na Halmashauri husika.

Walimu wote waliopangiwa vituo vya kazi wanaagizwa kuripoti katika Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri au Wakuu wa Vyuo vya Ualimu walikopangwa tarehe 1 Machi, 2013. Tarehe ya mwisho ya kuripoti ni tarehe 9 Machi 2013. Tarehe ya mwisho ya kuripoti imepangwa ili kuwezesha walimu wapya kuingizwa katika orodha ya mshahara wa mwezi Machi 2013. Watendaji na wasimamizi wa elimu kwenye Halmashauri na Vyuo vya Ualimu watakuwepo kuwapokea.

Walimu wote wanatakiwa kuripoti wakiwa na Vyeti vyao halisi vya taaluma, cheti cha kuzaliwa, pamoja na nakala zake ili viweze kuhakikiwa na kukamilisha taratibu za ajira zao. Waajiri, yaani Wakurugenzi wa Halmashauri na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi watawalipa walimu wapya malipo stahili kwa mujibu wa nyaraka na miongozo ya Serikali kuhusu waajiriwa wapya.

Nawatakia walimu wote waliopata ajiri hizi mpya utumishi mwema Serikalini katika Sekta ya Elimu.
Imetolewa na:
Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb)
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
13 Februari 2013

Tuesday, February 12, 2013

MAGAZETI YA LEO TAR 12/02/2013

MAGAZETINI LEO JUMANNE TAR 12/02/2013: HANDAKI NDEFU BAHARINI, PAPA BEENEDICT XVI AJIUZULU.


Monday, February 11, 2013

VURUGU ZA KIDINI GEITA

 
Majeruhi Sadick Yahya

Polisi na raiya

majeruh Said Ntahompagaze aliyejeruiwa mguu

Polisi na raiya
Imeripotiwa katika mitandao mbali mbali kuwa leo zimetokea vurugu za kidini nchini kati ya Waislam na Wakristu, katika kijiji cha Buselesele Wilayani Chato Mkoani Geita na kupelekea watu 10 kujeruhiwa vibaya huku mchungaji wa kanisa la Pentekoste Assemblies of God Mathayo Kachila (45) akipoteza maisha chanzo cha vurugu hizo kikiwa ni mvutano katika uchinjaji wa wanyama kwa ajili ya kitoweo. 

Mbali na mchungaji huyo kupoteza maisha, wengine waliojeruhiwa ni pamoja na Said Ntahompagaze(45), Sadick Yahaya(40), Yasin Rajab(56), Vicent Damon(22), wote wakazi wa Buselesele na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Ramadhani ambaye yuko mahututi katika wodi namba nane katika hospital ya wilaya ya Geita.

Kwa sasa Waislam ndio wanaotambulika kuwa na dhamana ya kuchinja katika mchinjio ya serikali.