Saturday, February 16, 2013

MVUTANO WA KUCHINJA NYAMA MKOANI MWANZA, TANZANIA WAENDELEA


Mwanza
 
Mwanza bado wavutania kuchinja
Toleo la 280
6 Feb 2013, RAIA MWEMA
  • Nyama zadoda buchani, wanunuzi wapungua.
ULE usemi wa Kiswahili kwamba mbuyu ulianza kama mchicha unaonekana kusadifu katika mgogoro unaohusisha haki ya kuchinja wanyama na ndege kwa ajili ya kitoweo unaoendelea Mwanza na Geita kati ya waislamu na wakristo.

Tayari Umoja wa Makanisa ya Kikristo Jijini Mwanza umetoa tamko la kupinga msimamo wa serikali kuwa wenye haki ya kuchinja kwa ajili ya kuwauzia wananchi ni waislamu na wakristo wanaweza kuchinja majumbani mwao tu.


Kwa mujibu wa tamko hilo, kitendo cha serikali inayosema haina dini kuwalazimisha wakristo kufuata ibada ya dini isiyokuwa ya imani yao ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19 kifungu cha 1 na 2, inayotoa uhuru wa kila mtu kuwa na uhuru wa kuabudu na kwamba suala la imani ya dini ni jambo binafsi na hiari ya mtu kulifuata.

Tamko hilo limewataka wakristo kutokula nyama zilizochinjwa kinyume na imani yao, kwa kuwa tendo la kuchinja ni sehemu ya ibada kwa waumini wa dini ya kiislamu tofauti na walivyokuwa wakifiriki mwanzoni kwamba tendo hilo halina uhusiano wowote na ibada na hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kushirikishwa katika ibada isiyokuwa ya imani yao.

“Kwa kuwa sasa imebainika kuwa tendo la kuchinja kwa wenzetu waislamu ni sehemu ya ibada kwa mujibu wa imani yao, tofauti na tulivyokuwa tukidhani hapo awali kuwa tendo la kuchinja halina uhusiano wowote na mambo ya ibada. Sisi wakristo hatuoni sababu ya kuendeea kushirikishwa katika ibada ya imani isiyotuhusu. Tunatoa wito kwa wakristo wote kuanzia sasa kutokula nyama zilizochinjwa kinyume na imani ya kikristo” ilisema sehemu ya tamko hilo lililotiwa saini na Askofu Charles Sekelwa ambaye ni mwenyekiti wa Umoja huo na katibu Mchungaji wake Jacob Kituu.
Katika kuonyesha uthabiti wa msimamo wao wachungaji na maaskofu walikutana Jumamosi iliyopita katika Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Kirumba chini ya kamati ya Ulinzi na Mwasialiano ya Umoja huo na kuazimia kuwatangazia waumini wao katika makanisa yote kususia kununua nyama kwenye mabucha katika kipindi chote ambacho watakuwa hawajapata machinjio yatakayowawezesha kuchinja kwa imani yao.

Tangazo hilo ambalo lilitolewa Jumapili iliyopita limeanza kuathiri biashara hiyo, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Umoja wa wenye Mabucha Jijini Mwanza, Joshua Machage, biashara yao imeathirika sana kwa kuwa hata waislamu wanaogopa kununua kwenye mabucha ya wakristo kwa kuhisi kwamba watakuwa wamejichinjia.

“Tatizo hili ni kubwa, kuna wanachama wangu wameleta taarifa hapa kuwa biashara haiendi kabisa kwa sababu ya mvutano huu, wakristo jana (Jumapili) wametangaziwa kutonunua nyama zinazochinjwa na watu wasiokuwa wa imani yao sasa hali ni mbaya sana kwenye biashara yetu, nyama zimesimama kabisa hali ni mbaya,” alisema Machage.
Mgogoro huo umeendelea kushika kasi pamoja na serikali kumtuma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uratibu na Sera, Steven Wassira, kusuluhisha mgogoro huo, ambaye katika kikao chake na viongozi wa dini hizo mbili alisisitiza msimamo wa serikali ambao ulikuwa umetolewa awali na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo huko Nyehunge, Sengerema ambako ndiko mgogoro huo ulikoanzia.
Sheikh wa Wilaya ya Sengerema, Ahmed Jaha Ally aliliambia Raia Mwema kwamba kwa mtazamo wa wengi na imezoeleka katika jamii kwamba muislamu hali asichochinja na kwamba mkristo akichinjia nyumbani kwake akala mwenyewe hilo haliwasumbui lakini akafafanua zaidi.
“Hilo la kuchinja nyumbani halina tabu, lakini wakichinja na kuanza kuweka kwenye mabucha hapo kunakuwa na shida kwa sababu wanaweza kununua watu wenye hoteli na kwenda kuuza, sasa akila muislamu kwenye hoteli hiyo itakuwa siyo haki, kwa sababu kwa mujibu wa maelekezo ya dini yake hapaswi kula kisichochinjwa na muislamu, ” alisema.
Akijibu kuwa kuchinja ni ibada na hivyo wasiokuwa waislamu wanashiriki ibada isiyo ya imani yao alisema kuwa hawawashirikishi wakati wa ibada na kwamba kula nyama ile si kushiriki ibada hiyo kwa kuwa hiyo inamhusu mchinjaji.
“Kwa kula tu hushiriki hiyo ibada kwa sababu inamhusu mchinjaji, kwa hiyo hatuwashirikishi lakini ndugu zetu pia wakumbuke tunavumiliana katika mambo mengi, Ijumaa ni siku ya kazi lakini Jumamosi na Jumapili ni siku za mapumziko na sisi tumekaa kimya, kwa hiyo haya mambo yanahitaji kuvumialiana” alisema Sheikh Ally.
Mwandishi wetu alipotembelea Ofisi ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza kutaka kujua msimamo wa Baraza hilo katika hali inayooendelea hivi sasa mkoani hapa kiongozi aliyemkuta ofisni hapo alisisitiza kuwa wao hawana cha kuongeza wala kupunguza kwa kuwa msimamo ulishatolewa na Waziri Wassira.
“Sisi hatuna cha kuongeza wala kupunguza, msimamo ulikwishatolewa siku ile, wewe si ulikuwapo? Ehee! Kama ulikuwapo basi sisi hatuongezi wala kupunguza kwenye hilo, na wala usininukuu, kama wao wakristo wanalo la kusema ni wao na serikali” alisema kiongozi huyu ambaye alikataa kunukuliwa gazetini.
Hayo yakiendelea mkoani Mwanza, hali si shwari pia mkoani Geita ambako uchunguzi wetu umebaini kuwa maaskofu wa Mkoa huo walikaa kikao siku ya Jumamosi wiki jana katika ofisi ya Jimbo Katoliki Geita ili kujadili suala hilo.
“Kikao hicho kilikuwa na dhamira ya kutoa tamko la kuwataka wakristo kutokula nyama zinazochinjwa na watu wasiokuwa wa imani yao na kulikuwa na mkakati wa kukubaliana kuwa na bucha au machinjio yao kwa kuwa wanaamini serikali imeamua kuegemea upande mmoja wa suala hilo,” kilisema chanzo chetu kuhusu kikao hicho cha maaskofu.


Imeelezwa kuwa hata viongozi wa kikristo walioungana na msimamo wa serikali wakati wa ziara ya Wassira walishawishiwa na serikali mkoani humo ili kuwasaliti wenzao.


Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula, alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba katika kikao hicho na Waziri Wasirra viongozi wote wa dini walikubaliana na wakatoa tamko hilo.

“Kile kikao kile kilikuwa kati ya waziri na viongozi wa dini zote na si maaskofu tu, wale waliosema ni watu wazima na wana heshima zao na ni viongozi wazito, wanawezaje kuhujumiwa? Lakini hoja hapa ni kwamba walikubaliana wakaelewana kama walishawishiwa hilo si hoja” alisema mkuu huyo wa Mkoa.

Maslahi ya Uchumi yahusishwa
Pamoja na kuhusishwa na imani, suala hilo pia limekuwa likitazamwa kwa mtazamo wa kiuchumi hasa kwa kuzingatia kuwa hiyo ni sehemu ya ajira kwa watu wanaohusika na shughuli ya uchinjaji kwa hiyo upo uwezekano mkubwa wa hilo kuchangia katika sintofahamu hii inayoendelea.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu hoja hiyo iliibuka katika kikao cha wachungaji Jumamosi wiki iliyopita jijini Mwanza ambako inaelezwa kuwa mtoa hoja mmoja alisema kuwa suala hilo limekuwa likiwanufaisha waislam kiuchumi wakati wamekuwa mstari wa mbele kuutukana na kuikashafu imani ya kikristo.

“Iliibuka hoja humo kwamba kila ng’ombe anayefugwa na mkristo anamuhakikishia muislamu shilingi elfu tano wakati wa kuchinja na katika hizo, shilingi elfu moja inachangwa msikitini na kwamba pamoja na yote hayo imani ya kikristu imekuwa ikikashfiwa bila serikali kufanya kitu, mtoa mada akasisistiza kuwa kuendelea kuchinjiwa na waislamu ni kuendelea kufadhili kukashifiwa kwa imani yao na kwa kuwa serikali imechukua upande katika hili ni bora wajisimamie,” kieleleza chanzo chetu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Mabucha Mwanza Machage anasema kuwa zamani kuchinjiwa ilikuwa ni kama huduma na ilikuwa ni bure pengine ndiyo maana hakukuwa na kelele za namna hii lakini sasa hivi imekuwa ni biashara.

“Chama change, kwa mfano, tunalipa karibu shilingi milioni moja au zaidi kwa mwezi kwa ajili ya kuchinjiwa, sasa hii ni biashara kubwa ndiyo maana hata serikali inatakiwa kuliangaliwa kwa umakini mkubwa suala hili si kulichukua juu juu tu kama inavyofanya, kwa sababu yakiingia masuala ya kibiashara inakuwa si haki kusema wengine wana haki na wengine hawana haki” alisema.

Ndikillo, Wassira wanyooshewa kidole
Mtazamo wa wengi ni kwamba suala hili limefikishwa hapa lilipo na serikali yenyewe hasa kauli zilizokuwa zikitolewa na Mkuu wa Mkoa Ndikillo huko Nyehunge wakati wa sakata hilo na kitendo cha Waziri Wassira kuunga mkono ikaonekana anakubaliana na kila kitu alichosema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

“Hili suala limekuzwa na Mkuu wa Mkoa na kauli zake za kejeli na dharau, alipokuja Nyehunge wakati wa mazungumzo ya mvutano ule, badala ya kutulia na kulichunguza jambo kwa undani alipoona hakuna maelewano alitoa amri tu kwa Polisi kuwa mkristo yeyote akichinja tia ndani, hilo liliwakwaza viongozi wa kikristo, uhalali wa amri hiyo ulikuwa unatokana na sheria ipi?” anahoji Mwinjilisti Ernest Charles wa Kikundi cha Biblia ni Jibu ambaye alishiriki katika kikao hicho.

Akizungumza na Raia Mwema mzee mmoja kutoka Nyehunge ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kuwa tangu aanze kujitambua hajawahi kuona kiongozi anashughulikia suala la mgogoro wa dini kwa jinsi alivyofanya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

“Mwanangu mimi sasa nina miaka 74, viongozi huwa wanakuwa na hekima na busara. Watu wakifarakana kwenye mambo ya dini yanatakiwa mazungumzo ya muda mrefu.

“Mkuu wetu alipokuja kwa kufoka na kutoa amri hapo aliharibu. Mambo haya yanatakiwa watu wakae na kuyazungumza tena na tena,” alieleza mzee huyo.
Chimbuko la mgogoro

Pengine Mwezi Mei mwaka jana ndiyo unaweza kuelezwa kuwa ndipo vuguvugu hili lilipoibuka wakati wa mazishi ya mzee Kamuli ambaye alikuwa muumini wa Kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT) Nyehunge.
Inaelezwa katika msiba huo ya kuwa mchungaji wa eneo hilo, James Lutambi, alichinja ng’ombe kwa ajili ya msiba huo.

Inaelezwa ya kuwa waislamu waliohudhuria msiba huo walipofika walihoji nani amechinja, wakaambiwa ni mchungaji. Wakataka kujua kwanini amechinja, yakatokea majibizano kidogo lakini waislamu hao waliondoka na kisha wakamwandikia mtendaji wa kijiji barua ya kutangaza kujitenga kushirikiana na wakristo katika misiba na sherehe, baada ya tangazo hilo, wakristo nao wakaamua kuwa na bucha yao.

Agosti 27, 2012 Umoja wa Wakristo Nyehunge ulimwandikia barua Afisa Mifugo wa Wilaya yenye kumbukumbu namba UMK/ NY/01/05 wakiomba idhini ya kuchinja katika machinjio ya Nyehunge.

Katika kujibu barua hiyo Afisa Mifugo alimwandikia mtendaji wa kijiji cha Nyehunge barua yenye kumbukumbu namba VYE/SENG/V.10/11/131 ya tarehe 02, Oktoba 2012 akimtaka kuitisha vikao vitakavyosaidia kupatikana muafaka juu ya uchinjaji wa wanyama katika machinjio ya Nyehunge, ambayo iliambatana na ufafanuzi mbalimbali wa kisheria kuhusu uchinjaji.

“Uchinjaji na ukaguzi wa wanyama kwa ajili ya kuuza kwa wananchi unafanyika chini ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 pamoja na kanuni ya mwaka 2007. Kifungu cha 7 sheria inatamka kuwa uchinjaji wa wanyama kwenye machinjio zilizoidhinishwa na serikali unafanywa kwa misingi ya imani za kidini inayokubalika na jamii husika. Sheria na kanuni zake haitamki wazi muumini wa dhehebu gani aruhusiwe kuchinja wanyama kwa lengo la kuuzia wananchi, kwa mantiki hiyo hakuna muumini wa dhehebu fulani aliye na haki ya kisheria kuchinja isipokuwa pale jamii husika inapokubaliana” ilieleza sehemu ya barua hiyo iliyotiwa saini na Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo Dk. Yohana Sagenge.

Katika kile kinachoonyesha kikao hicho kutozaa matunda wakristu waliendelea kwenda kuchinja lakini walikutana na kikwazo machinjioni ambako afisa aliyekuwa anahusika na kukagua nyama machinjioni alikataa kukagua iliyochinjwa na wakristo na hivyo wakaamua kuiuza hivyohivyo. Baada ya wakristo kuanza kuchinjia huko waislamu wakasusa kutumia machinjio hayo wakwa wanachinjia nje.

Ilipofika hapo Mkuu wa Wilaya ya Sengerema akaingilia kati na kutangaza wenye haki ya kuchinja kwenye machijio hayo ni waislam, wakristo wakaweka msimamo wa kuendelea kuchinja hali hiyo ikiwalazimu Polisi kuingilia kati na kufunga machinjio hayo kwa muda wa mwezi mmoja.
Baada ya wafanyabiashara ya nyama kulalamika, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema akaitisha kikao kingine na wachungaji ambacho kilikaa kwa zaidi ya saa kumi lakini hakikupata muafaka.

Katika kikao hicho akasisitiza kuwa kwa sasa wenye haki ya kuchinja ni waislam na kama wakristo wakitaka kuchinja wasubiri katiba mpya.

Mgogoro ulipoendelea ndipo alipolazimika kwenda Mkuu wa Mkoa ambaye ni kama alikwenda kuwasha moto zaidi badala ya kuutuliza.

Inaelezwa na baadhi ya wananchi wa Nyehunge kwamba Desemba 31, 2012 mchungaji Paul Range wa kanisa la EAGT alikamatwa na Polisi na kuwekwa mahabusu kwa kosa la kuchinja ng’ombe machinjioni na mwenye ng’ombe aliyechinjwa naye aliwekwa mahabusu kwa kosa hilo hilo.

Tukio hilo lilisababisha pia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuamuru Mtendaji wa Kijiji cha Nyehunge kufukuzwa kazi kwa kushindwa kudhibiti uchinjaji huo.

“Ndiyo maana ninakwambia Mkuu wa Mkoa amechangia sana kulikuza hili. Mchungaji alikamatwa kwa sababu ya maelekezo aliyotoa siku ya mkutano na hili likaibua hisia kali kwa watu ndiyo maana tuko hapa leo,” anasema Mwinjilisti Charles.

 Habari ni kwa hisani ya Mungu ni Mkubwa Blog.

No comments: